SABABU KWA NINI CHADEMA HAIPASWI KUGOMEA BUNGE LA KATIBA KWA SASA







BUNGE la Katiba ndio limeanza. Kama mambo yote yataenda vizuri basi Bunge hili litalipatia taifa rasimu ya Katiba ambayo Watanzania wataipigia kura ya maoni kama wanaikubali au wanaikataa.

Kama zaidi ya asilimia hamsini ya wapiga kura watachukua uamuziwa upande wowote kati ya hizo basi matokeo yake ama yatakuwa ni kuwa na Katiba mpya au kuendelea kutumika kwa Katiba ya sasa.

Tayari kumeshatokea mgawanyiko wa maoni ambao unaashiria kuwa mchakato huu wa Katiba mpya utakuwa mgumu zaidi kwa kadiri tunavyoendelea hasa kwa vile Upinzani na Chama tawala vimeshachukua misimamo tofauti kuhusiana na mojawapo ya masuala mazito kabisa yanayohusiana na Katiba mpya – Muundo wa Serikali Tatu, yaani ile ya Tanganyika, Zanzibar na ile ya Shirikisho.

Upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamechukua msimamo wa kutaka kuundwa kwa serikali tatu huku Chama cha Mapinduzi kinataka mwendelezo wa Serikali mbili za sasa.

Msimamo wa Upinzani unaonekana kupata nguvu kwa mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Katiba mpya iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba ambayo ilipendekeza muundo waserikali tatu.

Warioba na baadhi ya wanasiasa wengine wakongwe na wa upinzani wanaamini kabisa kuwa mfumo wa kuweza kuukoa Muungano ni mfumo waserikali tatu huku wakijitahidi sana kuzima jitihada za wanasiasa wengine ambao wanaamini kuwa pendekezo hilo ni pendekezo la watu wachache na ambalo linaonekana kuua Tanzania.

Hawa wanaamini yale maneno ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa “Kuifufua Tanganyika niKuiua Tanzania”.

Wenye kutaka mfumo wa serikali tatu kimsingi wanataka kuwaridhisha wale wananchi wa Tanganyika ambao wanaona kuwa mfumo wa sasa wa Muungano umekuwa ukibingirita kuwaridhisha Wazanzibari ambao licha ya kuwa na serikali yao wamekuwa na uhuru mkubwa wa kuendesha mambo yao na alama zao za kitaifa kuliko wale wa Tanganyika hivyo kuirudisha Tanganyika ni kujaribu kuwa sawa na Wazanzibari.

Upande wa CCM wao wanaaamini kuwa mfumo wa sasa wa nchi moja serikali mbili za kitaifa ni mfumo sahihi. Wanaamini kuwa kutokana na ukubwa wake na uwezo wake Tanganyika haiwezekani kuonekana imemezwa na Zanzibar lakini Zanzibar isipolindwa historia yake na alama zake mbalimbali basi itaonekana imemezwa na Tanganyika. Hii pia ni hofu ya baadhi ya watu huko Zanzibar ambao wanaamini kuwa Zanzibar imemezwa na Tanganyika na kuwa Tanganyika imekuwa na nguvu kubwa ya kuamua maisha ya kisiasa na vingenevyo ya Zanzibar kiasi kwamba baadhi yao wanaona Tanganyika kama ni “Mkoloni” na hawa hawajifichi kusema hivyo.

Hivyo wanaamini njia pia ya kujaribu kuleta aina fulani ya usawa ni kurudisha Tanganyika na kutoka hapo kuwa na muundo wa Shirikisho ambapo nchi mbili zenye utawala wake na mamlaka zake zitaweza kushirikiana pamoja katika mambo fulani fulani ambayo yameanishwa kwenye rasimu ya Katiba.

Misimamo hii inaonekana kugongana kwani kwa kuangalia mfumo wa Bunge la Katiba ni wazi kuwa wajumbe wenye mrengo wa KiCCM ni wengi zaidi kuliko wale wa upinzani. Kama – na hapa naweza kusema KAMA – wajumbe wa Bunge hili wataendesha majadiliano na upigaji kura wao kwa misingi ya kichama ni wazi kuwa wanaotaka serikali tatu watashindwa!

Watashindwa kwa sababu Sheria inayosimamia mchakato huu, ambayo wapinzani waliipinga lakini wakakubali kushiriki, imeweka mfumo ambao unahakikisha kuwa wana CCM ni wengi zaidi kwenye Bunge hili kuliko vyama vingine vyote vikijumlishwa kwa pamoja. Ni katika kulielewa hili ndiyo maana naaamini kuwa si haki, sahihi wala vyema kwa CHADEMA au wapinzani kugomea mchakato huu sasa ukiwa umeingia kwenye Bunge la Katiba kwani walikubali kuingia uwanjani wakijua sheria za mchezo na hivyo wawe tayari kukubali matokeo ya mchezo huo!

CHADEMA na vyama vingine na hata makundi mengine yasiyo na vyama hawana haki kuwakatalia wana CCM kutumia wingi wao kwenye Bunge la Katiba ati kwa sababu hoja yao ya serikali tatu inaweza kukataliwa. Hii si haki. Si lazima serikali tatu ikubaliwe na Bunge la Katiba ili mchakato uwe halali!

Sheria iko wazi ikihakikisha uhuru wa mijadala na kama hivyo ndivyo itakavyokuwa – kama ilivyo katika Bunge la kawaida – basi wengi itabidi wapewe hata kama kile wanachopewa tutakiona kuwa si haki yao au si sahihi lakini kama wamecheza kwa kufuata sheria ambazo wote tumezikubali kwa nini tukatae magoli ati kwa vile yamekuwa mengi?

Wapinzani hawawezi sasa kujitoa kwenye Bunge la Katiba kwa kisingizio kuwa ati mjadala umetekwa na CCM! Kina Christopher Mtikila na wengine wanaotaka Tanganyika wakikataliwa hawawezi kujitoa kwani utakuwa ni kuonyesha kilele cha unafiki wa kidemokrasia!

Kama walikubali refa, walikubali sheria, walikubali uwanja na wakakubali hata magoli yalivyo sasa wanapoona wanafungwa wakate kwanini? Lakini pia si lazima serikali tatu ziwe ndilo suluhisho pekee; kwa miaka 50 tumekuwa na serikali mbili pamoja na matatizo yake yote na inawezekana kabisa hata tutaendelea kuwa na serikali mbili kwa miaka 50 mingine hadi wajukuu na vitukuu vyetu vitakapokuja kusahihisha makosa yetu!

Lakini kujaribu kuteka mchakato huu kama vile maharamia wa Kisomali na kudai kuwa ati wasipokubali basi tutagoma si sahihi, ni kama kuteka nyara mchakato wa kisiasa.

Njia pekee ambayo CHADEMA na wengine ambao wanaona kuwa hoja zao zitamezwa kwenye Bunge la Katiba, na hili linawezakana likatokea sana, ni kwa wao kujitahidi kushawishi wananchi wengi zaidi juu ya nguvu ya hoja yao. Na endapo rasimu ya Katiba ambayo wao – CHADEMA na wengine – hawaikubali itapitishwa na Bunge la Katiba basi ni jukumu lao kuwashawishi wanachama wao na Watanzania wengine kuikataa kwenye sanduku la kura.

Ikumbukwe kuwa ili rasimu ya Katiba ipite kwenye kura ya maoni ni lazima ikubaliwe pande zote mbili za Muungano! Na upande wowote usipofikia idadi inayotakiwa basi rasimu haitapita.

Kama CHADEMA na wengine wataona kuwa mwisho wa siku rasimu inayopendekezwa na Bunge la Katiba si ambayo wao walitarajia mwisho wa vikao, wana nafasi moja ya kuwaambia Watanzania kuwa wasiikubali rasimu hiyo na kuwa watawashawishi kwa nguvu zote kuikataa.

Hawapaswi kutoka bungeni au kuachia ngazi ati kwa vile hawakubaliwi hoja zao. Itabidi wagangamale tu hadi mwisho! Waliamua kuyavulia nguo maji, sasa wayaoge! Hata kama ina maanisha kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika Soma zaidi...............

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top