Haya ndio Mambo mazito yanayoitesa CCM



Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za rushwa inayodaiwa kutolewa na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi mbalimbali ukiwamo urais.


Hali hiyo inabainishwa na kauli za baadhi ya makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao wameamua kulalamika waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii.


Moja ya kauli hizo ni ile iliyotolewa juzi na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwenye akaunti yake ya Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo wa uongozi. Aibu.”


Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu licha ya kwamba wapo wengi wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika katika mtandao ameandamwa na baadhi ya watu huku wengine wakimtolea lugha chafu.


“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni mawazo huru ambayo anayaamini.


Waliyonena kuhusu rushwa


Kauli ya Kagasheki haina tofauti na zile zilizowahi kutolewa na makada wengine, akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya chama hicho na Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka madaraka.


Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alimwambia mwandishi wetu jana kuwa suala hilo linafuatiliwa kwa karibu na dawa yake itaiva Februari baada ya kamati yake ya maadili iliyofuatilia kutoa tathmini yake.


“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda kamati ya ufuatiliaji harakati za kila mmoja kuona je, yale tuliyomtaka kutoyafanya ametekeleza? Sisi tunaheshimu vikao vyetu, hivyo tunasubiri kamati hiyo itakapotuletea taarifa yake.


“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”


Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa chama hicho waliopewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na ndani ya jamii.


Mangula alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa baadhi ya wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi. mwananchi

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top