Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wakiwa katika kikao
kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White House mjini Dodoma juzi na
kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Picha na Ikulu
Dodoma. Baadhi ya makada wa wa CCM wanaotajwa kuwania urais
kupitia chama hicho wanadaiwa kugeuza mkutano wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (Nec), kuwa sehemu ya kampeni kwa wajumbe wa mkutano huo wakidaiwa
kumwaga fedha usiku kucha.
Gazeti hili lilishuhudia kampeni hizo zikifanywa
na wapambe wa wagombea hao nje ya Ukumbi wa Nec uliopo nje ya jengo la
White House mjini Dodoma na baadhi ya watu wanaotajwa kuwania nafasi
hiyo.
Wapambe hao kwa siku mbili za vikao vya Nec
vilivyofanyika mjini hapa kuanzia juzi walionekana wakifika mapema,
kusalimia, kujitenga katika makundi madogomadogo na wajumbe wa Nec
tofauti na vikao vingine vilivyotangulia.
Harakati hizo hazikuishia katika viwanja hivyo,
bali hata nje ambapo mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo
kutoka Kanda ya Ziwa ameonekana kukutana na makatibu wa CCM katika moja
ya hoteli mjini hapa.
“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara
nyingi katika kile kinachoelezwa kuwa ni kusaka wajumbe ili wasijiunge
na kambi nyingine,” kilieleza chanzo chetu.
Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye, alisema bado hajazipata taarifa hizo na kwamba kama kuna
vitendo vya rushwa vinafanyika ni nje ya mazingira hayo.
Alisema katika mazingira kunapofanyika kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo hivyo.
“Sasa kama wanapeana barabarani mimi itakuwa ni
vigumu sana. Mimi ninashughulikia na mambo ya humu ndani (kikao cha
Nec),”alisema na kuongeza:
“Leteni taarifa nilikuta fulani anagawa ama fulani
anapokea, haya maneno ya jumla hivi yanaweza kuwa ni mkakati wa kupaka
chama matope,” alisema.
Alisema kama inagawiwa usiku wakati yeye akiwa amelala hawezi kufahamu.
Makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya wanaingia katika Nec kwa mujibu wa vyeo vyao.
Tayari hali hiyo imelalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa Nec, wakisema inakitia aibu chama. mwananchi
Post a Comment