Shutuma dhidi ya Tanzania DRC ni za kudharauliwa – Kikwete


Shutuma dhidi ya Tanzania DRC ni za kudharauliwa – Kikwete

TANZANIA imesema kuwa ni jambo la kusadikika na kufikirika tu kwa baadhi ya watu, kudai kuwa haiko tayari kukabiliana na vikundi vya uasi na ugaidi, vilivyobakia vikivuruga amani na kusababisha ukosefu wa utulivu ndani ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Badala yake, Tanzania inaendelea kuwa tayari kukabiliana na vikundi hivyo, kwa mujibu wa mamlaka ambayo majeshi yake pamoja na yale ya Afrika Kusini na Malawi, yamepewa na Umoja wa Mataifa (UN) ya kuvishambulia, kuvimaliza nguvu na kuvinyang’anya silaha vikundi hivyo vyote.

Nchi hizo tatu zinaunda Brigedi ya Kimataifa ya Force Intervention Brigade (FIB), ambayo ni sehemu ya Majeshi ya Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), yaliyoko chini ya Luteni Jenerali Alberto Santacruz wa Brazil.

Chini ya mamlaka ambayo Brigedi hiyo imepewa na UN, majeshi ya nchi hizo tatu, yana uhalali wa kuvishambulia vikundi vya kiasi katika DRC.

Msimamo huo wa Tanzania ulirudiwa jana na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Novisise Mapisa- Nqakula, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Afrika Kusini na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Waziri Nqakula amefuatana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, Mahlobo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akiwatakia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania Heri ya Mwaka Mpya wakati wa Hafla ya Mwaka ya Sherry Party iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete aliyaeleza maoni na shutuma dhidi ya Tanzania kuwa ni mambo ya “kudharauliwa”.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar, Rais Kikwete alimweleza Nqakula kuwa msimamo wa Tanzania umekuwa ule ule wa siku zote bila mabadiliko yoyote, yaani kuhakikisha kuwa majeshi na vikundi vyote vya uasi ndani ya DRC vinamalizwa.

Rais Kikwete amekuwa Zanzibar tangu juzi alipohudhuria sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Wako watu wanaojidai kuwa na uwezo mkubwa wa kusoma na kuelewa zaidi maoni na mtazamo wa Tanzania kuliko hata Tanzania yenyewe ….wanadai kuwa Tanzania haina nia ya kukabiliana na vikundi vya uasi katika DRC. Ni watu wa ajabu kabisa hawa kwa sababu Tanzania, kama zilivyo Afrika Kusini na Malawi, zina askari wake katika DRC chini ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza: “Tumeanza kuifanya kazi iliyotupeleka huko kwa kukisambaratisha Kikundi cha M-23. Tuko tayari kukabiliana na Kikundi cha FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda) na vikundi vingine kama vile ADF na vile vya mgambo kama vile Mai Mai. Kilichotuzuia kuimaliza kazi hii mapema ni kwa sababu FDLR waliomba kujisalimilisha wenyewe kwa hiari na wakapewa miezi sita. Sasa muda huo umemalizika.”  habari leo

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top