CCM yajiweka kando kauli ya Mwigulu



Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejiweka kando na kauli ya naibu katibu mkuu wake, Mwigulu Nchemba aliyoitoa kwamba Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea kutokana na uwezekano mdogo wa wajumbe wake kufanya uamuzi.


Mbali na hilo, chama hicho kimemtaka mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wake kutogeuza rasimu mradi binafsi.


Juzi, akiwa bungeni Nchemba ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi na naibu waziri wa fedha, alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.


Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema msimamo wa chama hicho ni Bunge la Katiba kuendelea kuichambua Rasimu ya Katiba na si vinginevyo.


“Alichokizungumza Mwigulu ni mtazamo wake binafsi, ndiyo maana katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya ilielezwa wazi kwamba watu wavumiliane katika utoaji wa maoni na mitazamo yao,” alisema Nape.


Nape alisema Mwigulu akiwa ndani ya Bunge hilo anazungumza akiwa mjumbe wa Bunge la Katiba na si kama kiongozi wa chama kwa maelezo kuwa Katiba si ya chama cha siasa, bali ya Watanzania wote.


Kuhusu upigaji wa kura kwa ajili ya kufanya uamuzi, Nape alisema kuwa hata kama wajumbe wa Ukawa watarejea bungeni, hakuna anayejua kuwa watapiga kura ya aina gani.


“Hata Ukawa wakirejea bungeni huwezi kujua watapiga kura ya aina gani, inawezekana wakawepo na hiyo theluthi mbili pia isipatikane.


Kwa idadi ya wajumbe waliofika bungeni hadi sasa akidi si tatizo tena maana hata hao Ukawa baadhi yao wameanza kurejea bungeni.”


Nape alisema Katiba si ya CCM wala Ukawa na kwamba wapo Watanzania wengi ambao wanakubaliana na uamuzi wa kuendelea kwa hatua nyingine za kupata Katiba Mpya. “Katiba ni mali ya Watanzania na waliopo bungeni ni zaidi ya vyama vya siasa. Kama kundi kubwa limeridhia na jingine ambalo hata kiganjani halijai limesusa, sisi tutaendelea tu,” alisema endelea bofya hapa

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright 2025 WORLD OF TODAY | Designed By Code Nirvana Published.. Blogger Templates