WAKATI Bunge la Katiba likitarajiwa kupitisha kanuni zake keshokutwa (Ijumaa), baadhi ya mapendekezo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu msimamo wake (Rasimu Mbadala ya Katiba) yameanza kuvuja.
Kati ya mapendekezo hayo ni kusudio la kurejesha mfumo wa zamani wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na hilo, chama hicho pia kimependekeza kuwapo kwa vyombo vitatu vya uwakilishi (Bunge) kwa kutumia majina yatakayoamuliwa, ikishauriwa Bunge la Jamhuri ya Muungano liitwe Seneti, huku tafsiri ikijitokeza kwamba, CCM inapinga pendekezo la mawaziri kutokuwa wabunge.
Kuhusu vyombo hivyo vya uwakilishi, chama hicho kinapendekeza kuwapo kwa Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, lakini pia kuwapo kwa chombo cha uwakilishi cha jumla, kinachounganisha wawakilishi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Mapendekezo hayo yaliyopata kuwasilishwa katika Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho iliyokutana wiki kadhaa zilizopita mjini Dodoma, yanatoa ruksa pia kwa Zanzibar kukopa katika jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, Zanzibar itaruhusiwa kukopa kwa masharti kwamba ni lazima kufanya mawasiliano na maelewano kati yake na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pamoja na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari katika suala la chombo cha uwakilishi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Bunge/Seneti) masharti yawekwe kwamba, kama Spika wa Bunge hilo atatoka Tanzania Bara, basi, Naibu Spika atoke Zanzibar.
Taarifa kuhusu mapendekezo hayo ya CCM zinaeleza kwamba ‘wabunge’ wa Zanzibar hawatahusika katika mijadala masuala ya Tanzania Bara, kama ambavyo wenzao wa Bara watakavyokuwa hawahusiki na mjadala kuhusu Zanzibar, isipokuwa tu wote wanaweza kuhusishwa kimjadala kama mjadala husika utahusu masuala ya Muungano.
“Msimamo ni kwamba nafasi ya Rais wa Zanzibar kwenye Muungano, irejeshwe kama ilivyokuwa awali, awe Makamu wa kwanza wa Rais; kuhusu akaunti ya fedha ya pamoja, chama kinataka ifunguliwe akaunti hiyo mara moja itakayoweka fedha zote zinatokana na mapato ya vyanzo vya Muungano,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, CCM kinataka kuwapo kwa sheria mahsusi kuhusu utaratibu wa mambo ya Muungano, pia kuwapo na Tume ya Usimamizi na Uratibu wa mambo ya Muungano ya yanayotokana na Katiba.
“Kuhusu suala la uhusiano wa kimataifa na mashirika au asasi za nje; inapendekezwa Zanzibar iweze kuwa na uhusiano wa kimataifa katika masuala yasiyo ya Muungano kwa kuihusisha Wizara ya Mambo ya Nje,” inaeleza taarifa hiyo na kuongeza; “Katika Bunge, inapendekezwa kuwapo kwa Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Bara tu.
“Katika mapendekezo haya ya Bunge, majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Bara inashauriwa yaundwe upya ili majimbo ya uchaguzi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar yawe ndio hayo hayo majimbo ya uchaguzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
“Endapo muundo huu utakubaliwa basi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio wabunge wa Muungano wakati wa kujadili mambo ya Muungano.
“Bunge la Muungano wakati likijadili mambo ya Tanzania Bara, basi wabunge kutoka Zanzibar wasiwe sehemu ya mijadala hiyo na kama Spika anatoka upande mmoja wa Muungano, basi Naibu Spika atoke upande wa pili na wakati wa mjadala wa mambo ya Bara, huyo Spika ama Naibu wa Bara ndio asimamie mjadala huo.
“Kuhusu mawaziri katika Muungano ni kwamba wabunge wa Bunge la Muungano wanaweza kuwa mawaziri wa wizara za mambo ya Muungano tu, wizara zisizo za Muungano ziongozwe na wabunge wanaotoka Tanzania Bara.
“Pamoja na orodha ya mambo ya Muungano ambayo yamekuwa kwenye Katiba, mambo yasiyo ya Muungano yaorodheshwe kwenye sheria itakayoainisha pia usimamizi, utekelezaji wake na gharama zake,” taarifa hiyo inaeleza.
Katika hatua nyingine, jana Jumanne, wakati tukienda mitamboni taarifa zilizotufikia zilikuwa zilieleza kwamba Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuweza kuwania uenyekiti wa Bunge la Katiba, unaotarajiwa kufanyika baada ya Bunge la Katiba kupitisha kanuni zake Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mshindani wake aliyekuwa akitajwa kuweza kuchuana naye, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, mwanasheria mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alitajwa na watu wake wa karibu kuweza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Lakini inaaminika kwamba kundi la Chenge ambalo ndilo kundi la Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, limekuwa likijipanga kupachika mgombea mwingine dhidi ya Sitta, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe akitajwa katika nafasi hiyo.
Mbali na Chikawe, zimekuwapo taarifa kwamba Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro naye anaweza kuwania nafasi hiyo huku majina yaliyokuwa yakitajwa awali, kama Paul Kimiti yakifuata taratibu kwa kadiri uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba unavyokaribia.
Wakati hayo yakiendelea, huku sakata la nyongeza ya posho likisubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete, taarifa zaidi zinaeleza kuhusu kufanyika kwa marekebisho ya malipo kwa wajumbe wa Bunge la Katiba, lakini bila kuathiri jumla ya fedha walizokuwa wakilipwa awali, shilingi 300,000 kwa siku za kazi.
Kwa sasa badala ya kulipwa shilingi 80,000 ndani ya shilingi 300,000 walizokuwa wakilipwa awali, kiwango hicho cha fedha kimepunguzwa hadi kuwa shilingi 70,000, lakini shilingi 10,000 iliyochomolewa katika 80,000 imeingia katika malipo mengine, yaani kazi maalumu.
Katika hatua nyingine, imebainika kwamba aliyeidhinisha nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Zanzibar ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, akisaidiana na ofisi ya Baraza la Wawakilishi visiwani humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ilimbidi ahangaike kupata ukweli juu ya taarifa kwamba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Zanzibar wamekuwa wakiongezewa shilingi 120,000 katika posho ya 300,000 kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na jumla wamekuwa wakilipwa shilingi 420,000 tofauti na wenzao wengine wanaolipwa Sh. 300,000 kwa siku za kazi.
Katika kufuatilia suala hilo, Jumapili iliyopita, Waziri Mkuu Pinda alikutana na Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ambaye ndiye Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kumuuliza ukweli wa jambo hilo.
Taarifa zinaeleza kwamba, Kificho alimweleza Pinda wanacholipwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Zanzibar ni malipo ya stahili zao ambazo walikuwa wakidai awali.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, wawakilishi hao wamekuwa wakilipwa nyongeza hiyo ya fedha kutokana na kile kinachoelezwa kwamba ni viwango ya fedha wanazopaswa kulipwa kila wanapokuwa nje ya Zanzibar kikazi.
Msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu kufuatilia mazingira hayo ni malalamiko ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kwamba, wenzao kutoka Zanzibar wamekuwa wakilipwa fedha nyingi zaidi, kwa tofauti ya shilingi 120,000. Rasimu ya ccm


Post a Comment