
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa, amesema wapo baadhi ya viongozi wa dini wanaodhani chama hicho ni cha kikabila lakini pia wapo Watanzania wanaodhani chama hicho ni cha kidini.
Kwa kuzingatia hayo, Slaa ameendelea kupingana na hoja iliyosambazwa kwa muda mrefu, kwamba chama hicho kinaendekeza udini na ukabila, na badala yake, akasema ni hoja isiyo kweli na nyepesi, isiyoweza kutatua shida za wananchi masikini.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Slaa, si vizuri kutumia muda wa Watanzania kujadili suala lisilo na uhalisia.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga, Dk. Slaa alisema wapo pia baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaogawa wananchi kwa kueneza propaganda hizo za ukabila na udini.
Katika hatua nyingine, aliendelea kusisitiza wanachama wa CHADEMA watakaomuunga mkono Zitto Kabwe ikiwa ni pamoja na kuandaa shughuli zake za kisiasa wataadhibiwa.
“Hao wafuasi wa Zitto kama wanashabikia mtu basi mtu huyo hatambuliwi na CHADEMA tena. Natoa tahadhari kwa wale watakaokuwa wanaratibu shughuli zake kama mapokezi kwa kumpa heshima ya mwanachama wa CHADEMA wamfuate yeye na si CHADEMA tena. Hastahili kupewa ushirikiano na wanachama wa CHADEMA kwa vile hatumtambui,” alisema.
Hata hivyo, hakufafanua nafasi ya Zitto ndani ya Jimbo lake la Kigoma Kaskazini, ambako yeye bado ni mbunge kutokana na tiketi ya CHADEMA. Hakufafanua kama ni makosa kwa chama kumzuia mbunge kufanya shughuli zake kwa kushirikiana na wenzake jimboni
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kuna-upotoshaji-mkubwa-%E2%80%93-slaa#sthash.NsmoqyHC.dpuf
Post a Comment