Wanawake wanavyoteswa na waume zao Zanzibar





Baadhi ya wanawake wa Zanzibar wakiwa kwenye mkutano wa kujitambua.Picha na Salma Said.







Wanawake wanachukuliwa kama ni watu wa kubaki katika ndoa kutii amri za mume hata kama amri hizo siyo za haki, heshima au zinavunja utu wa mwanadamu.


Kwa mfano, gwiji la fasahi ya Kiswahili, marehemu Sheikh Shabaan Robert katika kitabu chake “Maisha yangu na baada ya miaka hamsini” katika ukurasa wa kumi anatoa wasia kwa bintiye kwa kumwambia;


“Fanya kila hali, la mume kulikubali, ila lisilo halali, kukataa si hatia” Hapa anampa ujasiri mwanawe wa kike kutokubali mambo ya ovyo kutoka kwa mume, ana mjengea uwezo wa kuwa mwanamke na mama shupavu katika maisha ya ndoa yake na kuweza kukabiliana na familia.


Matukio ya kutendewa isivyo wanawake siyo mageni, wanawake wamekuwa wakipata vipigo, kuteswa na wengine kufikia hata kujeruhiwa hapa Zanzibar.


Wanawake Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi ngumu, wana mzigo wa kuhudumia familia, wanafanya biashara, wanafanya kazi ofisini huku wakisubiriwa kupika, kuchota maji, wanabeba mimba na kujifungua na wakati mwingine hata hayo matunzo ya mama mjamzito hayapati hasa wanawake wa vijijini.


Katika sehemu za mashamba Unguja na Pemba, wanawake wanalima, wanapanda, wanapalilia, wanachuma karafuu huku wengine wakianguka na wasipofikisha vyakula vinavyotakiwa, anapata matusi na hatimaye kuambulia kipigo.


Katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kati ya Novemba hadi Desemba mwaka jana, Zanzibar kuna matukio kadhaa ya wanawake kupata vipigo kutoka kwa waume zao.


Ijapokuwa TAMWA katika utafiti huo wanasema kwamba hulka ya kuwapiga wanawake siyo matukio maarufu sana, ukweli ni kwamba wanawake wengi wa Zanzibar ni wasiri mno, hata akipigwa au kuteswa hawi wazi kutangaza.


Mathalan mmoja ya wanawake aliyehojiwa Mtaa wa Kwamtipura, analalamikia hulka ya mumewe ya kumpiga mara kwa mara hasa pale anapodai huduma muhimu kama chakula na ikiwa akimweleza upungufu basi inakuwa nongwa na sababu ya kuanza kupokea vipigo!


Mwanamke huyu hivi karibuni alipokea kipigo pale aliposema kiwango cha chakula alichoachiwa ni kidogo na hakiwezi kumtosha, ndipo mume wake alianza kumfokea kwa maneno machafu na kuanza kumpiga jambo ambalo lilimfanya mwanamke huyo kukimbilia kwa Sheha Machano Khamis kwenda kujisalimisha.


Wanawake wanaopata vipigo kwa hakika ni wengi, lakini wamekuwa wakitofautiana kutokana na sehemu hadi sehemu. Wapo wanaopigwa kwa madai ya kudai haki za msingi za mke ikiwamo kupatiwa huduma za mahitaji ya chakula, mavazi na hata kufanya kazi. Miongoni mwa sababu za kushamiri kwa vitendo vya kupigwa wanawake na waume zao ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi, kugombania watoto na mali na kuporomoka kwa maadili katika jamii
soma jaidi http://www.mwananchi.co.tz/habari

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top