Dodoma/Dar. Kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuapa mmojammoja badala ya makundi kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Kanuni za Bunge kitaligharimu Taifa zaidi ya Sh500 milioni, Bunge limeelezwa.
Hayo yalielezwa juzi usiku na Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Kessy na Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe baada ya baadhi ya wajumbe kupinga pendekezo la Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo la kuapa kwa makundi ili kuokoa muda.
Katika maelezo yake, Kessy alisema kwa idadi ya wajumbe wote wa Bunge hilo ambao ni 629, ni wazi kuwa wakiapa mmojammoja, itawachukua siku tatu kumaliza na katika muda huo posho za wajumbe zitafikia Sh500 milioni.
“Jamani lazima tuwe na huruma na mkumbuke kuwa tunalipwa kwa kodi za Watanzania. Tukiapa mmojammoja tutachukua siku tatu na kwa siku hizo tutalipwa posho ambazo zitafikia Sh500 milioni. Ni bora tukaapa kwa makundi kama ilivyopendekezwa,” alisema Kessy.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbowe ambaye alisema: “Bunge hili limepangiwa muda maalumu wa kufanya kazi na mpaka sasa tumeshatumia siku 15. Tukiapa kwa muda wa siku tatu, ni sawa na kupoteza Sh500 milioni.
“Tunaelewa umuhimu wa watu kuweka historia, kamati imetuletea ushauri mzuri, ni vyema tungeufuata, nawaombeni turidhie maoni ya kamati maana tumekuja hapa kutunga Katiba siyo kanuni. Naunga mkono kuapa kwa makundi.”
Iwapo wajumbe wote watahudhuria vikao vya Bunge kwa siku tatu za kuapa, kwa siku moja watalipwa Sh188.7 milioni na kwa siku tatu watalipwa Sh566.1 milioni. Kila mbunge analipwa Sh300, 000 kwa siku.
Awali, kamati hiyo ilipendekeza kuwa wajumbe hao waape kwa makundi matatu ili kuokoa muda, lakini kutokana na michango ya wabunge, ilipitishwa kuwa kila mmoja aape kwa wakati wake.
Mapema, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu alisema kamati yake ilipendekeza kuapa kwa makundi ili kuokoa muda na kwamba kama wajumbe wakiapa mmojammoja, shughuli hiyo itachukua siku tatu.
Akitoa ufafanuzi zaidi, mjumbe Ezekiel Oluoch alisema, “Nimewahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika kwa miaka minne. Sisi tuliapa hotelini kwa makundi, tena kwa kutumia karatasi zilizokuwa zimechapwa sala kulingana na dini ya mjumbe husika na tulikuwa wabunge kutoka nchi 53.”
Alisema kama kuna wajumbe wanaotaka kuapa mmojammoja ili familia zao ziwaone kupitia televisheni, ni bora wakasubiri kushinda ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby alipinga kiapo hicho cha mmojammoja kwa maelezo kuwa kitawaumiza wanyonge ambao ni walipa kodi kwani kitachukua muda mrefu kwa watu kulipwa fedha bila ya kufanya kazi yoyote endelea


Post a Comment