Ubunge Chalinze mikononi mwa JK











*Wanasiasa waanza kupigana vikumbo
*Maneno, Madega, Ridhiwani watajwa
BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kuwania ubunge katika Jimbo la Chalinze, wilayani Bagamoyo, MTANZANIA Jumamosi limebaini.

Harakati za wanasiasa hao zimeanza, huku zikiwa zimepita siku chache tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo, ambaye alizikwa Ijumaa wiki iliyopita.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, baadhi ya wanasiasa na wapambe wao wameanza kampeni za chini kwa chini, ili kufanikisha mbio zao katika uchaguzi mdogo utakaotangazwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wanachama wa chama hicho wanaotajwa kuwania kiti hicho kilichowazi ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Ramadhan Maneno, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2005 hadi 2010 kabla ya Bwanamdogo.

Wengine ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (MNEC), ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, Imani Madega, Nassoro Duduma na Magreth Kikwete.

Wengine ni Gilbert Mahenge, Abdrahaman Waziri, Mwanamanga Maduga na Mwajuma Mchuka, ambapo mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Madega na Maneno.

Akizungumza na gazeti hili, Madega alithibitisha kuingiza jina lake katika kinyang’anyiro hicho muda ukifika na kwamba anachosubiri kwa sasa ni Tume ya Uchaguzi kupuliza kipenga.

“Ni kweli kabisa kama unavyosema, niko tayari kwa mapambano, nawaomba wana Chalinze na hasa wanachama wenzangu wa CCM kunipa fursa ya kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Chalinze.

“Nawaomba ili kuweza kurithi na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na kuendeleza miradi yote ya maendeleo iliyoachwa na marehemu Bwanamdogo,” alisema Madega.

Naye Ramadhan Maneno akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigoma, bila kumung’unya maneno, alisema suala la yeye kugombea si swali la kuuliza, kwani dhamira yake ya kuwania jimbo hilo ipo wazi.

“Chalinze mimi ni nyumbani na ukumbuke mimi ndiye nilimwachia kiti Bwanamdogo, mimi nakuja kugombea kama mbunge niliyeanza na si kama mtu mgeni,” alisema.

Kwa upande wake Ridhiwani, alipotafutwa kuzungumzia mbio hizo alikanusha taarifa hizo na kujibu kwa kifupi. “Hakuna ukweli wa jambo hilo,” alisema katika ujumbe wake.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za Bagamoyo wanasema, Ridhiwani hapewi nafasi kubwa, hasa kutokana na umri wake, lakini pia jina lake kuingizwa katika kinyang’anyiro hicho inatajwa kuwa italeta picha hasi katika familia ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hatua hiyo itaonekana kama ni uongozi wa kisultani katika jimbo hilo, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Kikwete alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu mbili mfululizo.

Rais Kikwete alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 10 kutoka mwaka 1995 hadi 2005, alipoachana na ubunge na kuamua kugombea urais, ambapo baada ya hapo, jimbo hilo liliongozwa na Ramadhan Maneno.

Wanasema kuwa, Rais Kikwete hawezi kukubaliana na wazo la mwanae kuwania ubunge katika Jimbo la Chalinze katika kipindi hiki ambacho yeye yupo madarakani.

Hata hivyo, habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, hivi karibuni Rais Kikwete aliwaita wajumbe wa kamati za siasa za Wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani, katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutuliza upepo.

Chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa Rais Kikwete alifanya kikao na wajumbe hao katika Kijiji cha Msoga, wilayani Bagamoyo, ambapo alikula nao chakula cha jioni.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, katika kikao hicho, Rais Kikwete alisisitiza sana suala la wanachama wa chama hicho kuacha kuparurana itakapofika wakati wa mchakato wa kumtafuta mrithi wa Bwanamdogo.

“Ni kweli kabisa Mheshimiwa Rais alituita Msoga na kutusisitiza sana hili kwa kuwataka wanachama wa CCM watakaojitosa katika kinyang’anyiro hicho kuacha kuparurana wakati ukifika,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema kuwa licha ya Rais Kikwete kusisitiza juu ya umuhimu wa wanachama wa chama hicho kuvumiliana na kuheshimiana, pia aliwataka kuacha tabia ya ‘upopo’, ambapo mchana wanakuwa wana CCM na usiku wanakuwa vyama vya upinzani.

Wachambuzi hao wanasema siasa za Jimbo la Chalinze zinategemea sana ushawishi wa Rais Kikwete, wakisema kuwa mgombea atakayeungwa mkono na Rais Kikwete ndiye mwenye nafasi kubwa ya kushinda

 http://www.mtanzania.co.tz/

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top