Dodoma. Mjumbe mwingine wa Bunge la Katiba kutoka Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana alionekana kwenye Viwanja vya Bunge na alisaini za mahudhurio.
Mjumbe aliyeonekana jana, Leticia Nyerere wa viti maalumu, Chadema, anafanya idadi ya wajumbe waliotinga kwenye viwanja hivyo hadi sasa kufikia watatu baada ya Chiku Abwao (viti maalumu Chadema) kuonekana juzi na Clara Mwatuka (viti maalumu CUF) kuonekana Jumapili.
Nyerere hakuwa akihudhuria vikao baada ya Ukawa kutangaza kususia Bunge mwezi Aprili na jana hakupatika kuzungumzia suala hilo.
Kuonekana kwa mjumbe hao kunaweza kutafsiriwa kuwa ni kubomoka kwa ngome za Vyama vya Chadema, NCCR na CUF vinavyounda umoja huo kwani tangu awali walikubaliana kutoshiriki shughuli za Bunge hadi pale watakapofikia makubaliano ya hoja zao.
Msimamo wa chama hicho chini ya viongozi wao ni kutohudhuria shughuli za Bunge Maalumu la Katiba hadi kutakapokuwa na mwafaka wa mwenendo wa shughuli za chombo hicho, ambacho jana kiliendelea na vikao vya kamati kujadili sura 15 za Rasimu ya Katiba.
Ukawa wanadai CCM imepora mawazo ya wananchi na kwamba kuna mpango wa kuchakachua rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza mambo yenye masilahi kwa chama hicho na Serikali yake.
Vyama vinavyounda Ukawa vinadai kuwa kuzungumzia muundo wa Muungano wa serikali mbili ni kuchakachua maoni ya wananchi ambao walitaka muundo wa serikali tatu kama ilivyo kwenye Rasimu ya Katiba.
Bunge jana lilikutana katika kamati zake 12 zilizotawanyika katika kumbi mbalimbali kwa ajili ya kupitia sura 15 za rasimu ya Katiba ingawa wajumbe wengine walilazimika kuanzia safari zao bungeni ili waweze kujisajili.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano ambayo Nyerere ni mjumbe, Hamad Rashid Mohamed alisema mjumbe huyo hakuwa amefika katika kikao cha jana ambacho pia kilifanyika Dodoma Hoteli.
Kuhusu mwenendo wa kikao cha kamati yake, Mohamed alisema hadi jana mchana walikuwa wamekamilisha kupitia sura ya pili na kwamba jioni walitarajia kuifanyia kazi sura ya tatu.
Kuhusu changamoto ya muda, Mohamed alisema: “Hiyo ndiyo hali halisi na tukiweza tutapiga kura kupitisha ibara hizo leo (jana), kama tukishindwa basi tutapiga kura kesho (leo) ili mradi tutumie muda ambao upo tufanye kazi kwa ufanisi.” mwananchi
Post a Comment