Morogoro. Mafuriko makubwa yametokea katika Kata ya Dumila, Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha mamia ya watu kupoteza makazi huku daraja la Mto Mkundi linaloziunganisha Wilaya za Kilosa na Mvomero likivunjika.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa
zilizoanza kunyesha jana alfajiri na kusababisha maafa makubwa yakiwamo
kuharibiwa kwa makazi ya watu, majengo ya Serikali zikiwamo shule, vyuo
na mahakama.
Habari zinasema mafuriko hayo pia yalichangiwa na
mvua kubwa iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana katika sehemu za
milima iliyopo Kilosa na Mvomero, hivyo Mto Mkundi kushindwa kuhimili
maji hayo.
Mashuhuda walisema waliona maiti ya mtu ikielea
kwenye maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi, tukio ambalo lilithibitishwa
na Diwani wa Kata ya Magole, Juma Rajabu Chewe. Chewe alisema maiti hiyo
ilionekana ikielea eneo la Mateteni na kwamba taarifa zilitolewa polisi
ili aopolewe. Hadi jana jioni idadi ya watu walioathiriwa na maafa
ilikuwa bado haijafahamika.
Maji yasambaa kwenye vijiji mbalimbali
vinavyozunguka mto huo na kuwalazimisha baadhi ya watu kulazimika
kujiokoa kwa kupanda kwenye paa za nyumba zao huku wengine wakikwea juu
ya miti.
Baadhi ya watu walikutwa na mafuriko hayo
mashambani na walipozidiwa na nguvu ya maji walijiokoa kwa kushikilia
vitu mbalimbali ikiwamo miti, huku baadhi yao wakipoteza nguo walizokuwa
wamevaa walipokuwa kwenye harakati za kujiokoa.
Polisi waliofika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji
walilazimika kuomba helikopta kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar es
Salaam ili kuwaokoa watu waliokuwa kwenye paa za nyumba na kwenye miti
iliyokuwa imezungukwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitaka
kuwapo kwa uvumilivu wakati Serikali ikiendelea na taratibu za kuwaokoa
walioko juu ya miti na kutoa misaada kwa walioathirika.
Alisema kuwa kutokana na hali kuwa mbaya, ofisi
yake ililazimika kuomba helikopta kwa ajili ya kuongeza nguvu ya juhudi
za uokoaji.
Taharuki kubwa
Mafuriko hayo yalizua taharuki kubwa kiasi cha
wananchi kutawanyika ovyo wakiwa hawajui cha kufanya, kutokana na nyumba
zao kuharibiwa na mali zao hususan mazao yakisombwa na maji.


Post a Comment