Mugabe alikasirishwa na unafiki huu, je CCM?



NIANZE kwa kuweka wazi mapema kabisa kwamba, mimi ni miongoni mwa Watanzania wanaokerwa na mwenendo wa kikao cha Bunge la Katiba kinachoendelea mjini Dodoma.



Kwa kweli ukiangalia majadiliano ya Bunge hilo kupitia televisheni ya TBC, hupati picha kwamba wengi wa wabunge hao wanajua umuhimu na unyeti wa shughuli iliyowapeleka hapo. Sidhani pia kama wengi wanafahamu bahati waliyonayo ya kuwa sehemu ya historia ya mchakato wa kuipatia nchi yetu Katiba mpya.



Kama wote wangekuwa wanafahamu hivyo, wasingepoteza muda kubishana juu ya mambo yasiyo ya kimsingi katika kanuni zilizopendekezwa za uendeshaji wa bunge hilo.



Kwa kubishanabishana kila mara kwa hoja zile zile, na hata wazungumzaji wale wale kuruhusiwa kuendeleza hoja zile zile, kasi ya Bunge hilo imekuwa ndogo, na hivyo kusababisha lichelewe kuanza kuijadili rasimu yenyewe ambayo ndiyo hasa shughuli iliyowapeleka hapo Dodoma.



Baadhi yetu tumeanza sasa kuingiwa na shaka kama kweli siku 70 zilizotengwa kwa ajili ya kuikamilisha kazi hiyo zitatosha. Shaka hiyo inaleta hofu nyingine ya wapi yatapatikana mabilioni mengine ya fedha ya kugharimia siku nyingine za ziada za Bunge hilo kukamilisha kazi hiyo.



Shaka hiyo inatokana na ukweli kwamba Serikali hivi sasa imeishiwa pesa, na inashindwa kuwalipa watoa huduma mbalimbali mabilioni ya pesa wanazoidai; achilia mbali kuwalipa watumishi wake mishahara na stahiki zao nyingine kwa wakati.



Moja ya mambo yaliyonikera ya jinsi Bunge hilo linavyopoteza muda, ni ule mjadala uliochukua karibu wiki mbili wa iwapo itumike kura ya wazi au ya siri katika kupitisha vifungu vya rasimu hiyo ya Katiba. Baada ya kushindwa kufikia mwafaka wameamua kuliweka suala hilo “kiporo” hadi baadaye.



Natambua kwamba suala hilo ni muhimu na nyeti, lakini siamini kwamba unyeti wake ulihalalisha muda huo wote kutumika kujadili suala hilo tu. Kama wajumbe wote wangeweka kwanza mbele u-taifa kuliko u-vyama, kusingekuwa na kuvutana huko kwa muda mrefu ambako ni dhahiri kunawakera wananchi wengi.



Binafsi, siikubali lojiki inayotumiwa kudai uwepo wa kura ya siri katika kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba; ilhali suala hili linapaswa kuwa wazi kabisa ili wananchi wafuatilie (kupitia redio na TV) hatua zote mpaka mwisho kabisa wa Katiba kupatikana.



Kama kuna kasoro zilizofanyika huko nyuma kwenye mchakato zinazosababisha umuhimu wa kuwepo kura za siri, basi ni heri Upinzani ungedai kuvunjwa bunge hilo la Katiba na mchakato uanze upya kuliko kupigia debe kura za siri. Katiba ya nchi haiwezi kuandikwa katika mazingira ya usiri!



Nadiriki kusema kwamba hoja zinazotolewa na pande zote zinazovutana kwenye suala hilo (vyama vya Upinzani vs CCM) hazina mashiko, na wala haziwakilishi mamilioni ya Watanzania wanaowawakilisha. Kwa hakika, zinathibitisha tu jinsi u-chama na unafiki ulivyotamalaki katika siasa za Tanzania na jinsi wanasiasa walivyouteka kutoka kwa wananchi mchakato huo wa kupata Katiba mpya



Kwa bahati mbaya, unafiki huu ulianzia mwanzo kabisa katika upitishaji wa sheria iliyoanzisha mchakato wa kuandikwa Katiba mpya – sheria iliyompa Rais mamlaka makubwa .



Unafiki huo ukaendelezwa katika uteuzi wa wajumbe wale 201 wa Rais wanaoungana na Wabunge na Wawakiliashi kutoka Zanzibar kuunda Bunge hilo la Katiba.



Katika hatua zote hizo maslahi ya CCM yaliwekwa mbele kuliko maslahi ya Taifa. Yaani maslahi ya Watanzania zaidi ya milioni 40 hayakupewa uzito unaostahili; bali maslahi ya CCM ambacho wanachama wake nchi nzima wala hawafiki milioni 4!



Nina hakika kama unafiki usingetumika katika mchakato huu wa kuandika Katiba mpya, na kama kusingekuwa na ajenda ya ‘kubeba’ maslahi ya CCM katika Katiba mpya, hoja hiyo iliyopoteza muda mwingi ya iwepo kura ya siri au ya wazi, isingekuwepo kwa sababu lojiki ni kuwa na kura ya wazi.



Lakini vyama vya siasa vya Upinzani vinavyotaka pendekezo la kuwepo kwa serikali tatu lililomo kwenye rasimu hiyo vinajua kwamba pendekezo hilo haliwezi kupita kwa kura kama zitafanywa kuwa za siri.



Ni kwa nini Upinzani unaamini kwamba pendekezo hilo litakalowezesha kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika haliwezi kupita kama kura itakuwa ya wazi; ilhali unafahamu kuwa wana CCM ndani ya Bunge hilo la Katiba ni wengi



Kwa maneno mengine, kama Upinzani unatambua kuwa wanaCCM ndani ya Bunge hilo la Katiba ni wengi, kitabadilika nini hata kama kura itakuwa ni ya siri?



Jibu la maswali hayo ni kwamba Upinzani unatambua ya kuwa unafiki ndiyo sehemu ya utamaduni wa wabunge wengi wa CCM, na hivyo ikipigwa kura ya wazi, wote watajitia kupiga kura ya kukataa serikali tatu ingawa mioyoni mwao wanataka serikali tatu na si mbili.



Kwa maneno mengine, wabunge hao wa CCM hawana ujasiri wa kupigia kura ya wazi kile ambacho nafsi zao zinakitaka au kile wananchi wanaowawakilisha wanakita katika Katiba mpya, kwa sababu wanaogopa kuadhibiwa baadaye na chama hicho kama kura hizo si matakwa ya chama.



Lakini ikiwa kura ni ya siri, watapiga kura ya kutaka serikali tatu, lakini wakitoka nje ya ukumbi watajitia walipiga kura kufuata msimamo wa chama chao – yaani kura ya kukataa Serikali tatu – kumbe ni uongo mtupu!



Na hicho ndicho ninachokiita unafiki. Mbunge yeyote asiye na ujasiri wa kupiga kura ya wazi na kueleza wazi wazi msimamo wake hata nje ya Bunge, na badala yake hupendelea kura ya siri ili asifahamike alipigia kura upande gani, hastahili kabisa kuwemo katika Bunge la Katiba.



Ni heri upige kura ya wazi ulaaniwe na hao wasiopenda upande ulioupigia kura kuliko kupiga kura ya siri ya kinafiki; ukiwaaminisha wenzako kuwa umepigia kura msimamo wa chama kumbe sivyo! Huo ni unafiki wa kiwango cha juu!



Kinachonishangaza ni kwamba chama chenyewe cha CCM kinaukubali na kuulea unafiki huu, na ndiyo maana kinataka kura ya wazi, kwa sababu kinajua kwamba kama ikiwa ni ya siri wako wanachama wake ambao watapiga kura ya kukubali Serikali Tatu; ilhali hayo si maelekezo ya chama! Hiyo, CCM inaona ni dhambi kubwa inayostahili mjumbe huyo ‘kuadhibiwa’.



Maana yake ni kwamba, hata kama hatimaye kura itakuwa ni ya wazi, na pendekezo hilo la kutaka mfumo wa serikali tatu kukataliwa, bado ukweli utabaki pale pale kwamba ndani ya wabunge wa CCM kuna idadi kubwa tu ambayo hawaupendi mfumo wa serikali mbili lakini hawakupiga kura kukubali mfumo wa serikali tatu, kwa sababu ya kuogopa kuadhibiwa na chama chao!



Sasa, ni nani mwenye busara na hekima na anayeitakia nchi yetu mema anayeweza kuchekelea na kufurahia ‘ushindi’ wa kura za kinafiki katika suala hilo nyeti la uwepo wa serikali mbili au tatu?



Ndugu zangu, hakuna kitu kinachoudhi maishani kupita kile ambacho mtu anatenda au anazungumza kile asichokiamini moyoni. Na hii inanikumbusha mkasa mmoja unaomhusu Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe niliosimuliwa nilipokwenda katika nchi hiyo mwaka 2000 kuwa mmoja wa waangalizi wa kimataifa wa Jumuiya ya Madola wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.



Kwa mujibu wa simulizi hiyo, siku moja Rais Robert Mugabe aliitisha kikao cha Kamati Kuu ya ZANU-PF ili ajadiliane na wenzake mapendekezo yake ya marekebisho ya Katiba ya chama hicho ambayo alikuwa akitaka yafanywe.



Baada ya Rais Mugabe kuyawasilisha yeye mwenyewe mapendekezo hayo, alikaribisha maoni ya wajumbe hao wa Kamati Kuu ili ajue misimamo yao. Kila aliyesimama kuzungumza alianza kwa kummwagia sifa kemkem Rais Mugabe, na mwisho kutamka kuwa anayaunga mkono mapendekezo hayo 100 kwa 100!



Baada ya wote kuzungumza na kumsifu sana kwa kufikiria kuifanyia Katiba ya ZANU-PF mabadiliko hayo, Rais Mugabe aliomba wasaidizi wake wagawe vikaratasi vya kupigia kura ya siri mapendekezo hayo.



Matokeo hayo ya kura ya siri yaliposomwa mbele ya Rais Mugabe na mbele ya wajumbe hao wa Kamati Kuu, yalionyesha kuwa ni wajumbe wanne tu kati ya 22 waliyoyaunga mkono. Wengine wote 18 walipiga kura ya kuyakataa!



Matokeo hayo yaliposomwa, Rais Mugabe alifura kwa hasira; huku presha ikimpanda, na inasemwa kwamba kama asingeondolewa ukumbini mapema pengine angelikufa hapo hapo!



Kilichomfurisha Rais Mugabe kwa hasira ni ule ufahamu wa dakika za mwisho ya kwamba kumbe wajumbe wote wale 18 waliozungumza na kumsifu mno kwa kuibuka na mapendekezo hayo walikuwa ni wanafiki tu wanaompaka mafuta kwa mgongo wa chupa!



Inaelezwa nchini Zimbabwe kuwa kama kura zile zisingekuwa za siri; yaani kama zingekuwa ni za mjumbe mmoja mmoja kusimama na kusema “ndiyo” au “hapana”, wote 22 wangesema “ndiyo”. Lakini si kwenye kura ya siri ambako unafiki hutawala!



Sasa, ni heri kwa Rais Mugabe ambaye yeye alifura kwa hasira baada ya kugundua kwamba kumbe wajumbe wa Kamati Kuu yake ni wanafiki; kuliko CCM yetu hii. CCM yetu hii inajua mapema kabisa kwamba “unafiki” utatumiwa na wanachama wake kwenye upigaji kura kipengele hicho cha pendekezo la uwepo wa serikali tatu, lakini haishtuki wala kuonyesha kujali.



Hata kama wanachama wake watapiga kura ya wazi kukataa serikali tatu ilhali mioyoni wanazitaka serikali hizo kiasi kwamba kama kura ingekuwa ya siri wangepiga kukubali ziwepo, CCM haijali! Na hapa tunazungumzia Katiba ya nchi.



Rais Mugabe yeye hakujua kwamba kura zikiwa za siri wajumbe wa Kamati Kuu yake ya ZANU-PF wangepiga kura kuyakataa mapendekezo yake japo kwenye mjadala waliyasifu sana, lakini CCM yetu inalijua hilo mapema, na wala haijali.



Yaani haitaona soni kufurahia na ‘kusherehekea’ ushindi wa kura za kinafiki – yaani ushindi wa kukwamisha ujio wa serikali tatu; ilhali mioyoni mwa wanachama wake waliopiga kura hiyo ya wazi wamo wengi wanaotaka serikali tatu na si mbili zinazotakiwa na CCM!



Nirudie: Heri Rais Mugabe ambaye baadaye alifura kwa hasira baada ya unafiki wa wajumbe wa Kamati Kuu yake kudhihirika mbele yake kwa kura hiyo ya siri, kuliko CCM ambayo yaelekea “imeubariki” na kuukubali unafiki huu hata kabla upigaji kura wenyewe haujawadia!



Nirudie kwa mara ya mwisho: Kama kuna mazingira yanayolazimisha umuhimu wa kuwepo kura za siri katika bunge hili la Katiba na si kura za wazi, basi ni heri kulivunja Bunge hili la Katiba na mchakato uanze upya ili mazingira hayo yaondolewe ili kura ziwe za wazi kuliko kukubali kura za siri. Katiba ya nchi haiwezi kutungwa katika mazingira ya usiri!



Ni Katiba mpya ya namna gani tutakayoipata juu ya msingi huu wa upigaji kura za siri na za kinafikiNi heri Bunge hili la Katiba likavunjwa, tukaanza upya, kuliko kukubali kuwa na kura za siri kwenye suala linalopaswa kuwa na uwazi kuliko masuala yetu yote mengine – yaani suala la kuipatia nchi Katiba mpya chanzo gazeti la raia mwema

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top