- M4C Pamoja Daima yatikisa
- Mbowe anusurika ajalini
HARAKATI
za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujiimarisha kupitia
operesheni mbalimbali wanazozifanya ikiwemo ya M4C Pamoja Daima zimeanza
kuwatia hofu ya kung’oka madarakani wabunge na viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Makada hao
wa CCM wakiwamo wabunge wa majimbo mbalimbali wameanza kufanya ziara
kwenye majimbo yao ili kujinusuru na vumbi lililoachwa na CHADEMA huku
wakikumbuka ziara kama hizo ndizo zilizosababisha chama chao kupata pigo
kubwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2010.
Katika
uchaguzi huo CHADEMA iliyokuwa na wabunge watano wa majimbo na sita wa
viti maalumu ilifanikiwa kupata wabunge 23 wa majimbo na wengine wa viti
maalumu pamoja na idadi kubwa ya madiwani.
Tanzania
Daima Jumapili limedokezwa kuwa hofu hiyo imewafanya makada hao kuwataka
viongozi wakuu wa CCM kuandaa ziara kwenye maeneo yaliyopitiwa na
CHADEMA ili wasipate maumivu kwenye chaguzi za serikali za mitaa
zitakazofanyika Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Operesheni
ya M4C Pamoja Daima inayofanywa na timu tatu za viongozi na makada wa
CHADEMA zilizogawanyika kwenye maeneo mbalimbali zikitumia usafiri wa
helikopta na magari zimeanza kulalamikiwa kwa kubeba gharama kubwa.
Wengi wa
wanaojenga hoja ya gharama kubwa ni makada wa CCM wanaojificha,
wanaohofia mustakabali wa chama chao, ambacho tangu uingie mfumo wa
vyama vingi hakijapata upinzani mkali kama ilivyo hivi sasa.
CCM kwa muda
mrefu imekuwa ikizoea kuona vyama vya upinzani vikianza harakati za
kujiimarisha unapokaribia uchaguzi, tofauti na hivi sasa ambapo CHADEMA
kimeonekana kuzika utamaduni huo.
Baadhi ya
makada wa CCM wanadai gharama ya kukodisha helikopta moja kwa saa si
chini ya sh milioni 2.5, hivyo kwa siku CHADEMA inatumia sh milioni 4.5
mpaka sita kwa helikopta moja.
Hoja
inayojengwa na makada hao ni kuwa, gharama hizo zisitumike kwenye
operesheni hiyo bali zipelekwe kuimarisha ofisi za wilaya, kata na
matawi ambazo zitaimarisha zaidi CHADEMA.
Hata hivyo
viongozi wa CHADEMA wameweka wazi kuwa CCM wanahofia kuimarisha CHADEMA,
si gharama zinazotumiwa na chama hicho katika shughuli zake.
Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, kwa
nyakati tofauti wamejinasibu kuwa operesheni hizo ndizo zitakazoiondoa
CCM madarakani.
Viongozi hao walibainisha kuwa demokrasia ina gharama kubwa na chama chochote kinachozikwepa hakitafanikiwa kupambana na CCM.
Wakati hofu
ikitawala kwa makada wa CCM, CHADEMA imeendelea na harakati zake ambapo
jana Mbowe, Slaa na timu zao walikuwa maeneo tofauti.
Mbowe anusurika kifo ajalini
Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa
akisafiria kutoka jijini Mwanza kwenda wilayani Ngara, Kagera kupata
ajali.
Ajali hiyo
ilitokea jana saa 6 mchana, umbali wa kilometa mbili kutoka Kata ya
Katoro, Geita na inadaiwa kuwa gari alilokuwa akitumia limeharibika
sehemu ya mbele.
Taarifa za
uhakika kutoka eneo la tukio zimeeleza kwamba chanzo cha ajali hiyo
iliyosababishwa na mwendesha pikipiki yenye namba za usajili T 212 BFR
aliyefahamika kwa jina la Sayi Kahindi (32) mkulima, mwenyeji wa Kijiji
cha Inyala kuingia ghafla barabarani.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, wakati ajali hiyo ikitokea alikuwa akielekea wilayani Ngara
kwa ajili ya mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima, iliyoanza hivi
karibuni nchi nzima.
Inadaiwa
kwamba, Mbowe katika safari hiyo alikuwa akitumia gari la Mbunge wa
Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA) lenye namba za usajili T 217 CPB.
Baada ya
ajali hiyo Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Kilimanjaro alipata gari
jingine lenye namba za usajili T 888 CGT Pajero, mali ya mkazi wa
Katoro, aliyejulikana kwa jina la Mbanju, ambalo lilimpeleka Ngara
anakoendelea na mikutano ya kukijenga chama wakati dereva na gari
lililopata ajali vikipelekwa kituo cha polisi.
Akizungumza
na Tanzania Daima Jumapili, Mbowe alikiri kupata ajali hiyo lakini
alisema yupo salama na alikuwa karibu kufika Ngara ambako alitarajiwa
kuhutubia mkutano wa hadhara.
“Niko
salama, nakaribia kufika Ngara kwenye mkutano ambapo nitaungana na
msafara wa chopa unaotokea Kigoma ukiwa na Makamu wa Zanzibar, Lema na
Mnyika,” alisema.
Naye Mkuu wa
Usalama Barabarani mkoani Geita, John Mfinanga na Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Geita, Kamanda Bwire, walithibitisha kuwepo kwa ajali hiyo
huku wakiainisha kuwa wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
“Nimezungumza
na mwenyekiti mwenyewe, Mbowe, ameniambia ni kweli alipata ajali umbali
wa kilometa mbili hivi kutoka mji wa Katoro akielekea Chato.
“Gari
alilokuwa akisafiria limeharibika vibaya maeneo ya mbele. Pikipiki nayo
imeharibika sana… wakati nawasiliana naye alikuwa ameshaondoka eneo la
tukio akielekea Bihalamuro kwenda Ngara,” alisema Mbunge wa Nyamagana,
Ezekiah Wenje.
Leo Mbowe
anatarajiwa kutua Geita kwa helikopta ili kuhutubia mikutano ya hadhara
katika mwendelezo wa shughuli za kukijenga chama chake.
Lissu awavaa Lowassa, Chenge
Mwanasheria
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na
Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratius Munishi, wamewataka makada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, Edward Lowassa
na Andrew Chenge, kuacha kutumia kigezo cha udini kutaka kuungwa mkono
kwenye harakati zao za kukimbilia Ikulu.
Lissu na
Munishi walitoa kauli hizo wakati wakimnadi mgombea udiwani wa Kata ya
Sombetini, Ally Bananga, kwenye viwanja vya Ngusero.
Lissu
alisema kuwa baada ya makada wa CCM kuona hawana sifa za uongozi
kutokana na kuwa si waadilifu wala wasafi kulingana na tuhuma za ufisadi
zinazowaandama, wameamua kukimbilia makanisani, wakiwashawishi viongozi
wa dini wawaunge mkono kwa kigezo kuwa ni Wakristo wenzao.
“Kuna makada
wengine wa CCM nao wanazunguka huko misikitini wakisema hii ni zamu
yetu sisi Waislamu, hivyo anashawishi wamchague kwa kigezo cha Uislamu
tu. Hawa watu wanasahau dini si kigezo wala sifa ya uongozi,
tuwakataeni, sijui wanalipeleka wapi hili taifa, zaidi wanatutafutia
machafuko, hawatufai wote hawa,” alisema Lissu.
Akizungumzia
muswada wa mabadiliko ya Katiba, Lissu alisema kuwa katiba inasema kuwa
nchi ni moja lakini kwa sasa kuna Maamiri Jeshi wawili, ambao mmoja ni
Mwenyekiti wa CCM, Kikwete na mwingine ni Makamu wake, Dk. Ali Mohamed
Shein, jambo alilosema kuwa ni hatari sana hasa ikitokea wakitofautiana
na kupishana kauli ilhali wote wana majeshi.
Kwa upande
wake Katibu wa BAVICHA, Munishi, alisema kuwa dawa za kulevya zimeathiri
kwa kiasi kikubwa wananchi hivyo vita yake inapaswa kuwa ya dhahiri na
ya dhati ili kuepusha madhara zaidi, hasa kwa vijana ambao ndio
waathirika wakubwa.
“Asilimia 35
ya wananchi wa Tanzania ni vijana ambao wengi wao kwa sasa
wanaangamizwa na dawa za kulevya, lakini inasikitisha Rais wetu Kikwete
alitutangazia kuwa anayo majina ya wauza dawa lakini hayataji,
kayakumbatia tu Ikulu, kama huu si usanii ni nini? Sasa tunamtaka
atueleze hao wauza dawa za kulevya ni kina nani, tofauti na hapo naye ni
mshirika wao, ndiyo maana hawataji,” alisema Munishi.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alisema kuwa endapo serikali
haitafanyia maboresho daftari la kudumu la wapiga kura kabla zoezi la
kukusanya maoni ya katiba halijafanyika, watarusha helikopta 10 kila
kanda ya chama hicho itakuwa na yake ili kuhamasisha wananchi
wasijitokeze kutoa maoni.
Alisema kuwa
haiwezekani serikali kucheza na haki za wananchi wake kiasi hicho,
kwani mara ya mwisho daftari hilo kuboreshwa ni mwaka 2010, jambo
alilosema kuwa linawanyima haki Watanzania waliotimiza umri wa kupiga
kura kama Katiba ya nchi inavyotaka.
Pia
aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea aliyesimamishwa na CHADEMA,
Bananga, awe diwani wao ili washirikiane kupigania na kusimamia
maendeleo ya kata yao, ambayo imekaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuwa na
diwani.
“Kama
mnaridhika na umeme wa mgawo mchague mgombea wa CCM, kama mnaridhishwa
na elimu inayotolewa kwa watoto na wadogo zenu kwenye shule za serikali
chagueni mgombea wa CCM. Kama mnaridhishwa na mgawanyo wa rasilimali ya
utalii, madini na gesi mchagueni mgombea wa CCM, lakini kama mnataka
mchapa kazi, mpigania haki za wanyonge, mpinga ufisadi na rushwa,
mchagueni Bananga kwa maendeleo ya kata yenu,” alisema Heche huku
wananchi hao wakipaza sauti kuwa wanamtaka Bananga.
No comments:
Post a Comment