
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.PICHA|MAKTABA 0
inShare
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiko katika harakati za kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, uliompa ushindi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.
Zitto ambaye pia ni Mbuinge wa Kigoma Kaskazini, juzi aliibuka mshindi katika maombi yake ya kuizuia Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake, hadi kesi ya msingi kuhusu suala hilo itakapokuwa imesikilizwa.
Kadhalika, chama hicho kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, John Mnyika kimesema kinaendelea na utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu wa kutompa Zitto ushirikiano wa aina yoyote.
Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, alisema jana kuwa japo wanauheshimu uamuzi wa Mahakama, hawajaridhika nao na kwamba wanakusudia kwenda Mahakama ya Rufani kuupinga.
“Ingawa uamuzi huu ni Interlocutory (uamuzi usiomaliza kesi), lakini sisi hatukuridhika nao. Hatukuridhika na uamuzi wa kutupilia pingamizi letu la awali, hati ya kiapo na hata amri yenyewe ya zuio la muda,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
“Kuna namna nyingi za kufanya kupinga uamuzi huo, kama vile kukata rufaa, kuomba marejeo au namna nyinginezo. Kwa hiyo kwa sasa tunaangalia namna bora ya kwenda Mahakama ya Rufani bila kuathiri matakwa ya kisheria.”
Wakili Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema kuna haja ya kuiomba Mahakama ya Rufani kuuchunguza uamuzi huo kwa kuwa una athari si kwa Chadema tu, bali hata vyama vingine dhidi ya wanachama wake.
Kauli ya Mnyika
Mnyika kwa upande wake alisema kutompa ushirikiano Zitto ni uamuzi wa Kamati Kuu ambao ulitokana na hatua yake ya kwenda mahakamani kwa masuala ya chama, kinyume cha matakwa ya Katiba ya Chadema na Kanuni zake. Mnyika alikuwa akirejea taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baada ya kikao hicho akiwataka viongozi wa ngazi zote za chama hicho, wanachama, mashabiki na wapenzi wake, kutoshiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yote ya nje, ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto na mawakala wake
chanzo gazeti la mwananchi
Post a Comment