
Iringa. Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Rose Kamili amedai kupigwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati walipomkamata na kumshikilia kwa muda kwa tuhuma za kutoa rushwa.
Mbunge huyo kwa sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa akitibiwa majeraha yake na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kwa sasa wanasubiri taarifa ya uchunguzi ili kuamua kama ahamishiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au KCMC.
“Wamenipiga, wamenidhalilisha vya kutosha,” alisema mbunge huyo huku akitokwa na machozi. “Walipanua miguu yangu na kunikanyaga sehemu za siri. Kama angekuwa mwanamume sijui angekuwa katika hali gani?”
Alisema vitendo hivyo vilifanywa na walinzi wa CCM, wanaojulikana kwa jina la Green Guard, ndani ya ofisi ya chama hicho Mkoa wa Iringa na vilishuhudiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Iringa, Jesca Msambatavangu.
Muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, Kamili aliliambia gazeti hili kwamba wafuasi wa CCM walimteka wakati akitoa maelekezo kwa mawakala wa Chadema waliokuwa wamepangwa kusimamia uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kalenga.
Mbunge huyo alisema aliporwa Sh350,000, Pauni 500 za Uingereza, simu mbili; moja aina ya Nokia na nyingine Samsung, pamoja na nakala 16 za daftari la wapigakura ambazo walikuwa wapewe mawakala waliokuwa kwenye mkutano.
Wakati kukiwa na tuhuma utekaji uliofanywa na wafuasi wa CCM, Msambatavangu alikiri jana kuwa chama hicho tawala kilimshikilia kwa lengo la kumuhifadhi hadi polisi walipofika, lakini akakanusha madai ya kuhusika kwa wafuasi wa CCM katika tukio hilo.
“Siyo kweli. Ni madai ya uongo na kama anadai hivyo tusubiri uchunguzi wa polisi ili ukweli ujulikane,” alisema Msambatavangu.
Kamanda wa Polisi wa Iringa, Ramadhani Mungi alikiri kuwa polisi walimkuta Kamili kwenye ofisi za CCM za mkoa na kwamba waliondoka naye baada ya kupewa taarifa na makada wa chama hicho kwamba alikutwa akitoa fedha.
“Askari wetu waliokuwa kwenye msafara wa mgombea wa CCM waliporudi, maana ilikuwa jioni, walimkuta huyo mtuhumiwa akiwa kwenye ofisi za chama hicho ndipo walipompeleka kituoni,” alisema.
“Tuliambiwa amekutwa akitoa rushwa, lakini alipofika kituoni naye akadai kwamba alitekwa, kupigwa na kudhalilishwa. Sasa tumefungua majalada ya kuchunguza tuhuma zote mbili – suala la rushwa na madai yake ya kutekwa.”
Kamanda Mungi alisema polisi hawafahamu mbunge huyo alikaa kwa muda gani kwenye ofisi za CCM kabla ya wao kumchukua.ENDELEA....................
Post a Comment