Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbroad Slaa,
amehitimisha ziara yake wilayani Igunga na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
kuwawajibisha Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Jeshi la Polisi
pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutokana na sakata la
Operesheni Tokomeza Ujangili (OTU).
Vile vile,
amemuonya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kwa kusema kuwa
anakabiliwa na tishio la kufukuzwa uanachana kutokana na kuwepo na
vikaratasi vinavyogawanywa kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Barafu, Igunga,
Dk Slaa alisema kwamba Rais Kikwete anapaswa kuwawajibisha iwapo
hawatafanya hivyo ili kujijengea heshima katika kipindi cha miaka miwili
ya utawala wake uliobakia.
Alisema
katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyowasilishwa Bungeni,
Serikali na vyombo vya dola vimeumbuka kutokana na kubainika kuwa
vilihusika katika kuwatesa raia, kuwaua ikiwa ni pamoja na kupora mali
zao, hivyo kwa vile watekelezaji walikuwa ni idara ya usalama wa Taifa,
Polisi na Jeshi la Wananchi bado wakuu wake wanapaswa kujiuzulu kutokana
na aibu hiyo.
“Kule
Serengeti mkoani Mara walimkamata kijana wetu, tena Diwani wa Chadema na
kumlazimisha kukiri kuwa alikuwa akimiliki bunduki na kuwinda tembo,
alipokataa walimpiga shoti ya umeme, wakamwekea waya wa baiskeli na
kuusokota, lakini kule Babati wamemkamata mama wakidai kuwa alikuwa
akiua tembo na kumbaka kwa zamu,” alieleza Dk Slaa.
Alisema
kwamba mateso haya yanafanyika sasa na vyombo vya dola baada ya kufanywa
kwa muda mrefu na watendaji wa vijiji, wakuu wa wilaya na wakuu wa
mikoa, lakini licha ya kwamba njia ya kuondoa kero hizo za manyanyaso
kwa wananchi hazihitaji fedha, lakini bado Serikali imekuwa ikishindwa
kuchukua hatua.
Alisema watu
wanabambikiwa kesi za mauaji kwa makusudi, Serikali ipo ikiangalia
pamoja na vyombo vya usalama wa Taifa, hivyo kuwataka wakuu wake nao
kufuata njia za mawaziri wanne kwa kujiuzulu ili kulinda hadhi ya
taasisi zao.
“Polisi
walikamata vijana wetu wa Chadema wakati walipokuwa wakitaka
kutubambikia kesi ya ugaidi, waliwapeleka kule Tabora waliwatesa na
umeme mateso makali sana, waliwachanachana kwa visu vya bunduki sehemu
zao za siri na kuwawekea waya, mateso haya ni makali na yamefanywa kwa
vijana ambao wameoa juzi, bora hata wangefanya kwangu mimi mwenye umri
mkubwa,” alieleza kwa masikitiko.
Alipokuwa
katika Wilaya ya Nzega, Dk Slaa, alimuonya Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe kuwa anakabiliwa na tishio la kufukuzwa uanachama kwa kile
kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nzega Mjini alisema chama
kimepokea taarifa za mpango wa kundi la watu ambao wanasadikiwa kuwa
wafuasi wa Zitto kupitisha karatasi na kusainisha majina ya wanachama
kwa lengo la kuandaa pingamizi dhidi ya uamuzi wa chama jambo ambalo
alisema litamponza.
Post a Comment