Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Hamphrey Polepole akizungumza kwenye mjadala wa wazi kuhusu Katiba mpya, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam. Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema makongamano na mijadala inayohusu Katiba mpya yataendelea kwa sababu ni ya lazima pia ni haki ya kikatiba.
Akizungumza kwenye Kongamano la Katiba lilioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jana, Polepole alisema mtu anayezuia wananchi kuendelea kuzungumzia Katiba amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa nchi.
Huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo, Polepole alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, inayoheshimu haki za binadamu na utawala wa kiraia. Hivyo inashangaza kusikia kuna kiongozi anajaribu kuwafunga mdomo wananchi.
“Nimesikia mtu mmoja anasema msifanye makongamano. Sijamfahamu vizuri, lakini ninachokiona ni kwamba anaendelea kupoteza sifa za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama alikuwa anataka kufanya hivyo,” alisema Polepole.
Ingawa hakumtaja jina, juzi Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi hivi karibuni walikaririwa wakihoji uhalali wa mijadala inayoendelea sasa kuhusu Katiba Mpya.
Sitta, akiongoza kikao cha Bunge la Katiba juzi, alimtaka Waziri wa Habari na Utamaduni kuvichunguza vyombo vya habari vinavyorusha matangazo ya watu aliodai wanapotosha ukweli kuhusu Katiba.
Ingawa Sitta hakukitaja chombo chochote, alikuwa akielekeza maoni yake kwenye mdahalo uliorushwa Jumatatu wakati wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na Jaji Joseph Warioba waliposhiriki na kujibu hoja mbalimbali zinazoonekana kuwa na utata kwenye Rasimu ya Katiba.
Polepole aliongeza kusema: “Mimi nimsihi tu kwamba kuongea ndiyo haki yetu na jadi yetu. Wakati tupo kwenye Tume, kila mtu alikuwa anaongea na wakati huo kazi ilikuwa ngumu zaidi kwa sababu tulikuwa hata hatufahamu rasimu itaonekana namna gani.”
Alisema kipindi hicho vyama vya siasa ndiyo vilikuwa mstari wa mbele kuongea na kushinikiza wananchi kusema maneno yasiyokuwa ya kwao na kushauri kuwa ni vyema kama viongozi hao wangewapa watu elimu ya uraia.
Huku akiendelea kushangiliwa, Polepole alihoji: “Sasa nashangaa tena hivi sasa tunaambiwa tusizungumze, tufunge midomo, tukae kimya. Kwani sisi kazi yetu ni kazi gani? Tusiongee halafu tukafanye kazi gani? Napenda nipeleke salamu hizo,” alisema.
Aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuacha kuwapuuza wananchi kwa kudhani kwamba hawajui wanachotaka na kwamba ni kosa kubwa kuwaambia Watanzania kitu cha kufanya, wakati wao wanajua wanachofanya.
“Hizo zama zimepita na sidhani kama zipo kwenye ulimwengu wa leo. Haikuwa na maana kuwafuata na kuwaambia watoe maoni, halafu mwisho wa siku waletewe kitu cha ajabu,” alisema.bofya hapa kuendelea
Post a Comment