Mauaji ya ajabu ya mtoto JonBenet Ramsey III

WAKATI wa mahojiano yao na CNN, Patsy hakuwa mzungumzaji lakini baadaye alisema kwa kifupi kwamba anaamini muuaji wa binti yao yupo na hajakamatwa tu.

Polisi wa mji wa Boulder hawakufurahishwa na maelezo ya familia ya Ramsey wakati akizungumza na CNN, siku iliyofuata Meya wa mji huo na maofisa wa polisi waliitisha mkutano na vyombo vya habari ambapo walikanusha kauli iliyotolewa na mke wa Ramsey aliposema kwamba muuaji wa binti yao yupo na hajakamatwa. Maofisa hao walisisitiza kwamba mauaji ya JonBenet siyo endelevu, hivyo waliwataka wakazi wa mji huo kulala kwa amani bila hofu kwa sababu hakutatokea mauaji kama hayo tena.

Maofisa hao walidai kwamba wanamjua aliyemuuwa mtoto JonBenet Ramsey na bado kitambo kidogo watathibitisha madai yao.

Kwa muda mfupi polisi walihamisha hisia zao kuwatuhumu John na Patsy Ramsey na mauaji ya binti yao na kuelekeza hisia zao hizo kwa watoto wake aliowazaa katika ndoa yake ya awali, wanaoitwa Melinda na John Andrew Ramsey.

Pamoja na minong’ono iliyoenea kwamba walionekana katika mji huo wa Bouliver siku ya Krismas, lakini wote walidai kwamba walikuwa Atlanta siku hiyo ya Desemba 25 na siku iliyofuata yaani Desemba 26, waliondoka katika mji huo kuelekea katika mji wa Minneapolis ambako walipanga kukutana na baba yao pamoja na mama yao wa kambo na wanawe katika nyumba yao wanayoitumia wakati wa likizo hapo Minneapolis, hata hivyo rafiki mmoja wa familia aliwapigia simu na kuwajulisha kwamba mtoto JohnBenet ametekwa nyara na hajulikani alipo. Walipanda ndege hadi katika mji wa Denver na hapo walikodi teksi hadi Boulder.

Polisi waliyachukua maelezo yao na kutokana na kutokuwa na muunganiko na tukio hilo, walibadilisha hisia zao kutoka kwa watoto hao na kuwageukia John na Patsy Ramsey wazazi wa mtoto JonBenet.

Lakini Februari 8, mwaka 1997 kitengo cha kuzuia uhalifu cha Boulder kilitangaza kwamba familia ya Ramsey itatoa zawadi ya dola 100,000 za Marekani kwa mtu yeyote atakayejitokeza kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa muuaji na kuhukumiwa.

Rais wa kitengo cha kuzuia uhalifu cha kimataifa Larry Wieda alifafanua juu ya hatua hiyo. “Tunachofanya ni kuhakikisha hakuna taarifa zinazotupita juu ya tukio hili.” Aliendelea kusema kwamba kwa kawaida taasisi anayoiongoza huwa inatoa zawadi inayofikia dola 10,000 za Marekani, lakini akaongeza kwa kusema; “Siwezi kukumbuka kesi yoyote ambayo ilipatiwa ufumbuzi kutokana na kiasi kikubwa cha zawadi kilichoahidiwa.”

Hata hivyo kiwango hicho kilichotangazwa na familia ya Ramsey kiliamsha mwamko kutoka kwa jamii ya Wamarekani kutoa taarifa kwenye taasisi hiyo ya kuzuia uhalifu. Kwa muda mfupi taasisi hiyo ilipokea simu zaidi ya 1,500 kutoka kwa raia wema ambao walidai kwamba wana taarifa ambazo zitasaidia kupatikana kwa muuaji.  Mpaka kufikia katikati ya Februari, polisi walikuwa wamepokea barua zipatazo 1,000 na simu zapatazo 3,000. Polisi walisema kwamba kati ya hizo taarifa ni asilimia tano tu ambazo zinaonekana huenda zikazaa matunda, lakini pia waliwatahadharisha wananchi kutowapotezea muda polisi. Kauli hiyo ilitokana na baadhi ya taarifa kuonekana zisizo na mashiko. Akitolea mfano baadhi ya taarifa hizo ni pamoja na zile ambazo wapo waliodai kwamba wana uwezo wa kufanya miujiza na kumbaini muuaji.

Kuanzia hapo, olisi hawakutoa taarifa zozote kwenye vyombo vya habari kuhusiana na kesi hiyo, na upelelezi wa kesi hiyo ulionekana kufanywa kwa siri. Wakati John Meyer wa kitengo cha uchunguzi wa maiti katika wilaya ya Boulder alipomaliza uchunguzi wa mwili wa JonBenet Ramsey hapo Februari 11, mwaka 1997, alikataa kutoa taarifa kwa undani kuhusiana na matokeo ya uchunguzi wake akidai kwamba askari wa upelelezi wa mji huo wa Boulder pamoja na waendesha mashitaka wanaohusika na kesi hiyo walimuonya kwamba, iwapo atatoa matokeo ya uchunguzi wake ataathiri kwa kiasi kikubwa mwenendo wa upelelezi wao katika kumtafuta muuaji.

Msemaji wa kitengo hicho cha uchunguzi wa maiti alisema kwamba, miongoni mwa taarifa za uchunguzi wa mwili wa binti huyo ambazo polisi na ofisi ya mwanasheria wa wilaya ambazo wasingependa ziwekwe hadharani ni kuhusu majeraha mangapi yamekutwa kwenye mwili wa marehemu, idadi ya vielelezo vilivyokusanywa baada ya uchunguzi, na mbinu iliyotumiwa na muuaji kutekeleza mauaji hayo (details of the Modus operand of the killer)

Hata hivyo kuna taarifa iliyovuja kutokana na uchunguzi wa mwili wa binti huyo ni kwamba, mwili wa binti huyo ulikutwa ukiwa na michubuko ya muda mrefu katika uke ambapo ripoti hiyo ilieleza kwamba michubuko hiyo inawezekana ilitokana na binti huyo kunajisiwa mara kwa mara.

Haraka sana msemaji wa familia ya Ramsey Pat Korten alizungumzia tuhuma hizo na alimshirikisha aliyekuwa daktari wa  binti huyo ambaye alikanusha, kwamba hajawahi kuona ushahidi wowote kwa binti huyo unaoonyesha alikuwa akinyanyaswa kijinsia.

Mwezi huo wa Februari haukuwa mzuri sana kwa familia ya Ramsey, kutokana na jinsi polisi walivyokuwa wakiizungumzia kesi ya binti yao na kusababisha uhusiano wa familia ya Ramsey na polisi kutokuwa mazuri.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/mauaji-ya-ajabu-ya-mtoto-jonbenet-ramsey-iii#sthash.68KJCcDU.dpuf

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top