WAZIRI AHOFIA WENZAKE SERIKALINI KUPIGWA MAWE







NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kiko hatarini kwa viongozi wa serikali kuweza kutukanwa au kupigwa mawe kama Wizara ya Ujenzi haitafanya juhudi kuhakikisha barabara ya Sengerema- Buchosa inakamilika ili ipitike katika kipindi chote cha mwaka.

Akichangia katika kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza Jumanne wiki hii, Dk. Tizeba, ambaye pia ni Mbunge wa Buchosa wilayani Sengerema, alisema jimbo lake linategemea barabara hiyo tu na kama ikishindwa kupitika katika wakati huu wa masika ina maana yake jimbo hilo litakuwa limejitenga na makao makuu ya wilaya.

“Mheshimiwa Mwenyekiti hili tulizungumza hata katika kikao kilichopita, na tukawaomba TANROADs wapeleke barua Wizara ya Ujenzi na kwa Mkurugenzi wa TANROADs, lakini hawajajibu barua mpaka leo, hali ya barabara hii ni mbaya sana, CCM kinatukanwa kiko kwenye moto sana, wanatukanwa viongozi wa serikali, hali ikifika hivi mpaka Juni watu watapigwa mawe,” alisema Tizeba.

Katika kuonyesha kuwa amedhamiria kuepusha balaa hilo la kupigwa mawe na kutukanwa, aliwataka wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa, ikiwezekana baada kumaliza kikao hicho wafunge safari ambayo ataigharimia waende kwenye barabara hiyo ili wakaone jinsi ilivyo na hali mbaya.

“Inawezekana watu wa Sengerema tukaonekana tunasema sana, watu wengine humo kwa kuwa hawajaiona barabara hiyo wanaweza wasielewe hasa tunazungumza nini, ninaomba baada ya kikao hiki twende, nitagharimia safari hiyo, wajumbe wajionee hali ilivyo mbaya,” alisema Tizeba.

Naibu Waziri huyo pia aliomba kikao hicho cha Bodi ya Barabara kuunda timu ya watu watakaokwenda kumuona Waziri wa Ujenzi ili kumweleza hali hiyo kwa sababu kama wamepuuza kujibu barua waliyoandikiwa mwaka jana, haitakuwa na maana kuendelea kusubiri majibu ya barua hiyo.

“Uzoefu wangu mdogo serikalini unaonyesha kuwa kuendelea kusubiri majibu ya barua ya mwaka jana ni kupoteza muda, Mheshimiwa Mwenyekiti wa chama (Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, aliyekuwepo kikaoni hapo) Ilani yako haitekelezeki twende kumwambia waziri hali ni mbaya,” alisema Tizeba.

Katika kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Machi 21, 2013 kilimuagiza Meneja wa TANROADs Mkoa, amwandikie barua Mkurugenzi wa TANROAD ngazi ya taifa ili pamoja na mambo mengine, kumuomba makabidhiano ya mradi (Performance based Management and Maintenance of Roads) yafanyike upya.

Akijibu hoja hizo Mwenyekiti wa kikao cha bodi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikillo alikubaliana na Tizeba na kuagiza timu ya watu watatu ikimuhusisha Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa na Meneja wa TANROADs Mkoa kupanga siku ya kwenda kumuona Waziri wa Ujenzi kuhusu suala hilo.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa kikao hicho, aliagiza Meneja wa Wakala wa Ufundi wa Serikali (TEMESA) Mkoa wa Mwanza, Amon Senkoro, aandikiwe barua ya kujieleza kwa nini anapuuza maagizo ya Bodi ya Barabara na kutohudhuria vikao badala yake amekuwa akituma mwakilishi tu.

Hali hiyo ilitokana na agizo lilitolewa na Bodi hiyo katika kikao chake kilichopita kikimtaka meneja huyo kuhakikisha kuwa vivuko vyote chini ya ofisi yake, vinatoa elimu kwa abiria jinsi ya kujiokoa kwa kwa kutumia CD kama ilivyo kwenye kivuko vya Nyehunge, na mwakikishi wa meneja huyo kuwahakikishia wajumbe kuwa agizo hilo litatekelezwa.

Awali, mwakilishi wa Meneja wa TEMESA Daudi Nyoni alijaribu kutoa maelezo ambayo hayakuwaridhisha wajumbe ndipo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, aliposimama na kueleza kuwa meneja huyo amekuwa akiwakilishwa katika vikao vingi, kwa hiyo hata kuendelea kumsikiliza mwakilishi wake ni kupoteza muda.

“Huku ni kudharau uamuzi wa kikao cha Bodi ya Barabara, aandikiwe barua ya kujieleza kudharau kutekeleza maazimio ya bodi. Tuko hapa leo kwa shughuli hii muhimu yeye yuko likizo na hajatekeleza maelekezo ya bodi hata moja,” aliagiza mwenyekiti wa kikao hicho, Ndikillo
CHANZO Raia mwema

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top