
WAZIRI Mkuu wa zamani na makamu wa kwanza wa rais ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema kutikishwa kwa Muungano kumesababisha Rais wa Jamhuri kutofanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ahadi kwa upande wa Zanzibar.
Akiwasilisha rasimu ya Katiba Mpya katika Bunge la Katiba, Warioba alisema sura ya Serikali ya Muungano inaonyesha kuegemea zaidi upande wa Tanzania Bara.
“Kati ya Wizara 24 ni wizara mbili tu ndizo zinashughulikia mambo ya Muungano pekee. Wizara kumi zinashughulikia mambo ya Tanzania Bara na Wizara kumi na mbili zinashughulikia mambo mchanganyiko ambayo mengi ya mambo hayo yanahusu Tanzania Bara.
“Kwenye utawala, viongozi wakuu wengi wa wizara wanatoka Tanzania Bara. Hivi sasa ni Katibu Mkuu mmoja tu ndiye anayetoka Zanzibar. Hali hii inatokana na ukweli kwamba Serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo yasiyo ya Muungano na ndiyo imeifanya Tanganyika kuonekana imevaa koti la Muungano.
“Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeona hakuna njia ya kubadili hali hii kwa sababu Serikali ya Muungano haina mamlaka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar. Mawaziri na Serikali kwa ujumla, wanalazimika kupanga maendeleo na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Tanzania Bara kuliko kwa Zanzibar.
“Zanzibar hufanya mipango yake ya maendeleo, lakini, ili kupata rasilimali kama mikopo na misaada, ni lazima Serikali ya Zanzibar ipitie Serikali ya Muungano, jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi,” alisema.
Aliweka bayana kwamba njia pekee ambayo ingefanya maendeleo ya Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka mambo yote ya Zanzibar chini ya Serikali ya Muungano, yaani kuwa na Serikali Moja.
“Lakini kama nilivyosema, wakati wa kukabidhi rasimu kwa marais wetu, muundo wa Serikali moja una changamoto nzito. Waasisi waliona matokeo ya muundo huo ni Zanzibar kumezwa na Tanganyika. Tume ilipokuwa inakusanya maoni, wananchi wengi, hasa Zanzibar, walionyesha hofu hiyo ni kubwa sana hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzoni. Kwa hiyo, tathmini ya Tume ni kwamba Muundo wa Serikali moja hauna uhalisia,” alisema.
Mgongano wa Katiba
Warioba alisema eneo jingine lenye matatizo ni mgongano kati ya Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar kwamba ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Jambo hili limeleta mgongano wa Katiba. Juhudi zilizofanywa na pande zote mbili hazikufanikiwa kuondoa mgongano huo. Katika muafaka wa mwaka 1994 Serikali zote zilikubaliana kwamba Zanzibar ifanye mabadiliko kwenye Katiba yake ili mgongano huu wa Katiba uondolewe.
“Lakini hadi sasa muafaka haujatekelezwa. Zaidi ya hapo, mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya kwanza yaliyofanywa mwaka 2010 yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati ya nchi mbili zinazounda Muungano wakati Katiba ya Jamhuri inaelekeza kwamba Tanzania ni nchi moja.”
“Mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya Serikali ya Muungano kwenda Zanzibar. Kwa mfano, Katiba ya Jamhuri inampa Rais wa Jamhuri madaraka ya kuigawa nchi katika maeneo. Lakini Katiba ya Zanzibar imeyahamisha madaraka hayo kwenda kwa Rais wa Zanzibar.”
“Wakati wa kukusanya maoni ya wananchi, Tume ilibaini kwamba haitakuwa rahisi kubadili Katiba ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuonekana kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano badala ya kuwa na sura ya nchi. Mabadiliko ya aina hiyo yatahitaji kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza,”
“Kwa tathmini ya Tume, baada ya kuwasikiliza wananchi wa Zanzibar, ni dhahiri kwamba uwezekano wa kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ili Zanzibar iwe sehemu ya nchi moja badala ya kuwa nchi, ni mdogo sana,” alisema.
chanzo raia mwema.
Post a Comment