Dk slaa atoa kalipio kali kwa Rais Kikwete




Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amesema Rais Jakaya Kikwete asitumie kivuli cha mapumziko ya sikukuu kuchukua uamuzi dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anayehusika katika kashfa ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow ya Sh306 bilioni.


Pia, amemtaka Rais Kikwete kuwaeleza ukweli Watanzania kuhusu kigogo wa Ikulu aliyenufaika na mgawo wa fedha, Sh800 milioni za akaunti hiyo zilivyotumika na mnufaikaji alikuwa nani.


Dk Slaa aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi wa Somangila-Kigamboni Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa kuwachagua wenyeviti sita kati ya 13 wa Ukawa wa kata hiyo yenye mitaa sita.


“Tunamtaka haraka Rais Kikwete amfukuze kazi Profesa Muhongo, asiseme anakula ‘bata’ Msoga (Kijijini kwake Bagamoyo mkoani Pwani) eti sikukuu...Tumemchagua atusimamie na kutuongoza kwa saa 24 kwenda kula Krismasi huku wagonjwa wanakufa hospitalini ni dharau kwa Watanzania,” alidai.


“Rais ni mtumishi wa Watanzania, wachache hawawezi kunufaika na mabilioni hayo huku wengi wanaendelea kusota na ugumu wa maisha...Unakulaje ‘bata’ wakati Watanzania kila kona wanataka uchukue uamuzi kwa masilahi ya Taifa, hiyo ‘bata’ kweli au ndiyo msemo unaosema ukimwaga mboga mimi ninamwaga ugali anamwogopa Muhongo kumwajibisha?” alisema Dk Slaa.


Alisema kumfukuza kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka pekee hakutoshi, huku wengine waliofanya makosa kama hayo bado wanaendelea kuzunguka mitaani.


“Huyu Tibaijuka ametolewa kafara tu, kuna kigogo wa Ikulu ambaye anaratibu shughuli za Ikulu za nchi nzima (jina tunalihifadhi) alipewa Sh800 milioni lakini yeye hajaguswa, sasa Rais Kikwete atueleze kwa nini alimchukulia hatua Profesa Tibaijuka na huyu kigogo wake amemwacha kuna nini hapa kinachoendelea,” alisema Dk Slaa.


Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka huu, Rais Kikwete alisema amemweka kiporo waziri huyo hadi atakapopata ufafanuzi wa mambo kadhaa na kwamba atakapojiridhisha ataujulisha umma.


Dk Slaa alisema, “Rais Kikwete anatumia maneno ya yasiyofaa katika jambo lenye masilahi mapana, kumweka kiporo kisheria au utawala bora halipo na mimi kwa miaka zaidi ya 60 nimekuwa Padre, Mbunge kwa miaka 15 na sasa mtumishi wa umma sijawahi hata siku moja kusikia mtu badala ya kuchukulia hatua anawekwa kiporo.”


Juzi, Ikulu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema suala la Profesa Muhongo litatolewa uamuzi wakati wowote baada ya mapumziko ya sikukuu.


Rais Kikwete bado hajakamilisha kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa hatua alizozichukua.


“Unakumbuka Rais alichosema? Bado analifanyia kazi, atakapomaliza tu mtajulishwa, sasa hivi ni kipindi cha sikukuu,” alisema Sefue. mwananchi

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top