
Dodoma. Madai ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge hilo yamegonga
mwamba, Mwananchi limebaini.
Habari kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ili
kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe
wa kamati hiyo hawakuona sababu ya kupendekeza posho hizo kupandishwa.
Taarifa hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia
uamuzi huo baada ya kupitia viwango vya posho vinavyolipwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.
Pia kamati hiyo ilichambua viwango vya posho
walivyolipwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viwango vya
posho ya kujikimu vya Sh80, 000 kwa siku wanavyolipwa watumishi wa
Serikali.
“Hili jambo linahitaji busara sana na kutazama
mazingira ya nchi pia, kwa hiyo wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango
vya posho vya taasisi mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha,” alisema
mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Mjumbe mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa,
alisema kuwa watakaa leo kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya
kuikabidhi kwa Mwenyekiti Kificho.
Alisema pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge,
lakini isingekuwa rahisi kuongeza posho katika mazingira ya sasa, ambapo
wananchi wanalia hali ngumu ya maisha.
Wajumbe hao walioteuliwa na Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho ni William Lukuvi, Mohamed Abood
Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Awali, taarifa kutoka ndani ya Bunge zilidokeza
kuwa wajumbe hao walikuwa wakutane jana saa 9:00 alasiri ili kuandaa
ripoti itakayopelekwa kwa Kificho ikiwa imebeba ushauri kuwa kiwango cha
sasa cha posho kinatosha.
Sh300,000 wanazolipwa wajumbe wa Bunge Maalamu la
Katiba zinajumuisha Sh80,000 kwa siku ambayo ni posho ya kujikimu na
Sh220,000 kwa siku kama posho maalumu ya kuhudhuria kikao.
Posho maalumu ya Sh220,000 inajumuisha posho ya
dereva inayopaswa iwe kati ya Sh40,000 na Sh45,000 kwa siku, usafiri wa
ndani (mafuta ama teksi), mawasiliano na matumizi mengine binafsi.soma zaidi...............
Post a Comment