
MEI 14, 2008, niliandika katika gazeti hili kuonya namna nchi ilivyokuwa ikielekea kutekwa na genge la Mafia kwa kushirikiana na mafisadi wa nchini, na kwa Serikali kufumbia macho ishara na viashiria vyote vya utekwaji huo.
Baadhi ya viashiria na matukio yaliyonifanya niandike na kuonya, yalikuwa ni pamoja na Serikali kuwaonea haya mafisadi wa sakata la EPA wanaofahamika,walipora mabilioni ya fedha za wavuja jasho wa nchi hii, lakini “ikawahurumia” na kuwakingia kifua kwa kuwataka warejeshe tu kwa ahadi ya kutochukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huohuo, serikali ilikuwa ikijitahidi kufunika maovu ya mafisadi wa sakata la mkataba wa kilaghai wa IPTL waliotajwa tangu serikali ya awamu ya tatu, wakati uchumi wa nchi ukiendelea kuangamia kutokana na gharama kubwa za umeme usiotabirika huku TANESCO, likielekea kufilisika kwa kukamuliwa zaidi ya 4.6bn/= kwa mwezi na IPTL kwa kuuziwa umeme usiokuwepo na kwa kutumia mtambo wake, yaani “Capacity Charge”.
Nilikuwa nimekerwa pia na kashfa za mabilioni ya fedha za umma za Meremeta, Deep Green, Tangold, Kagoda na rada; na kwa kiburi cha viongozi kufikia kuwaita wananchi waliohoji hayo kuwa “wavivu wa kufikiri”, na kwamba kama wananchi waliona huko ni kufilisi nchi, basi, wale majani.
Hicho ni kiburi cha kihayawani na kulewa madaraka ikizingatiwa kwamba, Baraza la Mawaziri kwa ujumla wake linawajibika kwa Bunge, ambapo waziri mmoja mmoja anawajibika kwa Bunge kuhusiana na utendaji wa wizara yake. Kwa mantiki hii, mawaziri ni wadogo kwa Bunge na kwa mbunge kutokuwa na ubavu wa kukemea, vinginevyo ni kudharau wananchi wanaowawakilisha bungeni.
Ni uhayawani kwa sababu, haiingii akilini kwa waziri kumkemea mbunge badala ya kinyume chake. Kufanya hivyo maana yake ni kwa serikali kutaka kuwafanya wananchi kuwa wananchi wa serikali, badala ya Serikali kuwa “Serikali ya wananchi kwa ajili ya wananchi”, ambayo ndiyo tafsiri sahihi ya neno “demokrasia”.
Nilikwazika na naendelea kukwazika, kuona wafanyabiashara wakubwa wakivamia uwanja wa siasa huku wakilinda biashara zao, na kugeuza siasa na vyama kuwa kichaka cha kuficha dhamira zao mbovu kwa Taifa kwa kuwa karibu na serikali ili wapore bila hofu ya kuulizwa.
Tabia hii mbovu imeleta utamaduni wa kifisadi ambapo siasa sasa inapora rasilimali za nchi na utajiri [kwa kinga], na utajiri sasa unanunua siasa. Ni kwa sababu hii hivi leo, wanasiasa ni watu matajiri na wenye nguvu kuliko watendaji wenye elimu nchini. Kama hivi ndivyo, kwa nini wanataaluma wasitelekeze fani zao kutafuta malisho mapya kwenye siasa na kuacha Taifa likigwaya kwa kukosa Wataalamu?.
Hali hii imekikumba zaidi chama tawala – CCM, ambapo ufisadi unafanywa na kulindwa kwa kufichiana maovu kwa hofu ya kudhalilisha Chama. Kwa waliokosa uzalendo kiasi hiki, hili haliwakeri; na inapokuwa hivyo, kwao ni “heri Taifa liangamie lakini chama kisalimike”. Huu ni uhaini ulio dhahiri.
Hata hivyo, CCM kilibaini, japo kwa kuchelewa, hatari kwa nchi, ya kuchanganya uongozi na biashara; kikatoa ilani kwa wanasiasa kuchagua kati ya siasa na biashara; lakini mafisadi ndani ya chama na genge la Mafia yalipoinua uso kuwatazama waliotaka iwe hivyo, wote wakanywea na mambo yakaendelea kama kawaida. Kama huku si chama tawala na serikali yake kutekwa nyara na Mafia, ni kitu gani?
Tena, CCM kilitaka viongozi wote wanaotuhumiwa kwa kashfa mbali mbali wajipime na kuachia ngazi chini ya mkakati wa “Chama kujivua gamba”. Hawa ni pamoja na wale waliotajwa katika kashfa za IPTL, EPA, Mfuko wa “Import Support”, rada na ununuzi wa ndege mbovu ya Rais na ubinafsishaji usiojali.
Wananchi wakaingiwa matumaini kwa nchi kuanza kujisafisha ili kuleta neema kwao. Lakini wapi; baadhi ya viongozi hao mafisadi, wenye kupewa nguvu na boya za “kuogelea” na genge la Mafia la Kimataifa, waliweza kujitokeza kifua mbele kukiambia chama tawala, serikali na wananchi bila woga wala aibu, kwamba, “gamba limekwamia kiunoni, limeshindwa kutoka”; na kwamba “mwenye kutaka litoke achukue shoka aling’oe”.
Chama na serikali yake vikanywea; mambo yakaendelea kama kawaida, lakini safari hii kwa kasi ya kutisha katika hali iliyoashiria chama na serikali kusalimu amri kwa ufisadi na mafisadi, huku nchi ikiendelea kukamuliwa zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa mwezi kwa njia ya kifisadi na uwekezaji usiojali.
Wakati huohuo, mawakala wa ufisadi nchini wakidanganya umma kwa kusema, “ndege ya uchumi inapaa”, kwa maana ya kukua kwa kasi kwa uchumi, wakati ni kinyume chake, huku wananchi wakizidi kufukarika kwa kufukarishwa na mfumo.
Haya yakiendelea, tulidumazwa fikra kwa kupandikiziwa miradi na programu mbali mbali za ulaji kwa jina la “Maendeleo”, ikiwamo programu“Matokeo Makubwa Sasa” [BRN], iliyoletwa kwa kishindo na kwa gharama kubwa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuinua tija, lakini sasa ni kimya; tija, uadilifu na maadili yanazidi kuyoyoma huku“EPA” na “IPTL” mpya zikizidi kuzaliwa kila siku.
Nayo programu ya “Kilimo Kwanza” tuliyoambiwa italeta mapinduzi ya kijani nchini imekuwa “Kilimo Mwisho” kwa kufanywa bango la kuvutia waporaji wa ardhi kutoka nje na ndani kwa kisingizio cha uwekezaji, kwa kilio na kusaga meno kwa wakulima na wafugaji na hivyo kutishia kuzuka kwa vita ya “Mau Mau” kugombea ardhi.
Ipo siku wanyonge watasema “imetosha”, na kwa wawekezaji hao kunyweshwa “shubiri” kwa ghadhabu ya wanyonge hao.
Nilishindwa kujizuia kuandika tena, Novemba 12, 2012; pale kufuru ya ufisadi ilipotia fora kwa Twiga hai kuibwa na kutoroshewa nje kwa ndege wakati mihimili yote ya dola ipo ikijipongeza kwa BRN. Kama ilivyo kwa ufisadi mkubwa wowote nchini, serikali inadai kutojua wala kuona wizi huo ulivyotokea.
Kwa mujibu wa kamusi iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili [TUKI], Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam [Kiingereza – Kiswahili], neno “Mafia” limetafsiriwa kumaanisha chama cha siri kinachojishughulisha na ujangili na ujambazi [wa kiuchumi na kisiasa] kwa lengo la kutesa serikali madarakani. Kwa kifupi, “Mafia”, ni genge la wahalifu dhidi ya serikali na watu wake.
Genge la Mafia huendesha na kuongoza katika nchi. Ni serikali isiyo rasmi [parallel government] lakini yenye nguvu kuliko serikali iliyo madarakani. Huendesha biashara kubwa kwa magendo, ikiwemo biashara haramu ya utakatishaji fedha [money laundering] na biashara ya dawa za kulevya.
Tumejionea jinsi taifa letu lilivyoingizwa mkenge katika sakata la Meremeta, Richmond na IPTL ambapo biashara haramu ya fedha ilikuwa dhahiri; wakati biashara ya dawa za kulevya ikiendelea sambamba nchini bila kuguswa. Kama huku si serikali kutekwa nyara na genge la Mafia, ni nini?.
Genge hili lina vikosi vya mauaji kuweza kumtoa uhai yeyote anayeonekana kikwazo kwa malengo yake; halichagui wala kuogopa cheo cha mtu: kuanzia Rais wa nchi, Waziri Mkuu hadi wakili wa kujitegemea, mradi tu atajaribu kuingilia mkondo wa maslahi yake. Mauaji yanayoweza kufanywa na genge hili dhidi ya walengwa ni kwa njia ya kudhuru mwili au kudhuru kisiasa.
Tunashuhudia kuzuka kwa matukio hivi karibuni, kwa viongozi na watendaji wenye misimamo thabiti katika kutetea maslahi ya wanyonge na maslahi ya taifa, kulishwa sumu, kutekwa na kuteswa staili ya “Gestapo”, na kung’olewa kucha na meno katika mazingira ya kutatanisha.
Huu ni utamaduni mpya ambao serikali madarakani haijatueleza umetoka wapi; wakati vyombo vya dola vimekunja mikono tu na kusaidia kushangaa kuendelea kwake, kuthibitisha kwamba inajua lakini haina nguvu wala ujasiri kuukomesha.
Genge la Mafia linapenyeza watu wake katika taasisi zote nyeti za utawala wa nchi, ikiwa ni pamoja na utumishi wa umma ili kuhakikisha kwamba serikali inatumikia uharamia na ufisadi zaidi kuliko kutumikia wananchi; sera na mipango ya “maendeleo” kulenga kunufaisha maharamia wa kimataifa na mawakala wao badala ya kunufaisha wananchi.
Genge la Mafia lina mawakala ndani ya Bunge na katika Baraza la Mawaziri. Bunge lenye kutekwa na “Mafia” na mafisadi utalitambua kwa sifa mbaya zifuatazo: Kwanza, wengi wa wabunge wake wanaingia bungeni kwa ushindi wa mizengwe, na wapo humo kutafuta maslahi binafsi badala ya kuwasemea wananchi. Hili si Bunge la uwakilishi wa wananchi, bali ni Bunge maslahi.
Tumejionea hivi karibuni, jinsi wabunge na baadhi ya mawaziri walivyosimama kidete bungeni, kutetea ufisadi na utakatishaji fedha wa Kampuni ya IPTL kwa kukana taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG] na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali [PAC] waliyoiteua wao wenyewe, ilimradi kutaka kuwaokoa mafisadi waliowalainisha kwa fedha haramu. Kwa wabunge hawa, kwao wanaona ni “heri taifa liangamie lakini fisadi apone”.
Tunawafahamu kwa majina na kila mmoja alichosema bungeni kwa kulisaliti taifa na wananchi. Hatuna nia tena kuwaona wakirejea bungeni; na watokomezwe kwa unafiki, umamluki na usaliti wao.
Uzoefu umeonesha kuwa, uteuzi wa mawaziri na watendaji wakuu wa taasisi za umma kutoka miongoni mwa watu wanaoishi ughaibuni bila kutumwa na taifa ni hatari, kwani siku zote umetupatia mawaziri na watendaji mawakala wa utapeli na ufisadi wa kimataifa, wenye mzio [allergy] na jasho la mdundakazi wa nchi hii.
Ni haohao wanaotudumaza na mipango hasi ya “maendeleo” isiyoshabihiana na mahitaji na mazingira yetu ambapo programu na miradi ya ulaji inayoshinikizwa kupitia wao na ufisadi wa kimataifa, inasambaratika baada ya wakubwa hao kuponda mali za miradi tunayopumbaziwa.
Ziko wapi SAPs? Tumeambua nini kwa ubinafsishaji wa viwanda vyetu kama si kujenga utegemezi kwa kila kitu hata “toothpick” na viberiti kutoka nje?.
Pili, Bunge lenye kutekwa na “Mafia” ni Bunge la kitabaka lisilowakilisha matakwa ya wananchi walio wengi, ambao ni wakulima na wafanyakazi; badala yake ni Bunge lenye kulemazwa na fikra za wafanyabiashara, wasomi na wanataaluma wasaliti wa umma, walioziasi fani zao na kukimbilia “pepo ya Mafisadi” kwa uchu wa utajiri.
Na kwa msaada wa mafisadi, baadhi yao hupewa Ukurugenzi wa Makampuni ya kifisadi kuwanyamazisha kitaaluma ili watetee maslahi ya makampuni hayo badala ya kuwatetea wananchi. Kama huo si usaliti kwa umma, ni nini?.
Mijadala ndani ya Bunge kama hilo hutawaliwa na mizaha, uchama kama kikundi ndani ya kikundi, kutetea maslahi binafsi, biashara zao na “wenzao”, na kwa mawakala wa genge la Mafia kujifunza siri na mbinu za serikali za kujenga nchi, wajue wapi na namna ya kupora salama.
Genge la Mafia lina mawakala pia katika Taasisi za Kidini, Viongozi wa Makanisa na Misikiti ili kupooza, kama si kuua dhamira ya kutetea wanyonge wenye kiu ya haki na usawa mbele za Mungu. Hatukushangaa kufahamu kwamba “makombo” ya fedha za IPTL yamewadondokea pia baadhi ya viongozi wa Kanisa Katoliki kwa madhumuni haya.
Haya tumejionea pia kwenye sakata la “Akaunti ya Escrow” Bungeni hivi karibuni, na wakati wa Kikao cha Bunge Maalum la Katiba, ambapo Wabunge mawakala wa ufisadi, walifurahia kuondolewa kwa ibara inayohusu “Tunu za Taifa”, Maadili na Miiko ya Viongozi, zilizopendekezwa kwenye Rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba ili Taifa likose dira.
Viongozi washiriki kupora rasilimali bila hofu ya kuwajibishwa; na wananchi wawaone wabunge wao miungu-watu, wasio na mamlaka nao baada ya kuwachagua.
Na baadhi ya waliojipa jukumu la kuandika Rasimu mpya baada ya kunyofoa vipengele hivyo kwenye Rasimu, tumewaona wamenaswa tena, si kwenye kashfa ya IPTL tu ya sasa, bali wametajwa karibu kwenye kashfa zote kubwa kubwa hapa nchini tangu kuingia kwa sera za uchumi huria zaidi ya miaka 20 iliyopita; na ni hao hao waliotuambia “gamba limegomea kiunoni; mwenye kutaka litoke aje na shoka alitoe”.
Ujasiri huu wa kifisadi na kejeli kama hii, unatokana na mawakala hao wa ufisadi nchini, kupewa nguvu ya kifedha na kisiasa na genge la Mafia linalotaka kuangamiza nchi.
Tujiulize: hivi ni kweli serikali madarakani imekosa “shoka” kuweza kung’oa, sio gamba pekee la mawakala hao wa maovu, bali pia na viuno vyao gamba lilipokwamia?.
Kiburi na kejeli kama hizi dhidi ya mamlaka ya nchi na wananchi, kinaweza kufanyika kwa nchi yetu pekee, kamwe si kwa nchi yoyote duniani yenye dola kamili. Hii inaonesha jinsi utamaduni wa maovu ulivyozamia hadi kilindi cha nchi hii. Na kwa sababu hii, kwa nini tusiamini bila ya shaka yoyote, kwamba nchi yetu, katika ujumla wake, imetekwa na genge la Mafia?. Na nini hatima yetu kwa yote haya?.
Ukiona Bunge na Serikali vinapuuza maoni na kilio cha wananchi, na kusikiliza zaidi ya wenye pesa; fahamu kwamba Bunge na Serikali hiyo wanatumikishwa na kutumikia wenye fedha katika hali ya ulevi wa madaraka, kwa kuwa madaraka yote hulevya; lakini madaraka makubwa zaidi hulevya zaidi. Kwa jinsi hii, Serikali ya aina hiyo hujitenga au hutengwa na watu kwa kujitakia, kwa chuki na ghadhabu ya kulimbikiza.
Inapofikia hapo, ni vyema kwa viongozi kuamka kutoka ulevini, kusikia kauli ya aliyekuwa Rais wa Marekani, John Fitzergerald Kennedy kwamba, “Kwa kuungwa na umma kwa dhati, naweza kufanya jambo lolote salama; lakini kwa kuungwa mkono na wenye dhamira isiyoshabihiana na matakwa ya umma, lazima nitaona giza mbele”. Je, kwa mazingira yetu leo, viongozi wetu hawaoni dalili za giza mbele; au wanajiandaa kuhamia ughaibuni na familia zao?. raiamwema
Post a Comment