Mkichezea Rasimu, mtaumia’







MWENYEKITI wa Tume ya Katiba, Jaji JosephWarioba, amesema Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete imetoa fursa mpya kwa makundi ambayo hayakuangaliwa vema katika Katiba iliyopo sasa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki hii, Warioba alisema katika Katiba ya sasa iliyotengenezwa mwaka 1977 iligusa maeneo mengi lakini haikugusa na kufafanua kwa undani malengo, maono na dira za makundi maalumu nchini.

Katika mahojiano hayo ambayo yamechapwa ndani ya gazeti hili, Warioba alisema rasimu hiyo imetoa mapendekezo ambayo yatahakikisha haki za makundi haya zinakuwa ndani ya Katiba na si kwenye sheria peke yake; jambo linaloashiria ustawi kwa makundi yote.

“Chukulia kilimo kwa mfano. Tunasema ni sekta muhimu lakini wakulima hawaoni kama sera zilizopo sasa zinawasaidia. Wametoa mfano wa wafanyakazi. Kama mshahara hautoshi wanagoma. Serikali inawajali. Kama bei ya bidhaa imepanda kwenye masoko, serikali inajitahidi kuongeza mshahara kwao. Hivyo wakulima wanaona sera za kusaidia wafanyakazi zipo. Lakini wao wanaona hawatazamwi. Kwa vipi. Nitaeleza.

“Kila mwaka bei za mazao yao zinabadilika. Wanahitaji zana na pembejeo za kuboresha kilimo. Bei za mazao zinapungua kila mwaka. Lakini hakuna sera za kuwalinda kutokana na matatizo kama haya. Hawana namna ya ku- control bei.

“Wafugaji wanasema hivyo hivyo kama wakulima. Wavuvi wanasema hivyo na vijana wanasema hivyo pia. Kuna sera gani? Sisi kama taifa tuna dira gani ya kulinda maslahi yao? Ilichofanya rasimu sasa ni kuweka mambo ambayo yatahakikisha wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi yanaangaliwa kupitia misingi na malengo ambayo sisi kama taifa tumekubaliana,” alisema Warioba.

Kimsingi, alisema Jaji Warioba, kama rasimu hiyo itapitishwa katika Bunge la Katiba lililopangwa kukutana mwezi ujao, Katiba itakayopatikana itakuwa ya kwanza hapa nchini ambayo watu wa makundi yote; bila kujali dini zao, itikadi zao za kisiasa, hali zao za kiuchumi, wanakotoka na tofauti nyingine zote, wameshiriki katika kuiandaa.

Katika mahojiano hayo, Warioba ameeleza masikitiko yake kuhusu mijadala iliyopo sasa hapa nchini kujielekeza zaidi katika masuala ya kiutawala na nani anapata nini katika mgawanyo wa madaraka, badala ya kujadili masuala ambayo wananchi waliyaona ya muhimu katika taifa.

Alisema wananchi walieleza mengi kuhusu Malengo ya Taifa, Dira ya Taifa, Tunu za Taifa na masuala mengine ambayo yangejenga msingi mzuri wa taifa, lakini mijadala mingi imeangalia katika maeneo aliyoyaeleza kimsingi kuwa ni ya utekelezaji tu.

Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, alionya kwamba kama hali hii itaendelea, wananchi watakwenda kupiga Kura ya Maoni pasipo kujua kama mambo ambayo wao waliyapigania, yameingizwa katika Katiba yao.

Kwa taarifa zaidi, soma kurasa za katikati za gazeti kupata mahojiano kamili na Jaji Warioba

- See more at: http://raiamwema.co.tz/%E2%80%98mkichezea-rasimu-mtaumia%E2%80%99#sthash.eWnhv1MM.dpuf

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top