IPTL maji shingoni yaomba Mahakama Kuu Dar imnyamazishe Kafulila



Dar es Salaam. Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imewasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikiomba itoe amri ya kumfunga mdomo Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila.


Kampuni hiyo imewasilisha maombi hayo siku chache tu baada ya kumfungulia mashtaka ya kashfa mbunge huyo kwa kuituhumu kujipatia Sh200 bilioni kutoka katika Akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT) kwa njia zisizo halali.


Kesi hiyo imefunguliwa na IPTL ambayo ni mdai wa kwanza kwa kushirikiana na Kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hizo, Harbinder Sigh Seth. Katika maombi ya sasa, walalamikaji wanaiomba Mahakama itoe amri ya zuio la muda kwa mbunge huyo asiendelee kutangaza taarifa za kashfa wala kuzungumza jambo lolote dhidi yao, hadi kesi ya msingi itakapoamuriwa na imwamuru alipe gharama za kusikiliza maombi hayo.


Maombi hayo namba 306 ya 2014, yaliwasilishwa mahakamani hapo na wakili wa walalamikaji hao, Agustine Kusalika na yanasikilizwa na Jaji Rose Temba. Yalitajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Alhamisi iliyopita na yamepangwa kutajwa tena Agosti 28, 2014.


Katika kesi ya msingi namba 131 ya mwaka 2014, walalamikaji wanaiomba mahakama imwamuru mbunge huyo awalipe fidia ya jumla ya Sh310 bilioni kutokana na madai hayo ya kuwakashifu.


Wanadai Sh210 bilioni kama fidia kutokana na kashfa hizo, Sh100 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana kashfa hizo na riba kwa kiwango cha mahakama, gharama za kesi na mdaiwa awaombe radhi.


Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, IPTL ilijipatia fedha hizo kihalali, baada ya uamuzi wa maombi ya mgogoro baina yake, dhidi ya Kampuni VIP Engineering and Marketing Limited na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Inadai kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo ya Escrow, iliyofunguliwa kutokana na mgogoro huo ili kusubiri hatima yake na kwamba baada ya kumalizika Mahakama iliamuru kuwa IPTL ina haki kuchukua fedha hizo.


Hati hiyo imedai kuwa mdaiwa anajua kilichoendelea mahakamani katika maombi hayo baina ya mdaiwa wa kwanza na VIP, lakini aliamua kutangaza kinyume kuhusu akaunti ya Escrow.


Imedai kuwa cha kushangaza na pasipo na uhalali wowote, mdaiwa katika matukio tofautitofauti ndani nje ya Bunge aliamua kusambaza taarifa za kashfa dhidi ya mdai wa kwanza na wa tatu, kwenye mitandao ya kijamii ya Jamii Forum, Twitter na Facebook. Hati hiyo ya madai inaeleza kuwa kitendo cha mdaiwa kutoa taarifa hizo za kashfa kimesababisha jamii kwa jumla kuamini kuwa kweli mdai wa kwanza amejipatia fedha hizo isivyo halali na kwamba anahujumu rasilimali zao.


Pia hati hiyo ya madai imesisitiza kuwa kitendo cha mdaiwa kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwa jamii si tu kimeshusha hadhi ya mdai, bali pia kimesababisha hasara ya kibiashara nchini na kimataifa.


Akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP).


Alisema kampuni hiyo inayomilikiwa na Singasinga iliidhinishiwa kuchota fedha hizo isivyo halali na kwa udanganyifu mkubwa kwamba PAP ilikuwa imeinunua IPTL wakati jambo hilo siyo la kweli.soma zaidi

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top