
MARA nyingi masaibu yanayotufika sisi wananchi wa kawaida huwa ni ya kujitakia. Mara nyingi vitendo vyetu hutufanya tuwe sawa na pweza wenye kujipalilia wenyewe makaa. Hebu chukulia, kwa mfano,namna tunavyowaenzi viongozi wetu, hususan wale wenye kututawala.
Viongozi hao wakipanda kwenye majukwaa sisi wananchi wa kawaida ndio wenye kuwashangilia na hata kuwaimbia nyimbo za kuwasifu utafikiri tunataka kuwafikisha mbinguni. Wakianza kuhutubu huwapigia makofi na vigelele hata kama wanayoyasema ni maneno ya uongo au yasiyoingia akilini.
Viongozi hao huwa hawaoni taabu kusema uongo au kutamka maneno ya kipuuzi. Hawaoni taabu kwa sababu wamekwishazoea kutufikiria sote kuwa ni wajinga, mabahaluli.
Mfano mzuri wa hivi karibuni ni matamshi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alipokuwa akiuhutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale kisiwani Pemba. Matamshi hayo yalisikitisha na yalikuwa ya namna mbili.
Kuna yale yaliyokuwa ya uzushi mtupu na mengine yaliyoubiruwa ukweli. Miongoni mwa ya uzushi yalikuwa yale yaliyofanana na uongo anaoambiwa mtoto mdogo. Mheshimiwa huyu kwa sauti ya kiburi na yenye kumtweza Maalim Seif Sharif Hamadi alimsingizia uongo huyo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Kinana alidai kwamba eti Maalim Seif aliulizwa hivi na Rais Kikwete: “Mbona huko unakokaa kwenye mikutano ya hadhara Pemba unazungumza mengine?” Na Maalim Seif akajibu: “Nazungumza yale ili kitumbua kisiingie mchanga.”
Mtu yeyote mwenye kuelewa jinsi mambo yalivyo na jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyozungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar atajua tu kwamba aliyoyasema Kinana ni ya uzushi mtupu. Ni propaganda yenye lengo la kumfitinisha Katibu Mkuu wa CUF na wafuasi wake.
Kinana pia alisema kwamba viongozi wa upinzani wenye kudai Muungano wa Serikali tatu wana uchu wa madaraka na wanatoa hoja za vitisho. Maneno hayo ni ya kuupinda ukweli. Hakika ya mambo ni kwamba hadi sasa wenye kutoa hoja za vitisho ni viongozi wa CCM kutoka Bara na Zanzibar.
Swali linalojitokeza hapa ni hili: kwa nini kiongozi wa hadhi kama ya Kinana akawa haoni taabu usiku kuuita mchana na mchana kuuita usiku?
Nadhani sababu moja ya hayo ni kiburi chenye kuwafanya viongozi wa aina hiyo wawadharau wananchi wa kawaida. Hiyo dharau yao ndiyo inayowasababisha wawadanganye wananchi, hasa wale walio wafuasi wao. Na kila pale wafuasi wao wanavyowaenzi ndipo nao wanapozidi kuwadharau kwa sababu wanaamini ya kuwa wafuasi wao hawana lao jambo, wana amini kila waambiwacho na viongozi.
Kuna jingine tulilolisikia katika hotuba ya Kinana hapo Gombani ya Kale: mwanasiasa huyo akimshambulia binafsi Maalim Seif badala ya kuziporomoa hoja zake za kutaka mfumo wa Muungano wa Serikali tatu.
Mashambulizi hayo ya Kinana yanathibitisha jambo moja, kwamba yeye na wenzake wamefilisika kisiasa. Kwa upande mwingine, hadi sasa wapinzani wao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) hawakumsema mtu yeyote binafsi bali walitumia hoja kuziporomoa hoja za watetezi wa mfumo wa Muungano wa serikali mbili.
Halafu Kinana alijaribu pia kumkashifu Maalim Seif kwa kusema kuwa hakuleta maendeleo kwao Pemba akisahau kwamba hata Mwalimu Julius Nyerere naye hakuleta maendeleo kwao Butiama.
Pengine ni stahili yetu kupata viongozi sampuli ya Kinana kwa makosa tuyafanyayo. Kosa letu moja kubwa ni kwamba wakati mwingine huwa hatuwaenzi tu viongozi hao bali hufanya baya zaidi: hufika hadi hata ya kuwanyenyekea. Huo unyenyekevu wetu ndio wenye kutuchongea. Hulka yetu ya unyenyekevu inakuwa kama sumaku inayozivuta dharau za viongozi.
Kosa letu jingine ni hii tabia yetu ya kuwaita “vigogo” viongozi wa ngazi za juu. Nafikiri tunavyowaita hivyo baadhi yao hudhania kwamba labda kweli wao ni vigogo vilivyoumbwa kuhimili vimbunga na kila aina ya zilzala na haviwezi kung’oka.
Wengine hujiona kuwa wana nguvu na uwezo wa kufanya walitakalo ilimradi yao yawaendee.
Katika kipindi hiki ambapo Tanzania inajaribu kujijengea utawala wa kidemokrasia, wananchi wanapaswa wawe macho na wahakikishe kwamba wanasiasa wao wanachukua hatua za kuimarisha utawala wa kisheria. Njia moja ya kufanya hivyo ni kujitahidi kuzifuata kanuni za kidemokrasia katika kupigania haki zao zote zikiwa pamoja na haki za binadamu.
Ni muhimu wananchi wawe macho hivyo hasa sasa ambapo matamshi ya baadhi ya viongozi wa CCM yanaonyesha kwamba wao si watu wenye kuziheshimu kwa dhati haki za binadamu wala si watu wenye nia ya kuhakikisha kwamba kanuni za kidemokrsia zinafuatwa. Kiburi chao kinawafanya wazipuuze na wasizilinde hata zile haki za kimsingi zilizo katika Katiba ya Tanzania, kama vile haki inayompa kila mtu uhuru wa kusema na wa kueleza mawazo yake.
Siku hizi viongozi wa CCM wamepigwa na homa kali iitwayo “Homa ya Warioba”. Matokeo yake ni kwamba hawajijui hawajitambui. Wameshughulika, wamo mbioni kuhakikisha kwamba wanaikwamisha Rasimu ya Pili ya Mapendekezo ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Rasimu hiyo ya Katiba imewatia kiwewe viongozi hao kwa sababu wanahisi kwamba itayachimba maslahi ya chama chao na yao binafsi. Ndiyo maana wanatumia nguvu zao zote kulivunja pendekezo la kuwa na muundo wa Muungano wa aina ya shirikisho. Tena wanafanya hivyo wakiwa na kiburi na majivuno yasiyosemeka.
Uongozi wa kiburi ni sumu kwa taifa lolote lile. Juujuu unaweza kufikiri kwamba hicho kiburi ni nguvu lakini kwa undani utaona kwamba kiburi hakionyeshi nguvu bali kinajaribu kuuficha udhaifu wa kiongozi. Viongozi wenye kiburi huwa hawawezi kuwavumilia mahasimu wao na wala hawawezi kuwaheshimu. Ndiyo maana wanawafanyia vitisho na wanawatukana matusi mabaya mabaya.
Kosa moja kubwa walifanyalo viongozi wenye kiburi ni kujifikiria kuwa kimsingi wao ni tofauti na watu wengine wakiwa pamoja na wafuasi wao. Hii ndiyo moja ya sababu zinazowafanya wawe wanapenda siasa za majungu.
Wanapendelea kupika majungu waweze kuwaponda wengine na kuwatenga ili wao waendelee kupanda ngazi za uongozi. Na katika upikaji wao wa majungu wanakuwa hawawezi kujiepusha na kusema uongo. Wanakuwa waongo, makidhabu wasio na haya.
Viongozi waliobobea siasa za kiburi wana tabia ya kuwadharau wananchi wa kawaida na wawe wafuasi wao au wa wenzao. Viongozi wa aina hiyo huamini kwamba wana nguvu za kutosha za kuwawezesha wapate wanachokitaka ikiwa ni ushindi katika uchaguzi au kama watakavyo sasa viongozi wa CCM, uendelezwaji wa Muungano wa Serikali mbili.
Sifa moja kubwa na ovu waliyo nayo viongozi wenye kiburi ni ile ya kuwa tayari kutumia kila hila na njia, za halali na haramu, kujipatia mradi wao. Wanakuwa wanaamini kikweli kweli kwamba hakuna chochote kinachoweza kuwazuia hata ikiwa kwa kupata wayatakayo watu wengi watasononeka au watakufa. Yasikilize matamko yao na viangalie vitendo vyao na utafahamu jinsi wenye siasa za kiburi wanavyoziendesha siasa zao.
Kiongozi aliyejaa kiburi huwa si kiongozi mwenye ujasiri au ushujaa. Kiongozi mwenye ushujaa ni yule ambaye wakati wote anaonekana kuwa anazitafutia ufumbuzi shida zinazowakabili wananchi wote bila ya kubagua.
Kiongozi shujaa huwa hachukui hatua yoyote ambayo anajuwa kwamba itawasababisha watu waingie taabuni au wafe. Kiongozi aina hiyo huwa mpole, mwenye dhamiri ya kutenda mema, mwenye kuaminiwa, mwenye kutegemewa na mwenye kusema ukweli.
Hizo ni baadhi tu ya sifa anazokuwa nazo kiongozi aliye jasiri na anayepigania maslahi ya umma. Hizo ni sifa zilizo mbingu na ardhi ukizilinganisha na zile alizo nazo kiongozi mwenye kiburi na mwenye kujiona kwamba yeye na wenzake tu ndio wenye haki katika nchi. chanzo raia mwema
Post a Comment