Na:

NI bahati nzuri kwamba Watanzania ni wapole. Kazi kubwa ni kubishania mpira, hapo wanaweza kushikana mashati kwa ushabiki wa mpira, lakini mambo yanayogusa maisha ya kila siku, wanakuwa wapole.
Ni watu wanaovumilia tabu za kila aina. Lakini uvumilivu huu unaweza kufikia kikomo wakati wowote. Njia pekee ya kuepusha jambo hili lisitokee, ni viongozi wetu kujifunza kuwajibika. Anayeshindwa kutekeleza yale yaliyoamriwa, basi awajibike kwa kujiuzulu!
Tukio la hivi karibuni na Jaji Werema ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, la kutaka kupigana na kumtukana Mheshimiwa Mbunge ni mfano wa upole wa Watanzania. Vinginevyo tungesema sote kwa sauti moja kwamba Jaji anayepigana, Jaji ambaye si mvumilivu hawezi kutenda haki. Mwanasheria Mkuu ambaye anataka kujichukulia sheria mkononi hawezi kuwa msimamizi na mlinzi wa sheria za Tanzania. Tungemkataa sote!
Baada ya kitendo kile na vyombo vyote vya habari vikatangaza, yeye mwenyewe angeomba kuondoka. Na kitendo cha yeye kuomba kuondoka kingemjengea heshima kubwa. Kujiuzulu kwa kuwajibika si mwisho wa maisha. Kujiuzulu kwa kuwajibika ni ukomavu wa kisiasa na ishara ya wazi ya mtu kujitambua, kutambua wajibu wake, haki zake na kuheshimu haki za watu wengine.
Yawezekana kwamba Jaji Werema, alipitiwa na kusahau kwamba yeye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, labda alisahau kwamba yeye ndiye mwenye wajibu na jukumu la kulinda wale wanaokatwa “vichwa”, wanaoonewa, wanaosingiziwa na wanaobambikizwa kesi, alisahau kwamba yeye ni Jaji, akiamua mtu anyongwe ananyongwa, akiamua mtu atoke kifungoni anatoka; hivyo ni mtu ambaye kila wakati ni lazima abaki kwenye mstari, na kujiepesha na vishawishi vya kumpeleka nje ya kazi yake; utetezi wa Spika wa Bunge unatia mashaka.
Spika alimtetea Jaji Werema, kwamba alichokozwa na Kafulila, na kwa vile na yeye ni binadamu, basi alichukia na kuanza kumshambulia Kafulila. Msimamo wa Spika ni msimamo wa serikali au ndo msimamo wa Watanzania wote wa “Upole”? Katika hali ya kawaida, Spika wa Bunge angemkemea Jaji Werema na kumkumbukusha kwamba yeye ni Jaji na Mwanasheria Mkuu.
Katika hali ya kawaida Spika angemkumbusha Mwanasheria Mkuu kuwajibika. Mpaka ninapoandika makala hii hatujasikia kauli ya Mkuu wa nchi ambaye ni Rais.
Amechukizwa au amefurahishwa na kauli ya Jaji Werema? Tunataka kusikia akimkemea au akimwajibisha. Ni lazima tufike mahali tuanzishe utamaduni wa kuwajibika. Tufike mahali, viongozi wetu watambue kwamba nchi yetu ina watu wengi wanaoweza kuwa viongozi na kuendesha mambo – wanaposhindwa au kupata doa, wasitake kulazimisha kuendelea kuwa kwenye nafasi zao kana kwamba wao wakitoka kila kitu kinasimama; kana kwamba hakuna mbadala.
Vyovyote vile kitendo cha Jaji kuonyesha hadharani nia ya kutaka kumpiga sifa yake imepungua na ni vigumu kuendelea kumwamini. Asipolitambua hili na kujiuzulu yeye mwenyewe ni lazima akumbushwe. Na makala hii ni njia moja wapo ya kumkumbusha Jaji aliyetaka kupigana wakati amefunga suti, kwamba wakati wake wa kuachia ngazi ni sasa hivi.
Yeye mwenyewe alishatamka kwenye Bunge kwamba kuna matendo ambayo huwezi kutarajia yafanywe na mtu aliyevaa suti. Yeye alitaka kumpiga Kafulila akiwa amevaa suti! Na mbaya zaidi alitaka kujichukulia sheria mkononi! Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajichukulia sheria mkononi ni hatari kubwa. Awajibike tu, ndo njia pekee ya watu wastaarabu!
Enzi za Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi alipokuwa Waziri wa Mambo ya ndani, watu walikufa kwenye mahabusu ya kule Shinyanga. Mzee, Mwinyi, hakusubiri Tume ya kuchunguza ni kwa nini watu wale walikufa ndani ya mahabusu. Aliwajibika mara moja. Kitendo hicho kilimpatia sifa na kumjengea heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania. Baadaye, alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuvaa viatu vya Mwalimu alipoamua kustaafu. Mzee Mwinyi, ni mfano mzuri katika taifa letu wa mtu anayewajibika kwa makosa yanayotendwa na wale walio chini yake.
Ni wazi kulikuwa na uzembe mkubwa hadi kusababisha vifo vya watu wa Shinyanga ndani ya mahabusu, na uzembe huo haukutendwa wala kusababishwa na Mzee Mwinyi, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa waziri mwenye dhamana, alilazimika kujiuzulu.
Ushauri wangu wa bure ni kwamba Jaji Werema, afuate nyayo za Mzee Mwinyi. Akisubiri kujiuzulu baada ya tume atakuwa amechelewa na baadhi ya Watanzania hawatamuelewa. Kitendo cha kujiuzulu baada ya kuelekezwa na Tume au kufukuzwa na Rais hakiwezi kumletea sifa na kumjengea heshima.
Ni lazima tufike mahali tujifunze vitu vya muhimu kutoka kwa ndugu zetu waliotutangulia kuendelea. Tuna tabia ya kutaka kujifunza yasiyokuwa ya msingi kutoka kwao (lugha zao, dini zao, utamaduni wao wa mavazi, chakula, michezo yao, ufundi wao, nyimbo zao, vinywaji vyao nk) na kuacha yale ya msingi kama demokrasia, ushirikishwaji, uhuru wa kusema, usawa wa kijinsia, kuwashughulikia walemavu na wanaonyanyaswa, uwajibikaji, uzalendo, kuyatunza mazingira nk.
Tunasoma kwenye nchi zao, tunatembelea nchi zao na wakati mwingine tunaishi kwenye nchi zao, lakini tunashindwa kabisa kuchota mambo ya msingi.
Tusipende kuendesha magari yao, kuvaa suti zao, kukalia viti vyao na kulalia vitanda vyao, kutumia simu ao na kusahau vitu muhimu kama uwajibikaji, uwazi na ukweli ambavyo kwao ni vya msingi. Ni bora kukubali kupoteza matumaini ya mtu mmoja mmoja, malengo na tamaa ya mtu mmoja mmoja na kusimika matumaini ya taifa, malengo ya taifa na tamaa ya taifa.
Ni bora kukubali kupoteza cheo cha mtu mmoja mmoja, utukufu wa mtu mmoja mmoja na uheshimiwa wa mtu mmoja mmoja na kusimika utukufu na uheshimiwa wa taifa.
Kwa kuwajibika na kuutanguliza uzalendo, wenzetu wamefanikiwa kuendelea, kwa nini sisi tutegemee kuendelea kwa mfumo tofauti?
Nakumbuka kule Spain, daraja la miaka zaidi ya 100 lilipovunjika, magari yakatumbukia mtoni na watu wakapoteza maisha, waziri wa ujenzi, alijiuzulu mara moja bila kusubiri tume ya kuchunguza chanzo cha ajali ile. Ni wazi daraja hilo lilijengwa zamani sana kabla hata waziri huyo hajaziliwa, lakini kwa vile lilivunjika wakati akiwa waziri mwenye dhamana ya ujenzi alilazimika kujiuzulu.
Tulisikia kule Marekani, ndege ya Rais Obama, iliporuka kwa urefu usioruhusiwa juu ya mji wa Washington, mhusika wa masuala ya anga alilazimika kujiuzulu mara moja. Hakusubiri kuhojiana na rubani kwa nini alifikia uamuzi wa kuirusha ndege ya Rais kwa kukiuka masharti ya anga. Nchi zote zilizoendelea, pakitokea aina yoyote ya uzembe – anayehusika anajiuzulu bila kushinikizwa. Ipo mifano mingi – hata hivyo si lengo la makala hii kutoa mifano. Hoja ya msingi ni kutoa ushauri wa bure! Jaji Werema ajiuzulu!

chanzo.raia mwema
No comments:
Post a Comment