Dodoma.Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini imefichua kuwapo kwa utoroshaji mkubwa wa madini unaofanywa na
baadhi ya wachimbaji wadogo na kubainisha tani 18 za dhahabu hutoroshwa
kila mwaka kwenda nje.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo Bungeni jana,
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Victor Mwambalaswa alisema taarifa kutoka kwa
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) zinathibitisha utoroshaji
huo wa madini.
“Kwa taarifa kamati ilizozipata kutoka TMAA ni
kuwa kiasi cha madini kinachochimbwa nchini mwetu na kutorosha nje ya
nchi ni kingi kuliko takwimu,” alisema mwenyekiti huyo.
“Kwa mfano takribani tani 20 za dhahabu huzalishwa
kila mwaka na wachimbaji wadogo lakini takwimu rasmi za Serikali za
uzalishaji ni chini ya tani mbili kwa mwaka,” alisema.
Kamati hiyo imeshauri kwa kuanzia, eneo lote la
Migodi ya Mirerani liwekewe uzio ili eneo hilo liwekewe ulinzi kwa
kutumia watu na mitambo maalumu ili kuhakikisha kila kipande kinachotoka
kinahakikiwa na kulipa tozo na ushuru.
Wakati huohuo, Sakata kusafirishwa kwa gesi kutoka
Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam, limeibuka tena bungeni ambapo
wabunge wawili wa Mkoa wa Lindi, wamesema kutotekelezwa kwa ahadi za
muda mrefu ndiko kunakosababisha mgogoro.
Wameyasema hayo bungeni jana wakati wakichangia
taarifa za Kamati za Bunge za Miundombinu pamoja na ile ya Nishati na
Madini kuhusu utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka 2010.
Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), alisema
wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara hawana tatizo na kusafirishwa kwa
gesi kwenda Dar es Salaam. Alisema wananchi wa mikoa hiyo wanahoji juu
ya baadhi za ahadi za serikali ambazo zimetolewa kwa muda mrefu lakini
hazijatekelezwa.
“Ahadi zilizoahidiwa hazijatekelezwa, lakini mradi
huu kwa kipindi cha mwaka unaelekea kukamilika, lakini ahadi hizo
hazijafanyiwa kazi, inashangaza bomba la gesi lifike Dar es Salaam
lakini vijiji vya mikoa ya lindi havina umeme,’alisema.
Alisema jimbo lake lina umeme katika vijiji
viwili, lakini waliahidiwa kupatiwa umeme tangu mwaka 2010 mpaka leo
hakuna hata dalili ya nguzo zilizowekwa.
Aliitaka Serikali kutimiza ahadi zake kwa wananchi
wa mikoa hiyo na kuangalia upya kuhusiana na viwango vya fidia kwa watu
wanaohamishwa kwenye maeneo yao.
Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF),
alisema kuwa mambo yote yanayofanywa na serikali yanafaa kujulikana kwa
wabunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi.
Post a Comment