
MKUU wa zamani wa Usalama nchini Rwanda na mkosoaji mkubwa wa Rais Paul Kagame, amekutwa akiwa ameuawa kwenye chumba cha hoteli aliyofikia, iliyopo katika kitongoji cha Sandton, mjini Johannesburg juzi. Kwa mujibu wa polisi wa Jimbo la Gauteng, Kanali Patrick Karegeya alikutwa kwenye chumba cha hoteli hiyo ya Michelangelo Towers, iliyopo Mtaa wa Maude, saa 11.30 jioni ya juzi, shingo yake ikiwa imevimba.
Taulo lililotapakaa damu na kamba pia vilikutwa kwenye sefu ya chumba cha hoteli hiyo, kwa mujibu wa Luteni Kanali Katlego Mogale.
“Kuna uwezekano amenyongwa shingo. Kesi ya mauaji imefunguliwa na polisi wa Sandton na uchunguzi uko njiani,” alisema Mogale.
Kanali Karegeya (53), ambaye ameacha mjane Leah na watoto watatu, alikuwa amepanga chumba katika hoteli hiyo Jumapili iliyopita.
Tayari lawama zimeelekezwa kwa Serikali ya Kagame kuwa inahusika na kifo hicho.
Kanali Karegeya, ambaye aliongoza Idara ya Usalama ya Rwanda, alikimbilia Afrika Kusini pamoja na mkuu wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Faustin Kayumba Nyamwasa, baada ya kutuhumiwa kula njama za kumpindua Rais Kagame.
Upinzani nchini Rwanda, umeilaumu Serikali ya Kagame kuhusika na kifo cha Karegeya, ambacho umekieleza kuwa mauaji ya kutisha.
Aidha Msemaji wa Kikosi cha Kupambana na Uhalifu Afrika Kusini cha Hawks, Paul Ramakolo, alithibitisha kuuawa kwa Karegeya.
“Tutachunguza iwapo ni matokeo ya kunyongwa shingo au sababu nyingine,” alisema.
Chama cha upinzani cha Rwanda National Congress (RNC) katika taarifa yake ya juzi, kilisema mwili wa Karegeya ulikutwa kwenye hoteli aliyokwenda kwa ajili ya mkutano.
“Kwa kuwaua wapinzani wake, utawala wa kihalifu wa Kigali unazidi kuzitishia sauti za wananchi wa Rwanda na kuzinyamazisha.
“Ni kweli,” Frank Ntwali, mwenyekiti wa chama hicho kwa Afrika aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) mapema jana. “Amenyongwa na mawakala wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.”
Msemaji wa Ubalozi wa Rwanda mjini Pretoria, hakuweza kupatikana mara moja kujibu tuhuma za RNC.
Awali Balozi wa Rwanda nchini humo, Vincent Karega, alikiambia kituo cha redio SAFM kwamba hafahamu kuwapo taarifa za mauaji hayo, lakini alikuwa akijua kuwa Karegeya amekuwa akiishi nchini humo kwa miaka kadhaa na amepewa hadhi ya ukimbizi.
“Tunazihimiza mamlaka za hapa kuliangalia suala hili kwa undani ili tujue ukweli wa kilichotokea,” alisema.
Mwaka 2011, Mahakama ya Kijeshi ya Rwanda ilitoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Karegeya, Nyamwasa na maofisa wengine waishio uhamishoni, kwa madai ya kutishia usalama wa nchi na adhabu hiyo ilitolewa wote wakiwa hawapo.
Mwaka 2010, Nyamwasa alipigwa risasi tumboni wakati akiendesha gari katika eneo la nyumba yake iliyopo katika kitongoji cha Johann.
Alinusurika kufa mara mbili katika kile familia yake ilichosema jaribio la kumuua lililoagizwa na Kagame.
Rwanda daima imekuwa ikikana kuhusika na majaribio hayo ya mauaji, lakini wakosoaji wanasema ushahidi unaonesha kuhusika kwake, ikiwamo tukio la hivi karibuni la kumteka kimafia mlinzi wa zamani wa rais katika ardhi ya Uganda.
Kanali Karegeya awali alikuwa karibu mno na Rais Kagame kwa muda mrefu, kabla wawili hao hawajatofautiana.
Aliiongoza idara ya usalama wa nje kwa muongo mmoja, kabla ya kushushwa cheo kuwa msemaji wa jeshi na baadaye kukamatwa na kufungwa jela.
Alivuliwa cheo chake cha ukanali mwaka 2006 na alikimbilia ugenini mwaka uliofuata.
Kanali Karegeya na Nyamwasa kwa sasa wameondokea kuwa wanasiasa mashuhuri kabisa wa kambi ya upinzani, pamoja na kwamba hawashikilii nyadhifa katika vyama.
Tukio hilo la mauaji linakuja miezi minne tu tangu aliyekuwa Mlinzi Mkuu wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Luteni Joel Mutabazi, atekwe na kikosi cha Jeshi la Uganda na kukabidhiwa kwa Serikali ya Rwanda.
Mlinzi huyo pia anashutumiwa na Serikali ya Rwanda kwa kutoa siri kwa Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa chini ya Majeshi ya Umoja wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) na kuwezesha kuchakazwa na kushindwa kwa kikosi cha waasi wa M23.
Kutokana na tukio hilo, hivi sasa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, imelazimika kumsimamisha kazi Mkuu wa Intelijensia wa Jeshi la Polisi, Joel Aguma, ambaye alihusika kumteka na kumkabidhi Luteni Mutabazi kwa Serikali ya Rwanda.
Hatua hiyo ya Aguma ilitafsiriwa kuwa ni mkakati wa kutii amri ya Serikali ya Rwanda, ambayo ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa mlinzi huyo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Rwanda imekiri kumkamata Luteni Mutabazi na kuzuiliwa katika jela maalumu ya kijeshi ya nchi hiyo mjini Kigali.
Post a Comment