WATANZANIA 100 WAHUKUMIWA KUNYONGWA





ZAIDI ya Watanzania 100 waliopatikana na hatia ya kuingiza dawa za kulevya nchini China, wamehukumiwa kunyongwa. Habari za kuaminika zilizolifikia gazeti hili zimesema, idadi hiyo ya Watanzania waliofungwa katika magereza mbalimbali nchini humo, wanaendelea kusubiri adhabu hiyo.

Taarifa zaidi zinaeleza, adhabu hiyo haijatekelezwa, kwa kile kilichodaiwa kuwapo kwa mazungumzo, kuona uwezekano wa watuhumiwa hao kupewa adhabu mbadala ya kifungo cha maisha badala ya kifo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Serikali ya China imeacha kutekeleza adhabu hiyo ya kifo, kutokana na kuthamini uhusiano mzuri wa kirafiki uliopo baina ya nchi hiyo na Tanzania.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ali, aliithibitishia MTANZANIA Jumamosi kuhusu Watanzania hao kupewa hukumu hiyo, ingawa alisema hadi sasa hakuna Mtanzania aliyenyongwa au kupigwa risasi kwa makosa hayo.

“Adhabu ya kifo ipo na inatolewa, lakini hakuna Mtanzania aliyenyongwa na hii inatokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China,” alisema Mkumbwa.

Mkumbwa alisema taarifa za China kuacha kutekeleza adhabu ya kifo kwa raia hao wa Tanzania pia alipewa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipofanya ziara ya kikazi nchini humo Oktoba, mwaka jana.

Kasi ya kukamatwa kwa Watanzania wakiwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi, imezidi kuchukua sura mpya, baada ya kubainika kuwa maelfu ya Watanzania wanatumikia vifungo mbalimbali, ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi.

Inaaminika kuwa Watanzania 176 wanatumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini China, huku asilimia 99 wakiwa wamekamatwa kwa dawa za kulevya.

Juhudi za Tanzania kuwasiliana na China kuhusu uwezekano wa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa zinadaiwa kugonga mwamba, kutokana na idadi kubwa ya wafungwa hao kutuhumiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya.

Tayari Tanzania imesaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Thailand, mkataba ambao utawafanya Watanzania waliofungwa nchini humo kuomba kutumikia vifungo vyao nchini.

Mkataba huo ulisainiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Thailand, Sura Pong Tovichakehaikul na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, huku wakishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra na Rais Jakaya Kikwete.

Takwimu za awali zilizotolewa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaeleza kuwa zaidi ya Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, huku wengine 132 wakikamatwa katika nchi nyingine, ikiwamo Pakistan

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top