SITTA AONYWA. soma kwa habari kamili


Samuel Sitta

MAPENDEKEZO ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao pia ni wajumbe wa Bunge la Katiba kwamba, Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta agombee uenyekiti wa Bunge la Katiba yamezua mjadala miongoni mwa wajumbe wengine wa chombo hicho, wengi wakiunga mkono na mjumbe Hashimu Rungwe, akimwonya Sitta kutoendeleza kile alichokiita laana ya CCM.

Rungwe aliyeingia katika Bunge la Katiba kupitia kundi la wateule wa Rais Jakaya Kikwete, ametilia wasiwasi pendekezo la Sitta kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu; “..ana laana ya CCM ya kusahau makundi mengine ya kijamii nchini na kung’ang’ania upande wao tu.”

Hata hivyo, wasiwasi huo wa Rungwe ambaye hajaweka bayana kama atagombea nafasi hiyo ama la mara baada ya kanuni za Bunge hilo kupitishwa, unapingwa na wajumbe wengine waliozungumza na gazeti hili, wakiamini Sitta ni chaguo lao sahihi wakati wa kupiga kura utapowadia kwa kuwa rekodi yake katika usimamizi wa mijadala ya Bunge linalohusisha makundi pinzani inajulikana.

Wajumbe hao wameeleza kuhusu matumaini au wasiwasi juu ya kupendekezwa kwa Sitta, ikiwa ni siku kadhaa sasa zimepita huku majina makubwa yakitajwa kuweza kugombea uenyekiti wa Bunge la Katiba, mara baada ya kanuni za Bunge hilo kupitishwa rasmi.

Mbali na Sitta, majina mengine yaliyokuwa yakitajwa ni pamoja na Asha-Rose Migiro, Mathias Chikawe, Paul Kimiti na Andrew Chenge, wote wakiwa wanachama wa CCM na wabunge wa chama hicho, isipokuwa Kimiti pekee anayetokana na kundi la wateule wa Rais Kikwete.

Akizungumza na Raia Mwema mjini Dodoma Jumanne wiki hii, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, alisema anaamini historia inampa Sitta nafasi nzuri ya kuliongoza kidemokrasia Bunge hilo.

“Ukikumbuka jinsi alivyoliendesha Bunge la Tisa, huwezi kuwa na shaka na uwezo wa Sitta katika Bunge hili gumu,” alisema Azzan ambaye maoni yake yanafanana na wajumbe wengine ukiondoa hao wa CCm waliompitisha kwa kauli moja katika kikao chao cha faragha, Jumapili iliyopita mjini Dodoma.

Hata hivyo, kwa upande wake Mjumbe wa Bunge Maalumu, Ezekiel Oluoch, alisema kuwapo kwa kanuni imara za kuongoza Bunge Maalumu la Katiba kutampa yeyote atakayechaguliwa kuwa Mwenyekiti uwezo wa kuendesha vyema vikao vya Bunge hilo na wala si historia yake.

“Ni kanuni ndizo zitakazomfanya atakayekuwa Mwenyekiti kufanya kazi yake vyema. Lazima atakayekuwa pale mbele azingatie kanuni, ndio maana tunapambana kuhakikisha kanuni bora zinapita.

“Watu wanapaswa kufahamu kuwa hili si Bunge la kawaida. Si la kisiasa hili wala halihitaji mtu mwenye mawazo au malengo ya kisiasa. Msingi wa Bunge hili ni maridhiano kuliko idadi ya wajumbe wanaounga mkono hoja fulani,” alisema Mjumbe huyo ambaye ni kiongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Oluoch vile vile alionesha shaka kwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akisema katika muda huu anapoliongoza Bunge hilo, ameonesha kuegemea zaidi upande wa siasa na wanasiasa wenzake.

Alisema Kificho amekuwa akiwapa nafasi kubwa zaidi watu anaowafahamu akiwaacha wajumbe wasiojulikana, lakini wenye hoja nzito, bila nafasi ya kuzitoa.

Akimzungumzia Sitta, naye Hashimu Rungwe alisema Sitta kwa sasa anaonekana kuegemea chama chake na yupo kwa maslahi yake.

“Mtu hubadilika. Sitta wa Bunge la Tisa hawezi kuwa Sitta wa Bunge Maalumu la Katiba. Huyu ana laana ya CCM ya kusahau makundi mengine ya kijamii nchini na kung’ang’ania upande wao tu.

“Tunahitaji Mwenyekiti asiye na upande kwani kwa sasa hata huyu wa muda (Kificho), ana upande anausimamia. Utakuta hoja imemalizika vizuri, lakini anaipindua na kuzua upya mjadala,” alisema Rungwe.

Ingawa hakusema kama atagombea nafasi hiyo, Rungwe alisema anaamini baada ya kanuni kupitishwa, nafasi itatolewa kwa wanaotaka kugombea nafasi hiyo kuchukua fomu, na hapo ndipo watajulikana watakaopambana na Sitta kutoka makundi mengine.

Katika hatua nyingine, jana Jumanne, hali ndani ya ukumbi wa Bunge Maalumu mjini iligeuka ghafla pale wajumbe wote wanawake walipoungana kudai kwa sauti kubwa kubadilishwa kwa kanuni inayoelekeza jinsi ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Kwa mujibu wa rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu, kifungu cha nane, viongozi hao wa Bunge Maalumu watachaguliwa kwa mujibu wa kifungu cha 23(4) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka jana.

Kifungu hicho kinasema kuwa iwapo Mwenyekiti atatoka upande fulani wa Muungano, basi Makamu wake atapaswa kutoka upande wa pili wa Muungano.

Akichangia kifungu cha nane cha kanuni hizo za Bunge, mjumbe wa Bunge hilo Dk. Ave-Maria Semakafu aliomba kifanyiwe mabadiliko na kiweke usawa wa jinsi; yaani endapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano, basi Makamu atoke upande mwingine.

Pamoja na ufafanuzi wa kisheria kutoka kwa wajumbe wanawake wa kamati ya kanuni, kwamba ni kinyume cha sheria kuweka masharti mawili tofauti ya kufuatwa katika sheria moja; la kwanza Mwenyekiti na Makamu watoke pande mbili tofauti za Muungano na kisha, kuwa lazima wawe wa jinsi tofauti, wajumbe wanawake hawakukubali.

Baadaye, George Simbachawene aliwaomba wanawake wajitokeze kugombea nafasi hizo, akisema kuirekebisha kanuni hiyo kutamaanisha kuwa kuna upande utalazimika kuchagua kiongozi ama mwanaume au mwanamke kwa kuwa tu kanuni imelazimisha.

Hapo ndipo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro alipofafanua kwamba, pamoja na sheria kuweka sharti la Bara na Visiwani katika suala hilo, si kosa Bunge kuingiza kikanuni suala la jinsi eneo hilo.

Kauli yake hiyo iliwanyanyua wajumbe wanawake ukumbini humo walioanza kuimba: “Tunataka, haki zetu!” huku wajumbe wanaume nao wakidai haki zao kwa wimbo huo huo.

Alipopewa nafasi ya kujibu hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, alikosoa tafsiri ya sheria aliyoitoa Dk. Migiro, akisema si sahihi.

“Dk. Migiro ni mwalimu wangu Chuo Kikuu, ninamheshimu sana. Lakini tukifuata tafsiri aliyoitoa hapa, tutakuwa tunaihalifu sheria. Bunge hili halina mamlaka ya kubadili sheria ambazo halijazitunga, ni makosa kwa kanuni kurekebisha sheria.

“Tunachoweza kukifanya hapa ni kufikia makubaliano tu kama alivyopendekeza mama Anna Abdallah, na kukubaliana ku-accommodate gender parity. Vinginevyo Bunge hili litakuwa limeanza kwa kituko (kanuni kukiuka sheria),” alisema Masoud, akikosoa tafsiri ya mwalimu wake.

Awali, katika kikao hicho, hoja ya Mjumbe Christopher Ole Sendeka kupinga kuingizwa kwenye kanuni haki za wajumbe kupewa nyaraka za serikali, ili kwama baada ya ufafanuzi kutoka kwa Masoud, ambaye aliongoza vyema majibu kutoka Kamati ya Kanun iiliyo chini ya Profesa Costa Mahalu.

Ole Sendeka alikuwa akitaka kukataliwa kwa ombi la John Mnyika la kurekebishwa kwa Sehemu ya Pili ya Kanuni hizo kuhusu Haki na Kinga ya Bunge Maalumu.

Mnyika alipendekeza kuongezwa kwa kipengele kitakachompa mjumbe haki ya kupewa nyaraka za serikali kuzifanyia kazi kwa mujibu wa sheria.

Kilichoonekana kumkera au kumtisha Ole Sendeka ni uwezekano wa mjumbe wa Bunge hilo kuomba kupewa na hata kuleta bungeni Hati ya Muungano.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright WORLD OF TODAY Published.. Blogger Templates
Back To Top