
WINGI “jeusi” bado limetanda kuhusu alipo mtuhumiwa wa kesi ya kuwatorosha wanyama hai 130 wakiwemo Twiga wanne, Kamran Ahmed (32), ambaye ni mtuhumiwa namba moja katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Kilimanjaro.
Kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo na wengine watatu ambao ni Watanzania ilitajwa Aprili 17 mwaka huu mjini Moshi na mtuhumiwa huyo hakutokea tena mahakamani hiyo ikwa ni mara ya tatu, hali inayotia shaka kuwa huenda ametoroka.
Tayari mahakama ya hakimu mkazi imetoa hati ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo popote alipo baada ya kutokuonekana mahakakani kwa zaidi ya mara tatu bila ya taarifa yoyote.
Lakini taarifa ambazo Raia Mwema imezikusanya kutoka vyanzo mbalimbali zinadai kuwa mtuhumiwa huyo hajulikani aliko na juhudi za polisi ambao wamepewa hati ya kumkamata bado hazijafanikiwa.
Kamran ambaye ni raia wa Pakistan na watuhumiwa wengine watatu ambao ni Watanzania wanakabiliwa na kesi ya kuhusika kutorosha wanyama hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro na kesi hiyo ilikuwa inaendelea kusikilizwa.
Wanyama hao wanadaiwa kutoroshwa kwenda Doha nchini Qatar, Novemba 26 mwaka 2010 kwa kutumia ndege ya Qatar Emir Air Force ambayo inamilikiwa na jeshi la nchi hiyo iliyokuwa inatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake, walikuwa nje kwa dhamana baada ya awali kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro lakini Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ilimpa dhamana baada ya wanasheria wake kukata rufaa.
Hata hivyo, wakati hakimu Kobelo anayesikiliza kesi hiyo alipoitaja tena mahakamani Aprili 17 mshitakiwa huyo hakutokea mahakamani kama ilivyokuwa kwa wakili wake, Edmund Ngemela.
Hali hiyo ya kutoonekana mahakamani imeongeza shaka kwenye mustakabali wa kesi hiyo kutokana na msingi kuwa Kamran alikuwa mshitakiwa muhimu kwa waendesha mashitaka wa serikali.
Hakimu Kobelo aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 6 mwaka huu ambapo itandelea kusikilizwa tena akiutaka upande wa Jamhuri kuleta mashahidi wake.
Akizungumza muda mfupi baada ya kesi hiyo kuahirishwa moja wa washitakiwa aliyekuwa mbia wa kibiashara na mtuhumiwa huyo Hawa Mangunyuka aliimbia Raia Mwema kuwa hana mawasiliano yoyote na mtuhumiwa huyo.
“Sina taarifa zake zozote, kuhusu mtuhumiwa unayeniuliza habari zake na wala hatuna mawasiliano kwa muda,” alieleza Mangunyuka.
Katika masharti ya dhama kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Jaji Mosses Mzuna, alitoa masharti sita ya watuhumiwa kupata dhamana na kufafanua kuwa sheria ya Uhujumu Uchumi ikisomwa pamoja na ile ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) inataka mshitakiwa anayeomba dhamana kuweka mahakamani nusu ya fedha za thamani ya kosa alilolitenda.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanatuhumiwa kusafirisha wanyamapori hai wenye thamani ya sh 170, 572,500 ambazo nusu ya fedha hizo ni sh 85, 286, 250 ambazo zikigawanywa kwa washitakiwa sita wakati huo zinakuwa sh 14, 214,375.
Inadaiwa kuwa Kamran alitoa kiasi hicho cha fedha ili kupata dhamana na hivyo dhamana ya awali ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kukosa nguvu ya kisheria.
Kwa mujibu wa Jaji Mzuna, mbali na kulipa fedha taslimu kortini lakini sharti la pili liliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro watakaosaini hati ya dhamana ya sh 14, 214, 375.
Katika sharti la tatu, Jaji Mzuna aliwaamuru mshitakiwa wa kwanza, Kamran Ahmed ambaye ni raia wa Pakistan, kukabidhi hati zao za kusafiria Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi.
Sharti la nne linawazuia washitakiwa kuingilia mashahidi na upelelezi wa kesi huku sharti la tano likiwa ni kutosafiri nje ya Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro bila kibali cha maandishi kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu Moshi na pia kutojishughulisha na biashara ya wanyamapori katika kipindi chote cha kesi.
Sharti hilo la sita la kuwazuia washitakiwa mmoja mmoja au kwa ujumla wao kujihusisha na biashara ya wanyamapori, linakwenda sambamba na kuwazuia washitakiwa wote kutotembelea Hifadhi yeyote ya Taifa nchini.
Kwa mujibu wa Jaji Mzuna, sharti la mwisho ni la washitakiwa kuhakikisha wanahudhuria mahakamani siku, tarehe na muda ambao utapangwa na Mahakama.
Wiki mbili zilizopita Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro aliimbia Raia Mwema kuwa wamepokea hati ya mahakama ya kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo lakini bado walikuwa hawajapata taarifa sahihi za mahali alipo.
“Ni kweli tumepokea hati ya kumkamata kutoka mahakamani na tumeshaanza kazi ya kumtafuta ila hadi sasa bado hatujapata taarifa sahihi kuhusu mahali alipo mtuhumiwa,” alikaririwa akisema Kamanda wa PoLisi Mkoa wa Kilimanjaro Robert Boaz.
Tukio la kusafirishwa kwa wanyama hao ilifichuliwa kwa mara kwanza na gazeti la Raia Mwema hadi likapongezwa ndani ya Bunge na ni moja ya kashfa kubwa kuwahi kuikumba sekta ya wanyamapori na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kufuatia kashfa hiyo maafisa kadhaa katika idara ya wanyamapori waliachishwa kazi akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Obed Mbangwa. chanzo raia mwema
Post a Comment