Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuacha kigugumizi katika kufanya maamuzi ya hatma sakata la Escrow.
Akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Sikonge, mkoani Tabora jana, Prof. Lipumba alisema kigugumizi cha Rais Kikwete kinatokana na shinikizo analopata kutoka Chama cha Mapinduzi(CCM) na ushiriki wa baadhi ya watendaji wake katika sakata hilo.
Alisema kuhusishwa kwa mawaziri katika sakata la Escrow kunazidi kuichafua nchi kimataifa hivyo kuchelewa kutoa maamuzi kunazidi kuwapa hofu jumuiya mbalimbali za kimataifa.
Alisema Rais Kikwete alikuwa na kila sababu ya kuchukua hatua za haraka kwa kuzingatia maazimio ya bunge ili kuepusha msuguano baina ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa.
“Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, Katibu wa Rais aliandika barua kuafiki fedha za Escrow zitolewe kama Mwanasheria Mkuu alivyopendekeza, kwa maana ya kawaida ni kuwa kama Katibu wa Rais alikuwa akifahamu suala hilo kimaandishi hivyo hata Rais analifahamu ndio maana anapata kigugumizi,” alisema Lipumba.
Lipumba alishangazwa na kitendo kilichoripotiwa na gazeti moja nchini kuwa Waziri wa Nishati na Madini kupewa ziara ya kiserikali nchini Norway, hali ya kuwa ni miongoni mwa waliotajwa kuhusika katika ufujaji wa fedha za serikali kupitia Escrow ambayo kwa mujibu wa maazimio ya bunge waliohusika walitakiwa kusimamishwa kazi kwa mujibu wa taratibu za kiserikali.
Alisema anayehusika kuidhinisha ziara ya kiserikali kwa viongozi wa nchi ni Rais lakini pamoja kuchelea kufanya maamuzi amemruhusu Waziri Muhongo kwenda kikazi nchini Norway.
Prof. Lipumba aliitaadharisha serikali kuwa endapo haitachukua maamuzi magumu dhidi ya maamuzi yaliyotolewa na bunge, wataitisha maandamano yatakayowahusisha wananchi kushinikiza serikali kuchukua hatua dhidi ya waliohusika.
Pia aliwataka wananchi wa Tabora kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kuiondoa CCM.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu CUF bara, Magdalena Sakaya akihutubia mkutano huo aliwataka akina mama kuacha utamaduni wa kukubali bila kupima kwani wanaoathirika kwa asilimia kubwa na maamuzi ni wao.
CUF ni miongoni mwa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Vingine ni Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Post a Comment