-
- Asema wanaosema wasilipwe ni mawakili wa shetani
- Barua yavuja kuhusu namna alivyoshinikiza
- AMWITA KAFULILA NGEDELE
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema,
alishinikiza kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL) ilipwe fedha zilizokuwepo
katika akaunti ya Escrow kiasi cha kufananisha wanaopinga hilo na ‘mawakili wa
shetani,’ imefahamika.
Habari hizi zimeibuka katika kipindi ambacho Bunge la
Tanzania linaanza rasmi kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) kuhusu namna fedha hizo, kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni
200, zilivyochotwa kutoka katika akaunti hiyo.
Raia Mwema sasa linafahamu kwamba kwa kutumia wadhifa wake,
Werema alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile,
Oktoba mwaka jana, akimtaka akubali IPTL, ambayo tayari ilikuwa inamilikiwa na
kampuni ya Pan African Power (PAP), ilipwe fedha za Escrow haraka.
Katika barua yake hiyo yenye Kumb. Na AGCC/E.80/6/65 ya
Oktoba 2 mwaka huu ambayo Raia Mwema limefanikiwa kuona nakala yake, Werema
alimwambia Likwelile kwamba hakutakuwa na tatizo lolote kama IPTL watapewa
fedha za Escrow.
“Uamuzi wowote wa kutoa fedha kutoka katika akaunti ya
Escrow hauna tatizo, unalindwa kisheria na umezibwa na uamuzi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania kupitia hukumu ya Jaji John Utamwa.
“Uamuzi huu wa Mahakama Kuu umetupa sasa fursa ya
kuhakikisha suala hili la IPTL linamalizika. Hii ni bahati ya mtende kwetu
kumaliza suala hili. Tunatakiwa kuchukua hatua sasa badala ya kuwa mawakili wa
shetani,” aliandika Werema.
Werema aliingia katika matatizo ndani ya Bunge kutokana na
majibizano yake na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kiasi cha kufikia
hatua ya kumuita mbunge huyo tumbili na yeye mwenyewe kuitwa mwizi.
Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliachim Maswi ndiyo viongozi wanaotajwa kusaidia kufanikisha kutolewa kwa
fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo.
Ni Werema na Maswi ndiyo waliokuwa vinara wa mashambulizi
dhidi ya wabunge waliokuwa mstari wa mbele kutaka suala hilo lichunguzwe, na
Katibu Mkuu huyo aliwahi kuita ushahidi wa wabunge kuwa unatokana na karatasi
za kupikia maandazi.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutokana na uchunguzi
uliofanywa na CAG, fedha zilizokuwamo katika akaunti ya Escrow zilipaswa
kulipwa kwa Tanesco kama malipo ya kutozwa kiwango kikubwa cha huduma za
kutumia mitambo ya IPTL kuzalisha umeme.raiamwema
Post a Comment