
Mbishi ni mdadisi. Ni mtu anayechokonoa watu wanaojua jambo ili wamulike kwa hoja zilizokwenda shule, kwa lugha au mifano kuntu isiyotatanisha – anajadili na anafanya ushindani.
Kwa hiyo, sibishi ila nadadisi. Kwani nani hajawahi kubisha jambo maishani mwake? Hebu fikiria, mtu anakunasihi eti “dogo achana naye,aliyejuu mngoje chini!” Yaani mimi miaka yote niwe mtu wa kusubiri tu ashuke! Kwa nini nisifanye juhudi kupambana naye huko juu?
Methali nyingine ambayo sitaki kuisikia ni isemayo “sheria ni msumeno...” Uongo mtupu, tena wa wazi kabisa. Sheria inayotumika kumfunga mlalahoi haiwezi kumfunga kigogo, mtoto wala rafiki wa mnene.
Mnataka ushahidi? Mwaka ule tulipokuwa vijana si tulishuhudia kigogo mmoja akimchukua mtoto wake kwa gari la kifahari aina ya Mercedes Benz kwenda mahabusu na kortini baada ya kushtakiwa kwa mauaji. Mbona hakuwa anapelekwa kwa karandinga la polisi? Usawa wa kisheria uko wapi?
Halafu kule Iringa, nyote mnajua kuwa yule polisi aliyetuhumiwa kumlipua kwa bomu la machozi, mwanahabari Daudi Mwangosi, habebwi kwa karandinga la polisi ila moja ya magari ya kifahari ya polisi, tena akiwa amefunikwa kwa shuka! Sasa hapo mimi nikubali eti sheria ni msumeno unaokata kote kote?
Mimi sibishi tu, hata Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana analia, anasikitika na analalama kuona sheria siyo msumeno.
Kila anakopita, Kinana analia Serikali ya chama chake cha CCM kutumia sheria kumhukumu huyu na kumwachia yule.
Sasa mtu mzima kama Kinana analia, sembuse mlalahoi mitaani?
Iko hivi, Mamlaka ya Utumishi wa Umma ilitumia sheria kumsimamisha kazi katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kupisha uchunguzi wa namna alivyohusika katika sakata la uchotwaji fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Na ili kuonyesha nia njema, Kamati Kuu ya CCM iliwasimamisha makada watatu; Profesa Anna Tibaijuka, Andrew Chenge na William Ngeleja kuhudhuria vikao vyote muhimu vya chama.
Pia, Profesa Tibaijuka alivuliwa nafasi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Chenge alivuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, na Ngeleja alifutwa uenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Bunge.
Hayo yamefanyika, lakini Kinana anashangaa kwa nini mamlaka iliyomsimamisha Maswi imekaa kimya kwa Shaaban Gurumo ambaye anafanya kazi Ikulu? read more.......


Post a Comment