
SIKU zote tumezoea kuona baadhi ya wanasiasa na viongozi wakiwa
mstari wa mbele kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na hata kupinga
ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Hali hiyo imekuwa ni tofauti kwa Kigogo mmoja wa Chama Tawala CCM
wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambaye mbali na kumtumikisha mtoto
aliyechini ya miaka 18 bali pia amemfanyia unyama na ukatili
uliopitiliza kwa kummwagia maji ya moto kwa kile kinachodaiwa kuwa mtoto
huyo anakula sana.
Kigogo huyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Mahango kijiji
cha Mageya kata ya Rujewa wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la
Ziada Bakari Mwihesi anadaiwa kummwagia maji ya moto mtoto Agustino
Sanga(12) ambaye alikuwa akimtumikisha kwa kufanya kazi za kuchunga
mifugo yake kuanzia alfajiri hadi usiku bila kumpatia chakula cha
uhakika.
Mtoto Agustino ambaye ni yatima anayelelewa na bibi yake baada ya
kufiwa na wazazi wake huko wilayani Makete mkoani Njombe alianza kuishi
na Mwenyekiti huyo wa chama mwaka 2011 akitokea wilayani Makete mkoani
Njombe ambapo Bibi yake kutokana na kutokuwa na uwezo alimkabidhi mama
huyo ili aishi naye huku akimsaidia kazi za kuchunga mifugo yake.
Akizungumza mkasa huo mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyefika
kijijini hapo kufuatilia taarifa za unyanyasaji dhidi yake, mtoto huyo
alisema kuwa aliletwa nyumbani kwa mama huyo mwaka 2011 na Bibi yake
akitokea Wilayani Makete Mkoani Njombe ili aweze kufanya kazi ya
kuchunga ng’ombe kwa mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa tukio la kuunguzwa moto lilimtokea mwezi Juni 2013
shambani kwa Mwenyekiti huyo eneo la Jangulutu majira ya usiku ambapo
Mwenyekiti huyo alianza kumsimanga kwa madai kuwa amekuwa akila chakula
kupita kiasi na kusababisha watoto wake kutoshiba.
Mtoto Agustino aliendelea kusema kuwa, mama huyo aliendelea
kumsimanga na ghafla alichukua maji yaliyoinjikwa jikoni yakiwa
yamechemka kwa ajili ya kupika ubwabwa usiku huo na kummwagia kifuani
na baadaye kumfungia ndani huku akilia kwa uchungu.
“Nilipata uchungu mkubwa, nililia sana sikuwa na msaada wowote usiku ule mama Yule alinifungia ndani, sikupata matibabu yoyote,’’aliongea kwa uchungu mtoto Agustino.
Agustino aliendelea kufafanua mkasa huo kwa kusema kuwa akiwa
amefungiwa ndani mama huyo alikuwa akisaga mifupa ya ng’ombe na kumpaka
katika jeraha la kidonda alichounguzwa na kwamba kila alipokuwa
akimpaka ndipo kidonda kilipozidi kutoa usaha.
Alisema akiwa ndani Bibi yake alianza kumtafuta ndipo siku hiyo
alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumuuliza alipo ambapo
alimweleza kuwa mjukuu wake aliungua moto alipokuwa akicheza karibu na
moto.
Agustino aliendelea kubainisha kuwa tangu alipofika nyumbani kwa
Mwenyekiti huyo mwaka 2011 hajawahi kupumzika na kwamba amekuwa
akitumikishwa kama Punda kuanzia alfajiri hadi usiku huku akipewa
chakula kidogo.
Kwa upande wake Babu wa Mtoto huyo Method Ndelwa(55) Mkazi wa
Kitongoji cha Mahango alisema mtoto huyo baada ya kufika nyumbani hapo
alikuja mume wa Mwenyekiti aitwaye Seleleka Twasanga na kumuomba mtoto
huyo awe anamchungia ng’ombe na mbuzi shambani kwake.
Alisema tangu mjukuu wake alipoungua mwaka 2013 mwezi wa 6 hakuna
msaada wowote ambao unatolewa na familia ya Mwenyekiti na kwamba
ameendelea kuugulia na majereha yake bila kupatiwa matibabu ya uhakika.
“Mimi na Bibi wa wa mtoto huyu hatuna hali zetu ni duni kipato chetu ni kidogo kama mnavyoona kidonda cha mtoto kinatoa usaha na hapo mwanzo kilikuwa kinatoa funza, mama mmoja Rukia Shomari alitusaidia kumnunulia dawa,’’alisema Babu wa mtoto huyo.
Alisema kuwa hakuwa anajua utaratibu wowote wa kutoa taarifa hizo
kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na kwamba tangu alipounguzwa
moto walikuwa wakimuangalia tu mtoto huyo huku wakishindwa kujua hatima
yake.
“Tunaomba mtusaidie kulifikisha hili ili jamii ijue kama mna uwezo wa kumsaidia mtoto huyu tunaomba msaada wenu kumuokoa mtoto huyu’’,alisema Mzee Ndelwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahango ambaye ndiye
anayedaiwa kufanya unyama huo,Ziada Mwihesi alikana kumchoma moto mtoto
huyo na kudai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na mume wake
aliyemtambulisha kwa jina la Seleleka kuwa mtoto Agustino ameungua moto
ndipo alipoondoka na kwenda shambani na kumkuta mtoto huyo akiwa
ameungua kifuani.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo anadai kuwa chanzo cha mtoto huyo
kuungua ni kutokana na kuota moto asubuhi wakati akipasha kiporo cha
wali katika jiko la kuni na kusema kuwa mtoto huyo alishaungua moto
akiwa kwa bibi yake na kudai kuwa hapo amekuja kuungua kwa mara ya
pili.
Pamoja na kufanya unyama huo Mwenyekiti huyo alionekana kutohitaji
kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi kwa kutoa majibu ya mkato
wakati alipokuwa akiendelea kuulizwa maswali juu ya kuchomwa moto kwa
mtoto huyo ambapo pia alikanusha kummwagia maji ya moto mtoto huyo kwa
madai ya kumaliza chakula.
Naye Mume wa Mama huyo Seleleka Twasanga alikiri kuungua kwa mtoto
huyo na kudai kuwa yeye alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na jirani
yake ambaye wapo jirani shambani kwamba Mtoto Agustino ameungua moto
ndipo alipoondoka na kwenda shambani ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Bw.Twasanga alisema wakati anamchukua mtoto huyo kwa Bibi yake
walifanya kama kubadilishana na Bibi huyo ambaye alihitaji kila mwaka
alimiwe shamba la heka mbili kwa ng’ombe wakati mtoto Agustino akifanya
kazi ya kulima na kuchunga Ng’ombe na mbuzi shambani kwa Twasanga.
Akielezea zaidi mume wa mama huyo alisema aliendelea kumlimia shamba
bibi wa mtoto Agustino na kukiri kutomlipa chochote zaidi ya bibi huyo
kulimiwa shamba.
Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa katika harakati
za kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji wa wanawake na
Watoto.
Mkurugenzi wa TAMWA Valerie Msokwa kupitia jarida lake linalotolewa
na taasisi hiyo alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria ya
Kimataifa ya haki ya mtoto ya mwaka 2009 iliyowekwa katika tamko la
Umoja wa Mataifa la Haki za Mtoto linalotoa mwongozo wa kulinda na
kutambua haki za mtoto nchini.
Alisema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wanapaswa
kulindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa
watoto katika maeneo mengi ya mijini na vijijini.
Naye Diwani wa Kata y Rujewa Bi.Gurzar Sabil alipotakiwa kuzungumzia
tukio hilo la kinyama la mwenyekiti huyo alisema kuwa hana taarifa hiyo
lakini aliahidi kuwasiliana na Ofisa Ustawi wa jamii wilaya ya Mbarali
ili waweze kwenda nyumbani kwa mtoto waweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na
kumkamata mtuhumiwa.
Mara baada ya Mwandishi wa habari hizii kuondoka wilayani humo Ofisa
Ustawi wa Jamii wilaya ya Mbarali Winifrida Mahali akiambatana na
Mratibu wa Dawati la Jinsia wilayani humo Christa Komba walifika
nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumchukua hadi kituo cha Polisi.
Bi Mahali alisema kuwa walimfuata mtuhumiwa pamoja na mumewe na
kuwapeleka kituo cha polisi ambako walilala hadi asubuhi na kufikishwa
katika mahakama ya wilaya ya Mbarali ambako wamesomewa mashtaka ya
kujeruhi na wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi Januari 29


Post a Comment