
KURUGENZI ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema Rais Jakaya Kikwete hajadhalilisha Bunge ama wabunge.
Pia, imesema uteuzi uliofanywa na Rais wa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Profesa Mighanda Manyahi haukulenga kumdhalilisha yeyote na kwamba umetokana na mamlaka aliyonayo kisheria.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana, Kurugenzi hiyo ilisema madai ya wabunge wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe wa Chadema na David Kafulila wa NCCR-Mageuzi, siyo ya kweli.
Ikulu iliwataka wabunge hao, kuviachia vyombo vingine, vilivyopewa mamlaka na madaraka kutekeleza maazimio ya Bunge na ushauri mwingine kwa Rais.
Taarifa ya Ikulu Gazeti la TANZANIA DAIMA linalomilikiwa na chama cha upinzani cha CHADEMA la Jumapili, Januari 4, 2015, liliandika habari kwenye ukusara wake wa mbele chini ya kichwa cha habari: ”Wabunge: Ikulu imetudhalilisha”, hata kama wabunge wanaokaririwa katika habari hiyo ni wawili tu, Freeman Mbowe na David Kafulila.
Habari hiyo inadai kuwa Ikulu na Rais Kikwete kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kwa “kumruhusu” Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuteua Wajumbe wapya wa Bodi hiyo, wamewadhalilisha Wabunge na “kuwafanya waonekane wajinga kwa sababu maamizio yao yametupwa.”
Ufafanuzi wenyewe Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu madai hayo ya Mbowe na Kafulila: [1] Kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kamwe hajapata kulidhalilisha Bunge ama Wabunge.
Anafurahishwa na kazi yao nzuri na ushirikiano wao kwa Serikali yake. Rais Kikwete alirejea kusisitiza jambo hili majuzi tu na kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri katika Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi, Alhamisi iliyopita usiku.”
Kwamba uteuzi wa Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Profesa Mighanda Manyahi, uliofanywa na Mheshimiwa Rais wiki iliyopita, unatokana na mamlaka aliyonayo kisheria na wala haukulenga kumdhalilisha yeyote, kama ambavyo teuzi nyingine nyingi azifanyazo, hazilengi kumfanya mtu yeyote “mjinga”. [1]
Kwamba vile vile hadhi ya sasa ya Mheshimiwa Muhongo, kama Waziri wa Nishati na Madini, bado inampa madaraka ya uteuzi kwa bodi zilizoko chini ya Wizara yake na wala hajapoteza “sifa ya kuendelea kuwa ofisini na hivyo kukosa sifa ya kuteua Wajumbe wa Wakurugenzi wa TANESCO” kama wanavyodai wabunge hao wawili.
Kwamba uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na Wajumbe wa bodi hiyo ni ushahidi mwingine usiopingika wa utekelezaji thabiti wa Maazimio ya Bunge, lililojadili suala zima la Akaunti ya Escrow ya Tegeta na ushauri wa Bunge hilo kwa Mheshimiwa Rais.
Kumshutumu Mheshimiwa Rais kwa hatua yake ya kutekeleza ushauri wa Bunge ni jambo la kushangaza sana. [1] Kwamba, tofauti na baadhi ya shutuma za wabunge wa upinzani, Mheshimiwa Rais ametekeleza kikamilifu kabisa ushauri uliotolewa kwake na Bunge katika maazimio yote manane, moja baada ya nyingine, ukiwemo ushauri kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na kuwajibishwa kwa maofisa mbalimbali wa umma na waandamizi wa Serikali.
[1] Kwamba Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kuwashauri Waheshimiwa Mbowe na Kafulila wakubali kufuata misingi ya haki ya kibinadamu katika kushughulika na watu wengine. [1]
Kwamba waheshimiwa hao hawawezi wao kuwa wapigaji mbinja (whistle blowers), wakawa wachunguzi, wakawa na mamlaka ya kukamata watu, wakawa na madaraka ya kushitaki, wakawa na madaraka ya kuhukumu na wakawa na madaraka ya kuwafikisha watu jela na kuendelea kuwalinda huko.
“Tayari wamefanya kazi yao, tena vizuri sana Bungeni, sasa waachie watu wengine na vyombo vingine vilivyopewa mamlaka na madaraka kutekeleza yale yaliyoazimiwa bungeni na kutolewa kama ushauri kwa Mheshimiwa Rais.
Aidha, utekelezaji huo wa masuala ya umma unapokuwa hauendi kwa mujibu wa matakwa yao, pia wawe tayari kukubali kwa sababu katika demokrasia nzuri kama yetu na utawala bora safi kama wa kwetu, hakuna atakayefanikiwa kupata kila kitu anachokitaka na kama anavyokitaka,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu kwa wabunge hao HABARI LEO
Post a Comment