Morogoro. Wanawake 14 na wanaume wawili wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu kwa makosa ya kufanya biashara ya ngono katika maeneo mbalimbali.
Kukamatwa kwa watu hao kulitokana na Jeshi la Polisi kufanya msako katika maeneo ya Kahumba na Itigi Masamvu.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu za Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa wananchi wa mkoani hapa.
Alisema wafanyabiashara hao wa ngono pia wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya wizi na uhalifu mwingine.
Kamanda Paulo alisema polisi wamejipanga kukabiliana na uhalifu na vitendo vya kuvunja amani vitakavyojitokeza wakati wa sikukuu hizo.
Alisema kuwa watu hao maarufu kwa biashara ya uchangudoa na ukahaba, walikamatwa Desemba 21 mwaka huu saa 6:00 usiku.
Alisema siku iliyofuata walifikishwa mahamani na kukiri shtaka na hivyo kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu ili iwefundisho kwa wengine.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Paulo alisema wataendelea kufanya msako huo katika maeneo mbalimbali ili kukomesha biashara hiyo haramu.
Pia, alisema kuwa polisi watafanya doria kwa miguu, magari pamoja na mbwa katika nyumba za ibada, kwenye mikusanyiko ya watu ikiwamo Kituo cha Mabasi cha Msamvu na barabara kuu zinazokatiza Morogoro kuelekea mikoa mingine.
Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha dhana ya ulinzi jirani na ukamataji salama inazingatiwa.
Aliwakumbusha wananchi kuziacha nyumba zao zikiwa na ulinzi wa uhakika katika kipindi cha sikukuu. Kamanda alisema hata wale wenye vyombo vya usafiri hasa magari wanapaswa kuhakikisha wanavifunga kabla ya kwenda kwenye nyumba za ibada MWANANCHI
Post a Comment