MJUMBE
wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa
Mwesiga Baregu, amefichua siri ya madai ya usaliti ndani ya chama hicho.
Akizungumza
na Mtanzania katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es
Salaam wiki hii, Profesa Baregu alisema kiini cha tuhuma na madai ya
usaliti ndani ya Chadema ni kutoaminiana na kukosekana kwa uvumilivu.
Alisema
kitendo cha wanachama na viongozi kunyoosheana vidole vya usaliti
kinakiangusha chama na kwamba Chadema kimefeli katika mambo matatu,
ambayo ndiyo yanapaswa kuwa msingi wa chama na kama yangezingatiwa
mapema, hoja ya usaliti isingezungumzwa leo.
Aliyataja
mambo hayo yanayozalisha hoja nzito ya usaliti iliyosababisha baadhi ya
wanachama wa chama hicho kuvuliwa uanachama kuwa ni kusikilizana,
kuvumiliana na kuaminiana.
“Kukosekana
kwa mambo hayo ndio kiini cha kuibuka kwa hoja ya usaliti, hatua hii ni
mbaya katika maendeleo ya chama kinachojijengea uaminifu kwa wananchi,”
alisema.
Alisema
kuendelea kwa hali ya kushutumiana ndani ya chama kunasaidia kukitafuna
na ipo siku Chadema haitakuwa na mtu msafi, kwani wote wataitana
wasaliti.
“Chadema
ni chama kizuri cha siasa, lakini kimefeli kabisa katika kuyadhibiti
mambo hayo matatu muhimu, nadhani hili ni tatizo kubwa linalokiandama
chama hiki.
“Matokeo
ya hali hii ndiyo yanayozalisha mivutano isiyokuwa na tija, huyu kasema
hivi yule naye anasema vile, hakuna mtu wa kumsikiliza mwenzake na
kibaya zaidi watu ndani ya chama hawaaminiani, utasikia leo huyu katajwa
msaliti, kesho yule, utafika wakati chama hakitakuwa na msafi,
wanachama wote watakuwa wasaliti,” alisema Profesa Baregu.
Akizungumzia
mgogoro wa hivi karibuni ndani ya chama hicho uliosababisha Samson
Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo kuvuliwa uanachama, huku Zitto Kabwe
akikimbilia mahakamani, Profesa Baregu alisema hayo ni madhara ya
kutotumia hekima na kukosekana kwa busara ya kumaliza tofauti kwa
mazungumzo.
“Kama
hamsikilizani wala kuaminiana, lazima athari ziwepo, tena kubwa tu, kwa
sababu matukio ya namna hiyo yanakuwa endelevu, leo kashutumiwa huyu ni
msaliti, huwezi kujua mwingine atashutumiwa lini …na mvurugano
uliotokea hivi karibuni ndio uhalisia wa kile nilichokisema hapo
awali, kwamba ndani ya Chadema kumekosekana utamaduni wa kumaliza
tofauti kwa mazungumzo, kwa ujumla watu hawavumiliani wala
kusikilizana,” alisema Profesa Baregu.
Aidha
alitahadharisha kwa kusema, usaliti utakidhoofisha chama kwa kiasi
kikubwa, ambapo alikitolea mfano Chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho
kilikumbwa na mazingira kama hayo na mwisho wake kikaparaganyika ovyo
kwa sababu kila mtu alijikuta anatazamwa kuwa msaliti.
Wakati
huo huo, imebainika kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini
haijatoa mwongozo wowote juu ya barua iliyoandikiwa na Mwigamba, ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha. Mwigamba aliitaka
ofisi hiyo iingilie kati suala la kunyofolewa kinyemela kwa kipengele
cha ukomo wa madaraka kwenye katiba ya chama hicho.
Inaelezwa
kuwa Mwigamba alifikia hatua ya kuandika barua hiyo kabla hajavuliwa
uanachama, ambapo alifanya hivyo baada ya kutokea sintofahamu baina ya
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto, Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe na wafuasi wanaomuunga mkono Mbowe.
Akithibitisha
madai hayo, Mwigamba alisema ni kweli kuwa alimwandikia barua Msajili,
ambayo ilikuwa ikihoji ukiukwaji wa katiba ya chama pamoja na kuondolewa
kwa kipingele cha ukomo wa muda wa uongozi, hata hivyo mpaka sasa
hajapatiwa majibu.
Alisema
mara baada ya kuandika barua hiyo, Msajili aliwaandikia Chadema ili
kupata ufafanuzi wa madai hayo, ambapo walijibu kuwa walisambaza waraka
kwa makatibu wa chama hicho wa mikoa ili kupata uungwaji mkono kabla ya
kukiondoa.
Hata
hivyo, Mwigamba alilalamikia hatua hiyo kwa madai kuwa inakiuka katiba
na utaratibu wa chama hicho na kwamba barua iliyosainiwa na aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu, Shaibu Akwilombe, Julai 13, 2006, kwenda kwa
makatibu hao ilikuwa ikiwaarifu kuwa yanapelekwa mapendekezo ya ziada.
Kwamba
waunge mkono pendekezo kuwa Katibu Mkuu na manaibu wawili wateuliwe na
Mwenyekiti, wasipigiwe kura na majina yao yapelekwe Baraza Kuu kwa ajili
ya kupiga kura kuchagua mmoja.
“Katiba
ya mwaka 2006 isomeke pia kiongozi anaweza kuchaguliwa tena na ndiyo
walileta mapendekezo na mwanzo mpaka mwisho wa barua ilikuwa inaongelea
mapendekezo tu. Msajili alinitumia nakala ya majibu yao ili nitoe
maelezo ya ziada, ambayo pia nilishafanya hivyo tangu Desemba 30 mwaka
jana,” alisema Mwigamba.
Alisema
kuwa katika majibu ya Chadema ya Desemba mwaka jana kwa Msajili,
yalionesha wazi kwamba Mwigamba alishavuliwa uanachama wa chama hicho,
wakati alikuwa bado hajafukuzwa, ambapo walidai kwamba kipengele hicho
kilifanyiwa marekebisho.
“Nilimweleza
Msajili kuwa katiba ya Chadema, inataka mapendekezo ya katiba yapelekwe
kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, siku 30 kabla ya mkutano huo, ukizingatia
kikao cha Mkutano Mkuu kilifanyika Agosti 13, 2006 na kufanya
mabadiliko ya Katiba Julai 13, mwaka huo huo ndiyo iliandikwa barua,
sasa hata kama barua ingesafirishwa kwa ndege ama kwa usafiri wowote
lazima zingeanza kupokelewa kuanzia Julai 14 mpaka 16, hapo tayari siku
zimepungua, si 30 tena,” alisema Mwigamba.
Alisema
kuwa waraka huo uliosambazwa kwa wajumbe ulitakiwa kuwafikia siku 30
kabla na kwamba haukueleza iwapo mapendekezo hayo yaliandaliwa na Baraza
Kuu ambalo linatoa mapendekezo kwa Mkutano Mkuu au la!
Alisema
waraka huo, ambao alibahatika kuuona, ulikuwa hauna uzito unaostaili,
kwani ulikuwa sawa na barua ya uchumba ambayo ni tofauti na cheti cha
ndoa unachoweza kupeleka ushahidi Mahakamani.
Anasema
wakati barua ya Akwilombe ikisambazwa ilikuwa pamoja na rasimu, ambapo
yeye (Mwigamba) akiwa mmoja wa Makatibu wa Wilaya hakuona nakala yake.
Gazeti
hili lilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi, ili kupata ufafanuzi, hata hivyo hakuweza kupatikana, kutokana
na kuwa katika vikao, huku simu yake ya kiganjani ikiwa haipatikani.
Alipotafutwa
Msemaji wa Chadema, Tumaini Mkene, alishindwa kujibu moja kwa moja
swali aliloulizwa, ambapo alisema suala hilo lilishazungumzwa katika
mkutano wa waandishi wa habari na majibu yake yanajitoshelezi
http://www.gumzolajiji.com/
No comments:
Post a Comment