Usichoke Warioba

TAHARIRI



ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, pamoja na wenzake 20 waliokuwa sehemu ya tume hiyo, hivi karibuni walikutana kwa faragha kutathmini mwenendo wa mchakato wa kuandika Katiba mpya, mchakato unaondeshwa ama kuratibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Warioba na wenzake hao, ingawa tume yao ilikwishakuvunjwa rasmi na Ikulu kwa kuzingatia matakwa ya sheria, lakini wameonyesha juhudi binafsi za uzalendo kwa kutumia muda wao kukutana na kisha kualika baadhi ya watu kwa ajili ya tafakuri, ili hatimaye kunusuru mchakato wa kupata Katiba mpya ambao umeanza kwenda kombo ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Kimsingi, uamuzi wa raia yeyote muungwana kutaka kufanya juhudi za kunusuru mchakato wa Katiba mpya kwa upande wetu tunaamini ni uamuzi sahihi zaidi ya uamuzi wa kutaka kushabikia kuvuruga mchakato huo, kama ambavyo tumekwishasikia kauli za baadhi ya wanasiasa, kutoka ndani ama nje ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ni kutokana na kuzingatia hilo, tunawahimiza Warioba na wenzake katika tume yake na Watanzania wengine wote kusaka muafaka ili hatimaye Bunge Maalumu la Katiba lirejee katika ukamilifu wake na kutenda kazi yake, si tu kwa mujibu wa sheria inayoongoza mchakato wa kupata Katiba mpya, bali vile vile kwa mujibu wa matarajio ya Watanzania kupata Katiba mpya ili kuhuisha mifumo ya kiutawala nchini isiyotoa tija ya kutosha.

Hata kama Katiba mpya haitaweza kubeba matakwa yote, kwa mfano, ya upande wa upinzani au masuala ya upande wa chama tawala bungeni, lakini angalau kuna uhakika kwamba mifumo ya utawala kwa sehemu kubwa itahuhishwa kulingana na matakwa ya Katiba hiyo mpya.

Kwa mfano, suala kupunguza madaraka ya Rais katika uteuzi nyeti ni suala lenye umuhimu mkubwa kwamba wateule hao sasa wafanyiwe usahili na chombo kingine huru na si tu kutegemea uteuzi wa Rais pekee.

Si hilo tu, masuala mengine muhimu kama ya maadili ya viongozi wa umma, masuala ya kuwajibishana kati ya wenye madaraka na wananchi, masuala ya uhifadhi wa haki za binadamu, masuala ya umiliki wa mali na mengine mengi ya aina hiyo, yote hayo ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unafikia ukingoni salama na kwa maridhiano.

Kuvuruguka kwa mchakato wa Katiba mpya maana yake ni kupoteza fursa nyingine muhimu ambazo zingeweza kuleta manufaa kwa nchi hadi pale mchakato wa aina hiyo utakapoweza kuitishwa tena baadaye kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo, ingawa kwa watu makini zaidi, mchakato huu ulipaswa kufanyika kwa ufundi zaidi ili Katiba itakayopatikana idumu kwa miaka kadhaa.

Kwa hiyo, tunasema Warioba na wenzako, msichoke, kwa pamoja tusonge mbele tukipuuza kejeli na maneno mengine ya hovyo kutoka kwa wenye shibe inayotokana udhaifu wa kiutawala ambao kwa namna fulani unahifadhiwa katika Katiba ya sasa 
chanzo raia mwema

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top