Wiki iliyopita nilijadili katika safu hii kuhusu haja ya kuwa na Serikali ya Tangangika. Ninawashukuru wote walionitumia ujumbe wa simu kuchangia hoja zao.
Leo nimeona si vyema mjadala ule ukaishia hewani, hivyo nauendeleza ili kuongeza kile nilichokianzisha. Nitajaribu kujibu ujumbe huo kupitia mfululizo wa makala hizi.
Ili kupata picha halisi ya muungano inabidi kwanza tuangalie historia yake.
Pamoja na kuwepo dhana kwamba chanzo cha muungano kati ya nchi hizi mbili ni undugu wa wananchi wake, lakini bado sababu hii haina mashiko.
Kama ni undugu, basi Watanzania wana undugu na nchi zote zilizowazunguka, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Zambia na Msumbiji. Mbona hatuungani nazo?
Sababu kubwa ya muungano kati yetu zilikuwa za kisiasa zaidi na Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyesimamia moja kwa moja.
Ieleweke kwamba, kabla ya miaka ya 1960 tayari Zanzibar ilishakuwa kwenye mizozo mingi ya kisiasa ambapo vyama vya ASP, ZNP, ZPPP na Umma vilikuwa vikivutana hadi vilifikishana kwenye umoja wa nchi za Afrika wakati huo kusuluhishana.
Pamoja na hayo, Zanzibar iliyotawaliwa na Waarabu ilikuwa na mwingiliano mwingi ulioifanya isitulie.
Hivyo, Zanzibar ilikuwa tishio kwa utawala wa Mwalimu Nyerere, ndiyo maana wakati fulani akiwa kwenye tafrija moja jijini Dar es Salaam, miaka hiyo ya 1960, Mwalimu alikaririwa akisema, angetamani ama visiwa vile vimezwe na Tanganyika au angeweza angevisukuma viende mbali kabisa. Kilichofuata baada ya hapo ni Mwalimu Nyerere kumshawishi Shekh Abeid Amani Karume kuunganisha nchi zao.
Zanzibar ilipata uhuru wake Desemba 10, 1963 chini ya Waziri Mkuu, Mohamed Shamte wa Chama cha ZNP chini ya utawala wa Sultan.
Hata hivyo, hali hiyo haikuwafurahisha baadhi ya Wazanzibari akiwamo John Okello aliyehamia kutoka Uganda. Huyo ndiye aliyesuka mipango ya mapinduzi ya Januari 12,1964. Mapinduzi hayo yanahusishwa na ASP kwa kuwa ndicho kilichokuwa kikipingana na ZNP. Wakati yalitokea, Karume hakuwepo Zanzibar
Post a Comment