HII NDIYO RELI YA KWANZA KUJENGWA TANGANYIKA, soma kwa undani zaidi






MITAALA yetu imebadilika sana kiasi kwamba kizazi cha sasa hakipati fursa ya kujifunza hata historia yetu kwa undani. Ingawa wahusika wanajitetea kwamba wanakwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, lakini binafsi naamini tunakosea sana kutowafundisha vijana wetu mambo ya msingi, hususan yaliyotokea nchini mwetu kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na hata baada ya uhuru.
Binadamu kuishi bila kumbukumbu ya mambo yaliyopita kamwe hakuwezi kumfanya akabadilika na kujua nini afanye ili kuyaboresha maisha yake. Hata tunapojifunza mambo ya imani za kiroho ni historia, sasa wahusika wa elimu wanaposhindwa kuandaa mitaala thabiti kwa vizazi vyetu wanakuwa wanafanya makosa makubwa.
Ndugu zangu, leo nataka kuwakumbusha tu kuhusu usafiri mkubwa uliozoeleka wakati wa ukoloni na hata baada ya uhuru. Usafiri wa treni. Sitaki kuzungumzia historia ya usafiri huo hapa nchini, bali nitazungumzia kuhusu reli ya kwanza kabisa kujengwa ndani ya Tanganyika, au Koloni la Kijerumani Afrika Mashariki (German East Africa) kama lilivyokuwa likijulikana wakati huo likizihusisha Tanganyika (Tanzania Bara ya sasa), Rwanda na Burundi.
Kwa wale wasiojua ni kwamba, reli ya kwanza kabisa kujengwa hapa nchini ni ile ya Usambara (Usambara-Railway). Reli hii ilijengwa baada ya kuanzishwa kwa kampuni moja ya reli mwaka 1891 ikiwa na dhamira ya kuiunganisha bandari ya Tanga katika Bahari ya Hindi na Ziwa Nyanza (Ziwa Victoria) kupitia kusini mwa Milima ya Usambara. Wahusika walipanga kwamba reli hiyo iwe na geji 1,000mm (futi 3 na inchi 3 3⁄8).
Tangu Junie 1893 ujenzi wa reli hiyo ukaendelea kuanzia Tanga kwenda bara. Kutokana na ukosefu wa mtaji ilibidi kampuni hiyo itaifishwe na serikali (ya Kikoloni chini ya Wajerumani) mwaka 1899. Baada ya hapo reli hiyo ikawa chini ya Shirika la Reli la Kijerumani lililofahamika zaidi kama Ostafrikanische Eisenbahngesellschaft (East African Railway Cooperation), kampuni ambayo ilikuwa imeundwa ili kujenga na kuendesha Reli ya Kati ya Tanganyika (Zentralbahn) kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma. Kati ya Pongwe na Ngommi kwenye Reli ya Usambara kulikuwa na michepuko miwili (double hairpin turn).
Mnamo Septemba 26, 1911 reli hiyo ilifika Moshi kwenye Mlima Kilimanjaro ukiwa ni umbali wa kilometa 351.4 kutoka Bandari ya Tanga. Safari kwenye njia hiyo zilianza Oktoba 4, 1911 na uzinduzi rasmi ulifanyika Februari 7, 1912. Mwaka 1914 treni moja ilifanya safari kati ya Tanga na Buiko na kurejea kila siku na kwa siku mbili kwa wiki safari zilifanyika kati ya Tanga na Moshi. Safari nzima kwa umbali huo ilitumia saa 14 na dakika 40.
Kutoka katika stesheni ya Tengeni hadi mji wa Sigi kulikuwa na njia-panda ya reli yenye urefu wa kilometa 23.3 iliyojengwa kwa kutumia geji 750mm (futi 2 na inchi 5 1⁄2) ikiwa na michepuko minne (four hairpin turns).
Kuanzia Juni 4, 1912 – Mei 12, 1913 reli hiyo ikaitwa Reli ya Kaskazini (Nordbahn - Northern Railway) kwa kipindi kifupi. Mipango ya kuiendeleza reli hiyo hadi Arusha ilikuwa inafanywa na fedha tayari zilikuwa zimetolewa lakini haikuweza kujengwa kutokana na kuanza kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Waingereza walipoanza kuitawala Tanganyika wakaamua kuiunganisha Reli ya Usambara kati ya Moshi na Voi na ile Reli ya Uganda nchini Kenya na kuiongezea mwaka 1929 hadi katika kituo chake cha sasa cha Arusha.
Baada ya Tanganyika kupata uhuru Reli ya Kati na Reli ya Usambara zikaunganisha kati ya Mruazi na Ruvu. Wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyohusisha nchi za Kenya, Tanzania na Uganda, Reli ya Usambara ilikuwa chini ya Shirika la Reli la Afrika Mashariki (EAR). Jumuiya hii ilipovunjika mwaka 1977 Reli ya Usambara ikawa chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo nalo lilibinafsishwa mwaka 2007 na kuchukuliwa na kampuni ya RITES ya India.
Chini ya utawala wa Wajerumani mwaka 1913, Reli ya Usambara ilikuwa na injini 18, mabehewa 31 ya abiria na mabehewa 199 ya mizigo pamoja na wafanyakazi 562 ambapo 35 kati yao walikuwa Wazungu.
Baada ya kujengwa kwa njia ya kuunganisha Voi, safari kati ya Arusha, Moshi na pwani zilielekezwa kwenye bandari ya Mombasa na sehemu ya kaskazini ya Reli ya Usambara ikawa kwa ajili ya huduma za ndani. Treni la abiria liliongozwa na watumishi (DMU) wanne wakati huo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top