Ataja sifa za mtu anayefaa kuwa rais ajaye, soma hizo sifa hapa







WAKATI nchi ikikaribia kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataka Watanzania kuwa waangalifu katika kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo wa kulifikisha mbali taifa la Tanzania.

Aidha, ametaja sifa 13 za kiongozi anayefaa kuiongoza Tanzania huku akionya kuwa katika nchi nyingi viongozi wasiofaa, huwa chanzo cha kuvunjika kwa amani na utulivu na kusisitiza umuhimu wa kuwaweka madarakani viongozi bora.

Pia ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vyombo vingine vinavyosimamia uchaguzi na vyama vya siasa, kutenda haki, akisema ikitendeka pasipo kutia shaka, uchaguzi utakuwa wa amani na utulivu wa nchi utaendelea kudumu.

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa, alisema hayo jijini Mbeya jana, ambako alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tamasha la Krismasi lililobeba dhima ya kuombea amani ya nchi.

Alitaja baadhi ya sifa za kiongozi ajaye kuwa ni pamoja na kuwa na uzalendo kwa nchi na wananchi wake, mwenye upeo, mwenye kuweka madarakani serikali inayowajibika, mwenye kupambana na umasikini, anayeweza kukabili tatizo la ajira, anayeweza kuboresha huduma za jamii na pia mwenye uthubutu wa kupambana na rushwa.

Nyingine ni kukabili ufisadi, tatizo la dawa za kulevya, mwenye mikakati ya kukuza uchumi wa nchi, anayeweza kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. Akizungumzia uzalendo, alisema: “Uzalendo una tafsiri pana.

Mzalendo wa kweli ni mkweli kwa nchi yake, ni mpenzi wa nchi yake na watu wake, husimamia haki na hujali maslahi ya umma badala ya maslahi yake binafsi.

Watanzania tunahitaji kupata kiongozi mzalendo wa kweli ambaye atajali maslahi ya umma kwanza kabla ya kitu chochote. “Kiongozi mzalendo atajali hali nchi yake kwa leo na baadaye na atapenda kuilea na kuitunza Tanzania ili iweze kulea vizazi vinavyokuja baadaye kwa kujali mabadiliko ya tabianchi na kuzuia au kupunguza madhara yanayotokana na mabadiliko hayo.

Kiongozi mzalendo atajenga heshima ya nchi ili Tanzania iwe na sifa mbele ya uso wa dunia. “Kiongozi mzalendo atapenda kuwainua Watanzania wote kwa kadri inavyowezekana ili wawe na maisha bora badala ya kulenga kundi dogo ambalo labda yeye ana maslahi nalo.

Watanzania mwakani tunayo nafasi ya kumweka kiongozi wa aina hiyo na tunayo nafasi ya kuwaweka viongozi katika ngazi zingine, ambao nao watakuwa na sifa hizo,” alisema. Aliongeza kuwa baadhi ya watu hujithamini wao kwanza na kwamba hilo limekuwa likiwakumba viongozi wengi.

”Watu huangalia zaidi kujitajirisha hata kama ni kwa gharama kubwa kwa nchi na taifa la baadaye. Hili ni jambo la hatari sana kwa amani ya nchi, likiachiwa kuota mizizi, hivyo ni vyema kiongozi tutakayemtafuta mwakani awe mzalendo wa dhati adhibiti hali hiyo,” alisema.

Mwenye upeo Alisema nchi inahitaji kiongozi mwenye kuielewa nchi yake vizuri, kuwaelewa Watanzania vyema na kuyaelewa matatizo ya Watanzania kwa dhati na matatizo hayo yawe yanagusa moyoni mwake.

“Kiongozi huyo lazima aelewe Watanzania wanataka nini, yeye anataka kutupeleka wapi na anatufikishaje huko. Asiwe kiongozi wa kutuburuza anavyotaka yeye au kiongozi asiyejali yanayotupata ambayo yana maumivu kwetu.

Tunataka kiongozi anayeelewa mipango ya taifa na kuifuata kama ilivyopangwa siyo kubuni mipango mipya kila kukicha wakati mipango ya awali haijatekelezwa,” alisema.

Kuhusu utawala wa sheria, alisema nchi nyingi zimetumbukia katika machafuko kwa sababu viongozi wao wakati mwingine huweka katiba na sheria kando na kutawala kwa imla kadri wanavyoona inafaa, hivyo kwa Tanzania, utaratibu unaomweka madarakani kiongozi ni vyema kiongozi huyo akauheshimu na kuutii.

“Tunahitaji kupata kiongozi ambaye ataheshimu Katiba ya nchi na sheria mbalimbali zinazowekwa mara kwa mara kwa maslahi ya umma. Aidha, kiongozi lazima awe tayari kuilinda na kuikuza demokrasia ya vyama vingi, ambayo imeanzishwa kwa maslahi ya wananchi.

“Ili aina hii ya utawala uwasaidie wananchi ni lazima vyama vya upinzani navyo viwe na nguvu ya kuwa changamoto kwa chama tawala na hiyo ndiyo maana na faida ya demokrasia ya vyama vingi,” alisema. habari leo

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top