
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuanza kwa kampeni maalumu ya kisiasa itakayojulikana kwa jina la “Pamoja Daima,” itakayokigharimu zaidi ya shilingi bilioni moja kwa siku 14, huku helkopta tatu za kukodi zikitarajiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 400, imefahamika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumanne wiki hii, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kampeni hiyo itajumuisha helkopta tatu na magari ya kutosha kuzunguka karibu katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mbowe alisema kampeni hiyo ilianza rasmi Jumanne (jana) na itafikia mikoa na majimbo yote ya Tanzania Bara isipokuwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako chama hicho bado kipo kwenye mazungumzo na uongozi wa Jeshi la Polisi.
Lindi na Mtwara pekee ndipo hatujapewa fursa. Kuna zuio katika mikoa hii kutokana na kilichotokea huko nyuma. Mawasiliano na Jeshi la Polisi yanaendelea na tukipewa fursa napo tutafika.
“Katika operesheni hii ya Pamoja Daima, tuna majeshi angani, tuna majeshi ardhini. Tutaibua kashfa na maovu ya watawala. Tutawaelimisha Watanzania kuhusiana na haki zao,” aliongeza Mbowe.
Ingawa hakuweka wazi gharama zitakazotumiwa na chama chake katika kampeni hii; ni wazi kwamba hii inaweza kuwa kampeni fupi na yenye gharama zaidi katika historia ya chama hicho, ingawa pia ikienda vizuri inaweza kuwa na manufaa ya kisiasa.
Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA kwamba bei ya soko, kwa sasa, ya kukodisha helkopta kwa muda wa saa moja ni kiasi cha dola 1500 za Marekani (shilingi milioni 2.4) na zikiwa tatu maana yake, moja inaweza kugharimu kiasi cha dola 4500 za Marekani (shilingi milioni 7.2).
Kutokana na uzoefu wa siku za nyuma ambao gazeti hili linafahamu kuhusu kampeni za kutumia helikopta, aliyekodi hudaiwa kwa ule muda ambao ndege iko hewani.
“Nadhani tutakuwa hewani kwa wastani wa walau saa nne hadi tano kwa siku. Tuseme tutakuwa hewani saa nne na hivyo gharama inaweza kuwa dola 6,000 kwa siku kwa helkopta moja. Zikiwa tatu, maana yake kwa siku tunaweza kujikuta tukiwa tunadaiwa dola 18,000 (shilingi milioni 28.8),” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kitajwe jina kwa maelezo kwamba si msemaji wa chama.
Kwa hesabu hizo, maana yake ni kwamba CHADEMA kitatumia kiasi cha shilingi milioni 403.2 kwa siku 14 ambazo kitaendesha kampeni hiyo ya Pamoja Daima.
Raia Mwema limeambiwa pia kwamba wakati wa mikutano ya kisiasa iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, katika mikoa ya Tabora na Kigoma mwishoni mwa mwaka jana iligharimu kiasi cha shilingi milioni 50 kwa wiki mbili.
Kampeni hiyo ya Slaa haikutumia helikopta na hivyo gharama zake ni zile za magari, mafuta na posho za waliokuwemo katika msafara.
Kwa makisio ya safari hiyo ya Slaa, inaweza kukadiriwa kwamba CHADEMA kitatumia kiasi cha shilingi milioni 50 kwa kila mikoa miwili itakayotembelewa–na kwa vile kuna mikoa 22 itakayotembelewa (ukiacha Lindi na Mtwara), maana yake ni kwamba mikoa 11 italipiwa kiasi hicho na kufanya hesabu kufikia shilingi milioni 550. Hesabu hiyo inafanya gharama za kampeni kukadiriwa kufikia kiasi cha shilingi milioni 953.
“Utaona kwamba gharama kubwa zaidi zitatumika kwenye hayo maeneo muhimu lakini ukumbuke hii ni kampeni kubwa zaidi na hivyo kutakuwa na gharama kubwa zaidi za magari, posho za wahusika na mafuta mengi. Inaweza kabisa kufika bilioni moja,” gazeti hili liliambiwa.
CHADEMA kinapokea kiasi cha shilingi milioni 237 kama ruzuku kutoka serikalini kila mwezi na hivyo kampeni hii inaweza kutumia karibu mara nne ya mapato ya mwezi mmoja ya ruzuku.
Alipotakiwa kusema gharama halisi zinazoweza kufikiwa kupitia kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema si vema kutaja gharama hizo kwa vile ni sawa na kuweka siri za chama hadharani.
“Vikao vya kikatiba vimepitisha mikakati na bajeti ya utekelezaji. Huu si wakati mwafaka kuanika kila kitu kwenye vyombo vya habari. Nikifanya hivyo, itakuwa sawa na kueleza siri za mapambano mbele ya adui wakati uko katikati ya vita,” alisema.
CHADEMA imekuwa na utaratibu wa kukodi helikopta zake kutoka kwa mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu wa Kenya, Simeone Nyachae.
Hata hivyo, si CHADEMA pekee ambayo imekuwa ikiingia gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli zake za kisiasa nchini, vyama vingine vinavyotumia kiasi kikubwa cha fedha ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM).
- See more at: http://raiamwema.co.tz/helkopta-chadema-zaidi-ya-ruzuku#sthash.stQWY08O.dpuf
Post a Comment