Mbowe: Usaliti hauna msamaha



Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake hakitavumilia vitendo vya usaliti na kwamba mwanachama yeyote atakayekiuka maagizo ya chama hicho atachukuliwa hatua kali.


“Katika hili hatutakuwa na mchezo na naomba niweke wazi kabisa kwamba usaliti hausameheki. Tuna vikao vya chama vinakuja siku za karibuni mtu yeyote ambaye atabainika kusaliti uamuzi wa chama, uwe wa Kamati Kuu au mwingine wowote, tutachukua hatua hata kama ni kumfukuza uanachama,” alisema Mbowe.


Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia taarifa za kuwapo bungeni, Dodoma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kinyume cha makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Wabunge hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu), John Shibuda (Maswa Mashariki) na Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye aliwasili jana na kwenda kushiriki kwenye kikao cha kamati namba 10 kilichokuwa kikifanyika Ukumbi wa Internet, Chuo cha St. Gaspar.


Mbowe alisema baada ya viongozi wakuu wa Ukawa kukubaliana kwamba hawatashiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu, kila chama kiliwaelekeza wabunge wake kuhusu msimamo huo ambao pia uliridhiwa na vikao vya vyama husika.


“Sisi suala hili limepitishwa na Kamati Kuu ya Chadema, sasa wewe ni nani kukataa, kupinga au kwenda kinyume cha matakwa ya Kamati Kuu? Ole wake mtu atakayethubutu kushiriki hivyo vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:


“Wakati tunagombea ubunge 2010 hakukuwa na ahadi kwamba kutakuwa na Bunge la Katiba, hili limetokea tu, sasa kama sisi kwa masilahi mapana ya umma tunauona mchakato hauko sawa, kwa nini wewe ulazimishe kushiriki, unakwenda Dodoma kumwakilisha nani?”


Vyama vingine vyenye wabunge ambavyo pia wanachama wake wamesusia Bunge Maalumu ni NCCR Mageuzi na CUF. Kadhalika Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ni miongoni mwa waliosusia vikao hivyo.


Kauli ya Arfi


Akizungumzia uamuzi wa kushiriki Bunge alisema licha ya kwamba yeye ni mwanachama wa Chadema, ameingia bungeni akiwa mwakilishi wa wananchi katika kutunga Katiba na kwamba ndani ya Bunge hakuna vyama, bali wawakilishi wa wananchi.


Alisema anaamini katika muungano wa Serikali tatu na kwamba kama kuna mgongano uliojitokeza lazima uamuliwe ndani ya mkutano wa Bunge na kwamba kutoka nje ya Bunge ni dalili ya woga na yeye siyo mwoga. “Ndiyo nipo kwenye kikao cha kamati namba 10, hivi sasa hatujamaliza,” alisema Arfi kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi baada ya mwandishi wetu kumuuliza jana endelea bofya hapa

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top