UTATA umeibuka kuhusu uamuzi wa Halmahauri ya Mji wa Korogwe kununua gari la kifahari kwa shilingi 142,510,000, kwa matumizi ya mkurugenzi wake na kupuuza agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda la kupiga marufuku ununuzi wa magari ya kifahari (mashangingi).
Pinda alitoa agizo hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2010, kwa kutoa maelekezo kwa serikali kuu na taasisi zake pamoja na serikali za mitaa, kutoagiza tena magari ya kifahari bila kupata kibali maalumu kutoka ofisini kwake.
Waziri Mkuu alirudia tena kusisitiza usitishwaji wa serikali kununua magari ya kifahari mwaka 2012, wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Kwa mujibu wa Pinda, lengo la uamuzi huo wa serikali wa kupiga marufuku magari ya kifahari serikalini ni kupunguza matumizi yasiyo na tija ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiigharimu serikali.
Magari hayo katika Halmashauri ya Korogwe ni Landcruiser Prado TX-L Turbo 2982cc iliyonunuliwa kwa gharama ya Sh 142,510,293 na Toyota Hilux Double Cabin Turbo iliyonunuliwa shilingi 61,775,800. magari hayo yalinunuliwa mwanzoni mwa mwaka huu kutoka kampuni ya Toyota Tanzania.
Awali, katika barua yake kwa Baraza la Madiwani wa Mji wa Korogwe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Lewis Kalinnjuna, Novemba 22 mwaka 2013 aliwasilisha ombi la kununua gari la idara ya mipango miji.
Hata hivyo, katika maombi hayo kwa Baraza, Mkurugenzi huyo hakuainisha maombi ya kununua gari la mkurugenzi katika kichwa cha habari lakini akajumuisha gharama katika maelezo ya barua, kupitia ‘mgongo’ wa gari la idara ya mipango mji.
Barua hiyo yenye kichwa cha habari: “MAOMBI YA KUENDELEA NA MCHAKATO WA KUNUNUA GARI LA IDARA YA MIPANGO MIJI” inasomeka kwamba katika vikao vya nyuma, waliwasilisha ombi la kuahirishwa kwa kipaumbele cha ununuzi wa gari la ofisi ya mipango miji na badala yake waanze ujenzi wa ofisi ya idara hiyo.
Kwa mujibu wa barua hiyo, bajeti iliyotengwa kwa ununuzi wa magari hayo ilikuwa shilingi 310,000,000 ambapo gari la mkurugenzi lilitengewa shilingi 180,000,000 na la idara ya mipango miji ni Sh. 130,000,000.
Magari hayo yaliwasili mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya Halmashauri ya Mji kukamilisha mchakato wa kuilipa kampuni ya Toyota Tanzania, kiasi cha fedha walichokubaliana.
Hata hivyo baada ya ununuzi huo yamezuka malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali katika halmashauri hiyo, huku Mkurugenzi Kalinnjuna na Mwenyekiti wa Halmashauri hiy, Angelo Bendera wakituhumiwa kukiuka taratibu za ununuzi na kupuuza maagizo ya Waziri Mkuu.
Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya halmashauri hiyo amedokeza kuwa katika uamuzi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi wake huyo hawakuzingatia waraka wa Waziri Mkuu unaoelekeza pamoja na mambo mengine, idara za serikali kuomba kibali maalumu pindi wanapohitaji kununua magari ya kifahari.
Katika waraka wake, Pinda alidokeza kuwa ni marufuku kwa idara za serikali pamoja na serikali za mitaa kununua magari ya kifahari ambayo yanatumia gharama kubwa katika kuyafanyia matengenezo ya mara kwa mara na kuyahudumia.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya halmashuri hiyo zinadai kuwa mkurugenzi huyo akitumia kile kinachotajwa kuwa ‘udhaifu’ wa Mwenyekiti wa Halmashauri Angelo Bendera na kamati yake ya fedha, alishawishi ununuzi wa magari badala ya ujenzi wa ofisi za idara ya mipango miji kama ilivyokubaliwa awali.
Inaelezwa kuwa fedha zilizotumika katika ununuzi huo ni za mauzo ya viwanja 1,500 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3.3 zilitarajiwa kupatika mwaka 2013.
Aidha ununuzi huo ulifanyika bila kuomba kibali kutoka kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kama waraka wa Pinda ulivyoagiza na pia kushirikisha mamlaka nyingine kama ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS).
Dosari nyingine ya ununuzi huo ni pamoja na kukiuka sheria ya manunuzi ambayo inaelekeza kuwa katika manunuzi yanayozidi shilingi milioni 80 ni lazima utaratibu wa zabuni ya siku 30 utumike, ili kutoa nafasi ya kushindanisha kampuni zingine.
“Kwa mfano kama mnunuzi amechagua aina ya gari maalumu kutoka kampuni moja kama ilivyofanyika katika sakata hili, basi alipaswa kuwasilisha maombi yake katika vikao vya ndani kujadiliwa ili ruhusa ya kimaandishi ipatikane,” alieleza mtoa habari wetu.
Katika barua yake ya maombi ya kununua magari hayo, Mkurugenzi Kalinnjuna hakufafanua ni sababu zipi zilizomsukuma kununua magari kutoka Toyota Tanzania.
Taarifa zaidi zinadai kuwa Mkurugenzi na Mwenyekiti wake wa Halmashauri hawakufuata taratibu za ununuzi hatua kiasi cha kuzua maswali mengi sambamba na uwezekano wa kuwepo kwa ufisadi katika ununuzi huo.
Akizungumza na Raia Mwema, mmoja wa viongozi muungano wa wafanyabiashara katika Soko Kuu la Wilaya Korogwe alisema ununuzi wa magari hayo ni kielelezo kuwa halmashauri hiyo imejaa watendaji wasiojali maslahi ya wananchi.
“Ununuzi wa gari la mkurugenzi umekuwa gumzo kwa wananchi wa Korogwe, tuna shida kwa mfano ya trekta kuzoa uchafu katika mji wetu na kuziba kwa mifereji ya maji wakati wa mvua na hakuna kiongozi anayejishughulisha kuwasadia wananchi,” alisema kiongozi huyo.
Naye Katibu wa Chama Cha Waalimu (CWT) Wilaya ya Korogwe, Festus Mitimingi, aliliambia Raia Mwema kuwa uamuzi huo “unaumiza” na ni mzigo kwa wananchi wa Korogwe.
“Inashagaza sana kutumia shilingi milioni 142 kwa ununuzi wa gari kwa ajili ya mtu mmoja tu, wakati halmashauri inakabiliwa na changamoto nyingi sana katika sekta ya afya, elimu na maji,” alieleza.
Alidai kuwa kati ya mwaka 2012 na 2013, halmashauri hiyo ilishindwa kuwapandisha daraja walimu zaidi ya 33 ambao haki zao zimepotea kwa sababu ya uzembe wa watendaji wake.
“Bado pia walimu wanadai fedha za malimbikizo kama uhamisho, safari na mengineyo na hawajalipwa lakini fedha za wananchi zinatumika kumtafutia usafiri mtumishi moja tu, jambo hili halikubaliki hata kidogo”
“Hili gari ni la kifahari mno kwa mkurugenzi kutembelea, wakati kuna magari ya gharama ya chini ambayo pia ni rahisi kuyahudumia na wakurugenzi wengi wa Halmashauri nchini wanayatumia,” alisema Mitimingi.
Alisema uamuzi huo umefanyika bila kuzingatia maslahi ya wananchi wa Korogwe pamoja na hali ya kijiografia ya mji huo ambao una kilomita za mraba 212 tu, eneo ambalo mtumishi anaweza akalihudumia hata kwa pikipiki au bajaji au gari nyingine ndogo ya bei nafuu zaidi.
Akizungumza na Raia Mwema kuhusu madai hayo Mkurugenzi anayetuhumiwa, Lewis Kalinnjuna alishangazwa na hatua ya gazeti hili kufuatilia ununuzi wa magari hayo.
“Kwanza umepata wapi hizi taarifa?” alihoji na kuendelea kusema “….kwa taarifa yako siwajibiki kwa chombo chochote cha habari pamoja na gazeti lako.”
Mkurugenzi akaendelea kusema; " Mwandishi lazima ujue halmashauri ni mamlaka kamili na haiwajibiki kwa mkuu wa wilaya wala mkuu wa mkoa. Sisi tukishapitisha mambo yetu kwenye baraza la madiwani hata Waziri Mkuu haruhusiwi kutuingilia.”
“Sisi tumenunua gari kwa kuuza viwanja vyetu na wala hatulazimiki kuomba kibali cha kununua gari letu kwa mtu yeyote and don’t west my time (usinipotezee muda)," alisema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halimashauri hiyo Anjelo Bendera alisema walipitisha uamuzi huo katika kamati ya fedha na vikao vya madiwani na hicho ndicho kipaumbele cha wananchi wa Korogwe mjini.
Alisema suala hilo linashikiwa bango na Mkuu wa Mkoa wa Tanga (Chiku Gallawa) ambaye kwa sababu anazojua mwenyewe, amekuwa akiingilia uamuzi wa halmashauri yake.
“Sasa yeye mkurugenzi pamoja na uzoefu wote kama ameacha kuomba kibali kwenye mamlaka husika hiyo siyo kazi yangu. Lakini nikuulize wewe mwandishi kiherehere chote hiki cha nini? Wananchi wetu wa Korogwe na Mbunge wa Korogwe mjini tumeridhia ununuzi wa magari haya,” alisema.
Akizungumza na Raia Mwema Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alithibitisha ofisi yake kutowahi kupokea maombi ya halmashauri hiyo kununua magari hayo.
“Sisi hatuna maombi yao, kimsingi maombi hayo yalipaswa kupitia ofisi ya RAS (Katibu Tawala) na hawakufanya hivyo na hiyo maana yake ni kukaidi maagizo ya serikali (Waziri Mkuu),” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Gallawa aliongeza kusema: “Sisi mkoa ndiyo tunaopaswa kupitisha maombi yao baada ya kujiridhisha kuwa kuna umuhimu wa magari husika kununuliwa na pia ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa maagizo yaliyotolewa na serikali yanasimamiwa ipasavyo”.
Alisema suala hilo wataliwasilisha kwenye mamlaka husika kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Waziri Mkuu, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika na akuonya akisema; “muda wa watumishi wachache kuichezea serikali umepita.”
Alisema umefika wakati kwa watumishi serikalini kutumia hekima na busara katika kufanya uamuzi kwa sababu, katika hatua ya mwisho serikali itahukumiwa na wananchi kutokana na uamuzi wao na watakaondamwa ni Rais na Waziri Mkuu



Post a Comment