Saturday, 28 June 2014

Siri IPTL hadharani



Mbunge wa Kigoma  Kaskazini, Zitto Kabwe
WAKATI kukiwa bado na utata wa yalivyotolewa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya pamoja (Escrow) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), taarifa mpya zinazozidisha utata zinaeleza kwamba asilimia 70 ya hisa za kampuni tata ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) “zimeuzwa kwa Sh milioni sita”.

Mauzo hayo tata ndiyo msingi wa BoT kuruhusu kuchukuliwa kwa takriban Sh bilioni 200 (Dola za Marekani milioni 122) zilizokuwa zimehifadhiwa kusubiri kwisha kesi kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Fedha hizo zililipwa muda mfupi kabla ya mitambo ya IPTL kuwa mali ya Tanesco, kukiwa na ushauri wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, kusubiri.

Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kuwapo kwa nyaraka zenye utata kuhusiana na kinachotajwa kuwa ni mauzo ya sehemu kubwa ya hisa (70%) za IPTL zilizokuwa zikimilikuwa na kampuni ya Mechmar ya Malaysia kwenda kampuni ya Piperlink limited ya British Virgin Island kwa bei ya shilingi milioni sita za Kitanzania.

Tayari taarifa na nyaraka za mauzo hayo sasa zimeshavifikia vyombo kadhaa vya maamuzi na uchunguzi ikiwamo Bunge, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

CAG na Bunge wamepokea taarifa na nyaraka kutoka kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe, ambaye ametaka vyombo hivyo kufanya uchunguzi na kufanya maamuzi sahihi na ya haki.

Katika mchango wake wa Bajeti ya Serikali ya mwaka huu aliouwasilisha kwa maandishi, Zitto amezungumzia IPTL kwa kusema;

“Hisa za kampuni ya Mechmar (ndani ya IPTL) 'ziliuzwa' kwa kampuni ya Piperlink Limited ya British Virgin Island kwa bei ya Shilingi za Tanzania milioni sita. Kwa hiyo kodi ya ongezeko la mtaji iliyolipwa TRA ni ya thamani hiyo. Kampuni hiyo ya Piperlink limited nayo ikauza hisa zake kwa kampuni ya PAP kwa bei ya dola za Marekani 300,000.

“Malipo ya kodi kwa kampuni zote ( Mechmar na Piperlink) yalifanywa siku moja tarehe 6 Disemba 2013 siku moja baada ya kampuni ya PAP kulipwa fedha za Tegeta escrow (iliyopo BoT). Nyaraka zote zinaambatanishwa hapa.”

Zitto amesema katika mchango wake huo wa maandishi kwamba Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 kifungu cha 29 inataka kwanza kodi kulipwa kabla ya mamlaka za ruhusa kutoa ruhusa kwa uuzaji wa hisa kutoka mmiliki wa zamani kwenda mmiliki mpya.

“Nyaraka hizi zinaonyesha kuwa kampuni ya PAP iliingia mikataba na mamlaka za Serikali bila ya kuwa na umiliki wa kampuni ya IPTL. Pia ni dhahiri kampuni hizi za Mechmar, Piperlink na PAP zilikwepa kodi kwa kuuziana hisa kwa bei ya chee ili walipe kodi kidogo. Iweje hisa 70% za Mechmar ziuzwe kwa shilingi milioni sita wakati kampuni ina mtambo, ardhi na akiba Benki Kuu na Tanesco ya thamani ya jumla ya dola za Marekani 250m?” alihoji akitaka Waziri wa Fedha kutoa maelezo kuhusiana na suala hilo.

Kabla ya kuwasilisha bungeni maelezo hayo kwa maandishi, Zitto aliwasilisha barua kwa CAG Juni 19 mwaka huu, akiomba uchunguzi mpya wa fedha zilizotolewa BoT kutoka akaunti ya Escrow katika mazingira tata.

Zitto katika barua yake kwa CAG amesema ni dhahiri mpango mzima wa kuchukua fedha za Escrow ulichorwa na mtandao mpana ndani ya Serikali na kumtaka CAG kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa ambayo itaanika ukweli kuhusu sakata hilo.

“Utakumbuka kwamba Kamati ya PAC ilikuomba ufanye uchunguzi kuhusu uhalali wa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta kulipwa kwa kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP). Napenda kukuletea nyaraka muhimu sana zikusaidie kwenye uchunguzi wako ili kubaini ukweli wa jambo hili.

“Nakuletea barua ya TRA yenye kumbukumbu nambari TRA/DR/ILA/RE/175 ya tarehe 15/11/2013 ambapo inaonyesha kuwa kampuni ya Mechmar ya Malaysia iliuza hisa zake asilimia 70 katika kampuni ya IPTL kwa kampuni ya PiperLinks Investment Limited mnamo tarehe 9/9/2013 kwa thamani ya Tshs 6,000,000.00,” anasema katika barua yake kwa CAG.

Amesema kwamba nyaraka za malipo ya kodi zinaonyesha Mechmar walilipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh. 596,000.00 na kodi ya stempu ya Sh. 180,000.00 Desemba 6 mwaka 2013 katika Benki ya CRDB Waterfront Branch.

“Kampuni ya PiperLinks nayo iliuza hisa zake kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions mnamo tarehe 30 Oktoba, 2013. Barua ya TRA inaonyesha kuwa kodi iliyolipwa ni kodi ya ongezeko la Mtaji tshs 47,940,000.00 na ushuru wa stempu tshs 4,800,000.00. Malipo ya kodi hiyo yalilipwa siku ile ile ambayo Mechmar walilipa, tarehe 6 Desemba 2013,” anasema.

Zitto amesema katika barua yake hiyo kwamba hata amri ya Mahakama ilipotolewa kuwa PAP wapewe mali za IPTL, kampuni hiyo haikuwa na umiliki wa wowote wa IPTL.

“Katika nyaraka ninazokuletea kuna ushahidi wa kutosha kabisa kwamba hapakuwa na uhamishaji wa umiliki wa hisa za IPTL kwa PAP kwani ni dhahiri nyaraka zote zilizowasilishwa na PAP serikalini zilikuwa ni nyaraka za kughushi.

“Katika uchunguzi wako ni muhimu pia nyaraka za PAP zichunguzwe uhalali wake. Kwa mfano, TRA hawana hati halisi za hisa za IPTL ambazo ziliwasilishwa na PAP ili kuthibitisha umiliki wao. Pili, utaona kuwa iweje kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na hisa 30% katika IPTL ilipwe dola za Marekani milioni 75 wakati Mechmar iuze asilimia 70 kwa tshs milioni 6 tu na PiperLink iuze kwa dola laki tatu tu? Halafu mali mojawapo ya IPTL iliyolipwa kwa PAP ni dola za Marekani milioni 122?” anahoji Zitto 

Chanzo raia mwema

No comments:

Post a Comment