
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amewashukia wajumbe wa Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliogomea kuendelea na mchakato wa kutengeneza Katiba, akisema wanapanga kuivuruga nchi.
Lukuvi alikwenda bungeni mjini Dodoma kwa kazi maalumu ya kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake aliyoitoa kwenye Kanisa la Methodist kwamba hoja ya serikali tatu ikipita inaweza kulifanya jeshi kuchukua madaraka, ambayo imeibua hisia kali kutoka kwa wana Ukawa.
Akizungumza bila kuwapo wanachama wa Ukawa waliosusia Bunge kuanzia juzi, Lukuvi alikishutumu Chama cha Wananchi (CUF), kwamba kimekuwa kikijiita ni chama cha siasa wakati ni kundi la Uamsho ambalo linasumbua Zanzibar.
Alisema kauli za Ukawa kwamba Rais Jakaya Kikwete atapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu The Hague, Uholanzi haiwezi kutokea badala yake watakwenda wao katika mahakama hiyo kwa kujihusisha na Uamsho.
Alisema ameamua kusema kile alichokichangia katika kanisa hilo wakati wa kusimikwa kwa Askofu Joseph Bundala kwa kuwa hana tabia ya unafiki na alitaka maneno hayo yarekodiwe kwenye kumbukumbu za Bunge.
“Nayasema yote haya kwa kuwa naamini huo ndiyo msimamo wangu na utakuwa msimamo ambao wakati wote utaendelea kuwa hivyo na ninawataka ndugu zangu kuacha unafiki,” alisema.
Alikanusha madai kwamba ni mchokozi badala yake akarusha tuhuma hizo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.
Alinukuu hotuba ya kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Zanzibar aliyoitoa mwezi uliopita katika Uwanja wa Kibandamaiti Zanzibar kwamba imekuwa ikipotosha hotuba ya Rais Kiwete kwa sehemu kubwa kuhusu mchakato mzima wa Katiba.
Lukuvi pia aliituhumu Ukawa kwamba imepanga kuigawa Tanzania katika vipande, kwamba Zanzibar itatawaliwa na CUF, Tanzania Bara na Chadema halafu CCM ipewe urais wa Muungano.
“Kutokana na hilo, nani ambaye hatakuwa na wasiwasi juu ya haya mambo? Nataka niwahakikishieni katika Katiba hii hakuna chombo chochote wala mtu yeyote atakayenizuia kusema ninachokiamini ilimradi nasema ukweli na ninayoyaamini,” alisema.
Alisema kama maneno yake yamewachukiza zaidi wapinzani, basi waendelee kugoma zaidi alichofanya kilikuwa kwenda kusimamia masilahi ya serikali mbili zenye masilahi kwa wananchi.
Lukuvi alisema wakati wote wananchi hawataki serikali tatu, bali wanataka maendeleo ikiwamo maji, barabara na vitu vingine lakini vyote viwe kwa kupitishwa kwa serikali mbili.a endelea
Post a Comment